DC Shekimweri:Tupo tayari kuadhimisha Siku ya Mashujaa

NA DENNIS GONDWE

WAKAZI wa Wilaya ya Dodoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa itakayofanyika katika Uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na mamia ya wakazi wa Dodoma katika soko kuu la Majengo baada ya kuongoza zoezi la usafi wa mazingira.

Shekimweri alisema, “Jumatatu tarehe 25 Julai, 2022 ni siku ya Mashujaa. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atashiriki nasi katika kuadhimisha siku hiyo kwenye Mnara wa Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa jijini hapa. Jumapili kuamkia Jumatatu, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka atawasha Mwenge pale kwenye Mnara wa Mashujaa.

"Na usiku Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma atakwenda kuzima Mwenge huo kwa dhamana yake”.

Alisema kuwa, Mkuu wa Mkoa katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari aliwaomba wananchi kujumuika nae na kuonesha mapenzi kwa Rais.

“Kuanzia saa 1:00 asubuhi tuwe tumefika pale uwanja wa Mashujaa. Ni ratiba kama ya saa tatu na baada ya ratiba hiyo watu wataendelea na majukumu yao,”alisema Shekimweri.

Post a Comment

0 Comments