Mama Mariam Mwinyi aongoza mazoezi huku akitoa wito maalumu kwa wazazi

NA DIRAMAKINI

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi amewasisitiza wazazi kuwalinda, kuwasikiliza na kuwa karibu na watoto wao ili kuwakinga na janga la udhalilishaji.
Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi akiongoza matembezi ya mazoezi ya viungo ya kilimita tano yaliyoanzia katika viwanja vya Kinyasini na kumalizia katika viwanja vya Mnazi mmoja Wete,kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Salama Mbarouk na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said na kushoto kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe.Dkt. Saada Mkuya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi,Mhe.Hamza Hassan Juma.(Picha na Ikulu).

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo mara baada ya kumaliza mazoezi aliyoyaongoza ambayo yalianzia uwanja wa mpira Kinyasini hadi viwanja vya Mnazi Mmoja, Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kufanya mazoezi na wananchi kila mwisho wa mwezi.

Katika maelezo yake, Mama Mariam Mwinyi amesema kwamba, ni vyema watoto wakasikilizwa na kuacha kuwatolea ukali ama kuwa na muhali kwani wanaofanya vitendo hivyo ni watu wa karibu.

Amesisitiza kwamba, hapa nchini kwa ujumla bila ya udhalilishaji inawezekana na kuwataka wadau wote wa kupambana na janga hilo kushirikiana kwa pamoja katika kupiga vita suala hilo.

Amesema kwamba, jambo hilo ni baya na limekuwa likiathiri kwa kiasi kikubwa akili kwa wale waliofanyiwa vitendo hivyo, na kusisitiza haja kwa kuwafikisha wale wote waaofanya vitendo hicho kuwafikisha mbele ya sheria.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa, ni muhimu kuwalinda, kuwafundisha na kuwasikiliza watoto ili linapotokezea jambo baya kwao iwe ni rahisi kuwahadithia na kuweza kuchukua hatua za haraka.
Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi akiongoza wanamichezo katika mazoezi ya viungo yaliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Wete Pemba, baada ya kumalizia matembezi ya mazoezi ya viungo yaliyoazia katika viwanja vya Kinyasini na kumalizia katika viwanja vya Mnazi Mmoja Wete na kujumuika katika mazoezi ya pamoja ya viungo yaliyofanyika leo Julai 28,2022.(Picha na Ikulu).

"Kuna wakati mtoto anataka kukwambia jambo, lakini mzazi unakuwa mkali, tuishi nao kirafiki zaidi watatuambia majanga yote yanayowakuta,"amesema.

Amesema kuwa, ili kuondoa janga hilo la udhalilishaji ni vyema jamii ikaacha muhali na badala yake wawafichue wahalifu ili wachukuliwe hatua za kisheria.

"Wanaodhalilisha watoto wetu tunawajua, ni ndugu zetu wa karibu, jirani zetu na tunaoishi nao majumbani mwetu, hivyo tuwafichue ili tuondoshe janga hili,"alieleza.

Mwenyekiti huyo aliwataka wadau wote wanaohusika na masuala ya udhalilishaji kuwa na huruma, watumie lugha nzuri na stara kwani wengine wanashindwa kufika kwenye vyombo husika kuripoti kutokana na maneno mabaya.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amesema kuwa, katika jumuiya hiyo anayoiongoza imeweka makusudi mkakati wa kuhamasisha mazoezi Zanzibar nzima kwa lengo la kujenga afya ya mwili na akili kwa wananchi wake.
Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi akizungumza na wanamichezo wa vikundi vya mazoezi ya viungo yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Wete, baada ya kumaliza matembezi hayo na mazoezi ya pamoja ya viungo yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba leo.(Picha na Ikulu).

Amefafanua kuwa, ili kuwe na Taifa lenye afya bora ni lazima wananchi wake wafanye mazoezi kwani wataepukana na magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo, kisukari na shindikizo la damu.

"Faida nyingine ya kufanya mazoezi inajenga urafiki na maelewano, upendo na pia inaleta amani katika Taifa letu, jambo ambalo ni muhimu sana katika maisha yetu," amesema.

Aidha, amesisitiza haja kwa wananchi kudai risiti ya kielektroniki katika utaratibu mzima wa kununua na kuwataka wanaouuza kutoa risiti ya kielektroniki.

Sambamba na hayo, Mama Mariam Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuhesabiwa na kuwataka wananchi wajiandae ipasavyo kwa ajili ya kuhesabiwa siku itakapofika ya Agosti 23, mwaka huu.
Wanamichezo wa mazoezi ya viungo Mkoa wa Kaskazini Pemba wakimsikiliza Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi (hayupo pichani) akiwahutubia baada ya kumaliza mazoezi ya pamoja ya viungo yaliofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Wete Pemba leo.(Picha na Ikulu).

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma alieleza kwamba hatua hiyo inayoichukua Mama Mariam Mwinyi ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Leila Mohamed Mussa amesema, mazoezi ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga afya bora sambamba na kujiepusha na magonjwa mbalimbali.

"Tutaendelea kuungana ya taasisi yako ya Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa lengo la kuboresha michezo Zanzibar, kama Rais wetu Dkt. Hussein Mwinyi alovyodhamiria kuinua sekta ya michezo nchini,"amesema Waziri Lela.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amemshukuru Mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kufanya matembezi hayo katika mkoa wake na kuahidi kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanafanikisha malengo ya jumuiya hiyo.

“Mama tunakuahidi tuko pamoja na wewe na tutaendelea kushirikiana na wewe katika kuhakikisha malengo yako yanafanikiwa,”alieleza.

Naye Katibu Tawala Mkoa huo Ali Mohamed Mwinyi alisema kuwa, katika Mkoa wao kuna umoja na mshikamano ambapo wananchi wanashirikiana katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib kwa upande wake alimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa uwamuzi wake wa kuungana na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na kufanya nao mazoezi.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali waliungana na Mama Mariam Mwinyi akiwemo Mama Hasina Kawawa, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapindzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa huo, viongozi wa vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi na vikundi mbali mbali vya mazoezi.
Mazoezi hayo ni muendelezo wa ahadi yake aliyoitoa Mama Mariam Mwinyi mnamo Febuari 19 mwaka huu wakati akizindua taasisi yake ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF) ambapo aliahidi atakuwa championi na kinara katika kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kwa kuungana na wananchi kwa ajili ya kujenga afya kila mwisho wa mwezi katika Wilaya zote za Zanzibar.

Matembezi hayo ya leo ya kilomita tano yalianza katika viwanja vya Kinyasini hadi viwanja vya Mnazi Mmoja Wete, ambapo Mkoa wa Kaskazni Pemba ni wa nne kufanyika matembezi kupitia taasisi hiyo.

Post a Comment

0 Comments