Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Tangini Kibaha yapata viongozi wapya

NA ROTARY HAULE

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tangini Kibaha Mkoani Pwani imepata viongozi wapya watakaoongoza Jumuiya hiyo kwa muda wa miaka mitano ijayo huku Jeremiah Komba (SHUNGU) akifanikiwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti.
Viongozi hao wamepatikana kufuatia uchaguzi uliofanyika katika kata hiyo ukiwa chini ya msimamizi Nobert Masebe kutoka CCM Wilaya ya Kibaha pamoja na wazee maarufu akiwemo Frank Kalua na Edson Lutumo.

Vita vikali katika uchaguzi huo ilikuwa ni juu ya nafasi ya mwenyekiti iliyokuwa na wagombea watatu akiwemo Jeremiah Komba(Shungu) aliyekuwa anatetea nafasi yake,Mariam Kapinga na Mary Msuya.

Lakini hatahivyo Komba alifanikiwa kuwabwaga wapinzani wake kwa kupata kura 33 dhidi ya wapiga kura 45,huku Kapinga akipata kura 11 na Msuya akiambulia kura 1, matokeo ambayo yaliwashangaza baadhi ya WanaJumuiya na WanaCCM waliofika ukumbini hapo wakitaka kushuhudia namna Komba anavyogaragazwa katika uchaguzi huo.
Akitangaza matokeo hayo Msimamizi wa uchaguzi huo Nobert Masebe,alimtangaza Jeremiah Komba kuwa mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwakuwa ndiye mgombea pekee aliyepata kura nyingi kushinda wenzake.

"Mmeona uchaguzi ulikuwa wa wazi na tumehesabu kura kwa uwazi kila mmoja akiwa anaona,hivyo kwa maana hiyo mshindi wa uchaguzi huu ni mshindi wa haki nami kwa mamlaka niliyopewa namtangaza Jeremiah Komba kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Tangini,"amesema Masebe.

Aidha,katika nafasi ya Katibu wagombea walikuwa watatu akiwemo Jacob Kadelema,Heri Lukando na Oscar Mapinduzi lakini Masebe alimtangaza Jacob Kadelema kuwa mshindi kwa kupata kura 23 dhidi ya Heri Lukando (11) huku Oscar Mapinduzi aliyepata kura 1.

Nafasi ya Halmashauri Kuu ya Kata wagombea walikuwa wawili akiwemo Lazaro Biya na Theresia Kisisiwe lakini Lazaro Biya ameibuka kuwa mshindi kwa kupata kura 31 dhidi 12 lakini hatahivyo Biya alishinda tena katika nafasi ya uwakilishi Jumuiya Wazazi kwenda vijana akipata kura 35 dhidi ya mpinzani wake Neema Robert aliyepata kura 8.
Nafasi nyingine ni pamoja na mjumbe wa mkutano mkuu Mkoa iliyochukuliwa na Lazaro Benjamin, wakati nafasi ya wajumbe wa Baraza walioshinda ni Fatuma Mondwe,John Mafuta na Theresia Kisisiwe huku nafasi ya kutoka Wazazi kwenda UWT aliyeshinda ni Mwanahamis Msuya.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo mwenyekiti Jeremiah Komba ,amewashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumpiga kura nyingi zilizotosha kuwa mshindi katika uchaguzi huo.

Komba,amesema kuwa hakuamini kama angeshinda katika uchaguzi huo kwakuwa kulikuwa na upinzani mkali lakini kitendo cha kumpa ushindi huo ni wazi kuwa wamempa heshima kubwa na kwamba lazima awatumike kikamilifu .
Amesema kuwa, uchaguzi umekwisha na washindi wamepatikana hivyo hakuna sababu ya kuendeleza makundi na kusema kuanzia sasa hataki kusikia makundi na kwamba wote waungane katika kukijenga chama.

"Jumuiya ya Wazazi Kata ya Tangini ipo imara na hakuna mtu wa kuichezea kama wanavyofikiri wao ,yeyote atakayetaka kuivuruga Jumuiya yao ni wazi kuwa ataanza kushughulikiwa yeye ili kusudi Jumuiya ibaki salama," amesema Komba.
Hatahivyo,Komba amewataka viongozi waliochaguliwa pamoja na wanachama wengine wa Jumuiya hiyo kuungana kwa pamoja katika kukisaidia Chama Cha Mapinduzi ( CCM)ili kiweze kushinda katika chaguzi zake zote za ndani na nje.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news