ZAMBIA YAJIFUNZA MENGI KUTOKA SEKTA YA MADINI NCHINI TANZANIA

NA TITO MSELEM-WM

WAZIRI wa Madini na Maendeleo ya Migodi wa Jamhuri ya Zambia Paul Kabuswe amesema amejifunza mambo mengi yanayofanyika katika kusimamia na kuendeleza sekta ya madini nchini Tanzania.
Waziri Kabuswe, ametoa kauli hiyo alipotembelea mgodi wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wa Nholi uliopo wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kwa lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kupiga hatua kwenye sekta ya Madini hususan kwenye usimamizi wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu. 
Aidha, Kabuswe amesema Tanzania wamepiga hatua kubwa hususan kwenye teknolojia ya uchimbaji mdogo wa madini ambapo ameahidi kurudi tena nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi mnyororo mzima wa shughuli za madini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema alifanya ziara nchini Nigeria ambapo sekta ya Madini Tanzania ilikuwa ikitolewa mfano wa kuigwa kwa nchi za Afrika kwa namna ilivyoweza kusimamia sekta ya Madini hususan katika kurasimisha sekta ndogo ya uchimbaji madini ambapo imepelekea wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kupitia mfumo ulio rasmi ambapo Serikali inaweza kufuatilia shughuli zao mpaka hatua ya kuuza madini yao kwenye masoko ya madini.
Dkt. Kiruswa amesema nchi ya Zambia inatarajia kufanya marekebisho ya Sera na Sheria zake za madini hivi karibuni ambapo imeona bora kufika Tanzania kujifunza namna wachimbaji wadogo wanavyofanya shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji, uongezaji thamani na usafirishaji wa madini. 

Aidha Dkt. Kiruswa amesema kuwa, ili sekta ya Madini ilete tija kwa nchi ni muhimu ikasimamiwa kikamilifu kwa kuweka mifumo imara itakayosaidia nchi na wananchi wake kunufaika na rasilimali madini zao hususan kwenye kukuza uchumi wa nchi.

Awali Waziri Kabuswe na Dkt. Kiruswa walitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ambapo Mtaka alimpongeza Waziri Kabuswe kwa uamuzi wa kuja kujifunza shughuli za na biashara zima za madini nchini Tanzania.
Waziri Kabuswe aliongozana na ujumbe kutoka Zambia ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Musina Sakwiba, Mhandisi wa Migodi Elite Mhore na Afisa Mipango Mwandamizi Pamela Nakombe.

Post a Comment

0 Comments