Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo kwa manispaa

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Manispaa kubadilika na kutofanya kazi kizamani na badala yake zitafute fedha kwa ajili ya miradi kwenye maeneo yao hasa ya Mjini.
Rais Dkt.Mwinyi aliyasema hayo akiwa katika muendelezo wa ziara zake za wilaya aliyoianza juzi ambapo mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika jengo jipya la Wajasiriamali wa vifaa vya umeme na elektroniki zilizotumika (Used) lililopo Mombasa,Shehia ya Kwamchina, Jimbo la Kiembesamaki Zanzibar. 

Katika maelezo yake, Rais Dkt.Mwinyi alizitaka Manispaa kutafuta mikopo ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kujenga majengo ya kibiashara ikiwa ni pamoja na kumalizia ujenzi wa jengo hilo. 

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alizihakikishia Manispaa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukua dhamana katika kuhakikisha hilo linawezekana kwa ajili ya kwuasaidia wajasiriamali ili wawache kuuza bidhaa zao katika maeneo yasiyohusika yakiwemo katika hifadhi za barabara. 

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ameamua kujenga miradi hiyokwa kuona kwamba Zanzibar haina maeneo maalum ya kufanya shughuli za wajasiriamali na kueleza lengo la ujenzi huo ni kuwa na maduka ya kisasa. 

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alieleza azma ya Serikali anayoiongoza ya kufanya ukarabati wa barabara zote za Mjini ikiwa ni pamoja na kujenga njia za wapita kwa miguu, baskeli zenye taa, bustani pamoja na kujenga barabara za juu (flyover) katika mzunguko wa barabara ya Mwanakwerekwe na Amani. 

Alisema kwamba Serikali ina nia nzuri ya kuwawekea mazingira mazuri wajasiriamali kwa kuwajengea majengo yenye hadhi na yenye kuweza kufanya shughuli zao kisasa. 

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa (JKU), kwa juhudi zake inazozichukua katika kutekeleza vyema miradi ya ujenzi waliyopewa na kueleza kwamba uwezo wa kikosi hicho pamoja na kiwango kidogo cha gharama za ujenzi ndio sababu iliyoipelekea Serikali kuamua kuwapa zabuni ya ujenzi. 

Rais Dk. Mwinyi pia, aliweka jiwe la msingi katika skuli ya msingi ya Mwanakwerekwe inayojengwa na Kampuni ya Estim Enteprises Company Ltd kupitia fedha za UVIKO-19 na kumtaka Mshauri Elekesi kumsimamia Mkandarasi ili kuhakikisha ujenzi huo unamaliza kwa mda uliopangwa. 

Aliongeza kwamba hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea bila ya watu wake kuwa na elimu nzuri. 

Alisema kuwa skuli hiyo ya msingi ni ya kipekee ambayo ina maabara, chumba cha kompyuta, ofisi ya mwalimu mkuu ya kisasa na kuwataka walimu kuendelea kufanya kazi zao vizuri kwani Serikali imeshawawekea mambo yao mazuri mwishoni mwa mwezi huu wao pamoja na watendaji wengine wote wa Serikali. 

Hata hivyo, aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha mara tu baada ya kumaliza kwa ujenzi wake iwekewe vifaa vyote muhimu. 

Mapema, akiweka jiwe la msingi la Hospitali ya Wilaya huko Shehia ya Jitimai Mwanakwerewe, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba lengo la Serikali ya Awamu ya Nane ni kuzifanya huduma za afya kubwa bora zaidi. 

Alisema Serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha inajenga hospitali zenye hadhi katika Wilaya zote kwa lengo la kuimarisha huduma za afya na kuleza kwambahospitali hiyo itakuwa ikitoa huduma zote muhimu za afya ambazo zitakuwa za kisasa zikiwemo huduma za upasuaji. 

Alimtaka Mkandarasi kuhakikisha mwezi wa Septemba anakabidhi jengo hilo na kumtaka afanye kazi usiku na mchana huku akiiagiza Wizara husika kuhakikisha mazingira ya nje ya hospitali hiyo yanawekwa vizuri ikiwa ni pamoja na kuweko kwa huduma ya maji ya uhakika. 

Rais Dk. Mwinyi alitoa agizo kwa uongozi wa Mkoa, Wilaya pamoja na Wizara ya Habari, Vijana Michezo na Utamaduni kuhakikisha inaujenga na kuuwekea mazingira mazuri uwanja wa michezo katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuuwekea nyasi za bandia na kuhakikisha unachezeka wakati wote. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news