WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO SITA UTEKELEZAJI OPERESHENI YA ANUANI NA MAKAZI

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi zote zenye dhamana ya masuala ya ardhi na makazi kuhakikisha zinakuja na mikakati thabiti ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi iliyoainishwa wakati wa utekelezaji wa zoezi la operesheni ya anuani na makazi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa operesheni anwani za makazi, Katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Juni 18,2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa wito huo leo Jumamosi Juni 18, 2022 wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa zoezi la operesheni ya anuani na makazi, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

“Pia toeni miongozo ya namna bora ya kushughulikia changamoto za Watanzania wenzetu kuishi katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria Ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na fursa zitokanazo na zoezi hili”.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi katika ngazi zote hususan kwenye Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utunzaji wa mifumo sambamba na kulinda miundombinu ya anwani za makazi kwenye maeneo yao.

“Viongozi na Watendaji hakikisheni kuwa jamii inaendelea kuelimishwa ili kujua manufaa sanjari na kutumia fursa zitokanazo na uwepo wa anwani za makazi katika maeneo yao”.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara zote, Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kuendelea kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa operesheni anwani za makazi na kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu.

“Mpango wa Uendelezaji wa Mfumo (System Sustainability Framework) unaotoa mwongozo wa shughuli zote za anwani za makazi zitakavyofanyika utumike vizuri ili kufanya zoezi hili kuwa na thamani wakati wote”

Naye, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleimani Abdulla amesema ni matarajio ya watanzania kuwa kukamilika kwa operesheni ya anuani na makazi kutasaidia kuongeza uwezekano wa kuendelea kukuza uchumi kuwa kidijitali.

kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kuwa hadi kufikia Mei 31, 2022 kupitia operesheni ya anuani na makazi taarifa na anuani za makazi 12,385,956 zilikusanywa sawa asilimia 106.94 ya lengo lililokusudiwa “hii ni zaidi ya lengo tulilojiwekea awali la kukusanya taarifa na kutoa anuani za makazi 11,582,106”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news