'Serengeti tuwakekete mabinti kwa kuwapa elimu bora si kuwapeleka kwa mangariba'

NA FRESHA KINASA

"Na polisi wakimkamata wamfikishe mahakamani kabisa maana hatakuwa na kisingizio, kwani elimu amepata tena ya kutosha. Tuache tamaa ya pesa kwamba binti akeketwe ili mzazi apate pesa,zama hizi urithi pekee wenye faida ni elimu, ndugu zangu wana Serengeti tuwakekete mabinti kwa kuwapa elimu bora na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma wafikie ndoto zao;

Hayo yamesemwa na wananchi kupitia elimu inayoendelea kutolewa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Serengeti.

Ni wakati wakizindua kampeni ya utoaji wa elimu kupitia mikutano ya hadhara kuhusiana na madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia. 
Ambapo elimu hiyo itatolewa katika kata 22 sambamba na kuwahimiza wananchi wajitokeze kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022. 

Kampeni hiyo imezinduliwa Julai 11, 2022 ambapo elimu hiyo ilitolewa kwa wananchi wa kata ya mbalibali na Machochwe ambapo Afisa Mwelimishaji Jamii Madhara ya Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuel Goodluck.

Sambamba na maafisa kutoka Jeshi la Polisi akiwemo (CPL) Sijali Nyambuche kutoka Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti, na (SSGT) Titus Mufuluki kutoka Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Serengeti, OCD (SSP) Mathew Mgema walitoa elimu hiyo na kuhamasisha wananchi wajitokeze kuhesabiwa Agosti 23, mwaka huu ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo. 

Emmanuel Goodluck ni Afisa Mwelimishaji Jamii Madhara ya Vitendo vya ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania amesema, kupitia zoezi la pamoja la utoaji wa elimu litaimarisha ushiriki wa jamii katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani ukeketaji ambao mwaka huu koo mbalimbali za kabila la Kikurya zimejipanga kukeketa wakati wa likizo kutokana na mwaka kugawanyika kwa mbili. Hivyo lazima elimu iwe chachu ya kuleta ufanisi katika kutokomeza vitendo hivyo. 

"Tunafikisha elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji kuona kwamba wasichana ambao hufanyiwa ukatili huu wanakuwa salama kipindi ambacho kiko mbele cha likizo. Wazazi wengi na walezi hutumia mwanya huo kuwakeketa mabinti wakiwa nyumbani.

"Shirika kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Serengeti tumeona tufikishe elimu kwa wananchi kwa njia ya mikutano ya hadhara, watu watambue madhara ya ukeketaji, ndoa za utotoni, ubakaji na pia kuwahimiza washiriki kupinga ukatili ikiwemo kuwafichua mbele ya sheria wanaofanya vitendo hivyo," amesema Goodluck. 

Aidha, Goodluck amesema kuwa, Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linaendelea kutoa hifadhi kwa wasichana waliopo kituo cha Nyumba Salama Hope Mugumu baada ya kukimbia ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao, kuwaendeleza kielimu wafikie ndoto zao, kuwahudumia mahitaji yao ya msingi, kuwajenga kisaikolojia pamoja na kuwafundisha haki zao na stadi za maisha.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Serengeti (OCD), SSP Mathew Mgema akizungumza wakati wa utoaji wa elimu kwa wananchi wa Kata ya Machochwe na Mbalibali aliwataka wananchi hao kuunga mkono juhudi za serikali katika kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni. 

Huku akisisitiza kuwa kila mwananchi awe sehemu ya kushiriki kupambana na vitendo hivyo ikiwemo kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya ukeketaji Polisi, Dawati la Jinsia, na katika ofisi za serikali ili kuwalinda watoto wa kike wasifanyiwe ukatili huo.

Pia, SSP Mgema amewaambia wananchi hao kuwa, Jeshi la Polisi wilayani humo litawachukulia hatua kali za kisheria watakaokaidi na kufanya vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Aidha, amewataka wananchi wote kuwathamini watoto wa kike na wa kiume kwa kuwapa fursa sawa ya elimu kwani kufanya hivyo kutawezesha pia kupunguza vitendo vya kihalifu katika jamii na kuandaa kizazi kitakacholeta maendeleo kwa jamii na taifa pia. 

Aidha, OCD Mgema amewahimiza wananchi wa kata hizo na Serengeti kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 23, mwaka huu ili kuiwezesha serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi na kwamba sensa ni muhimu sana kila mmoja ashiriki kwa ufanisi. 
Naye CPL Sijali Nyambuche kutoka Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti akizungumza na wananchi hao, amewataka kutowafumbia macho waliojipanga kufanya ukeketaji kipindi cha likizo bali wawaripoti. 

Huku akisema wazazi na walezi waweke mkazo katika kuwasomesha watoto wa kike na sio kuwakeketa kwani wakipata elimu na kufikia ndoto zao jamii nzima itaneemeka. 
Akizungumzia madhara ya ukeketaji, SSGT Titus Mufuluki kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti amesema, ukeketaji una madhara ikiwemo kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi kutokana na kutumia kifaa kimoja wakati wa kukeketa.

Pia kuchangia ndoa za utotoni kwani binti anapokeketwa huandaliwa kuozeshwa, madhara ya kisaikolojia, kupoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi na hivyo amewataka Wananchi hao kutambua madhara hayo na waachane na mila hiyo. 

Wakitoa maoni yao juu ya zoezi hilo wakati wakiongea na DIRAMAKIMI, Neema Mwita na Ester Paul ambao ni wakazi wa Kata ya Mbalibali wamesema, elimu hiyo wameipokea kwa shukurani na kulipongeza Jeshi la Polisi Wilaya ya Serengeti na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kutoa elimu hiyo kwa umoja, ambapo wamesema elimu hiyo itakuwa chachu ya kuleta hamasa kwa wananchi kuunga mkono juhudi za mapambano ya ukeketaji na aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia. 

"Elimu ya madhara ya ukeketaji imetolewa kwa upana wake, elimu ndio njia muhimu sana ya kumaliza ukeketaji naamini kila aliyehudhuria katika mkutano huu amepata faida, na pia niombe wananchi wenzangu tuyazingatie yaliyosemwa. 

"Tuache ukeketaji tumesikia madhara ni mengi na pia baadhi yetu tumeshuhudia wengine waliokeketwa walipata madhara kama vile ulemavu. Kupitia elimu hii niombe tuwe mabalozi wa kuwaelimisha wenzetu ambao hawafahamu madhara haya kusudi tuwalinde mabinti zetu na tuwasomeshe kwa juhudi kwani ni viongozi wa baadaye,"amesema Neema Mwita. 

"Tumeona Polisi wanatoa elimu hii tena kwa njia shirikishi kabisa, ninaamini kabisa kupitia elimu hii iliyotolewa mzazi aliyekuwa hapa mkutanoni akienda kumkeketa binti yake huyo anastahili adhabu kali sana. 

"Na polisi wakimkamata wamfikishe mahakamani kabisa maana hata kuwa na kisingizio kwani elimu amepata tena ya kutosha. Tuache tamaa ya pesa kwamba binti akeketwe ili mzazi apate pesa,zama hizi urithi pekee wenye faida ni elimu, ndugu zangu wana Serengeti tuwakekete mabinti kwa kuwapa elimu bora na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma wafikie ndoto zao,"amesema John Paulo mkazi wa Mbalibali.

Post a Comment

0 Comments