Serikali yaendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya maendeleo Nyakahanga wilayani Karagwe

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali kupitia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tayari imetenga shilingi milioni 405 za kutengeneza barabara ya Bisheshe-Kashanda-Omurusimbi katika Kata ya Nyakahanga ili iweze kupitika nyakati zote.
Mheshimiwa Bashungwa amesema hayo Julai 12, 2022 katika mikutano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kijiji cha Bisheshe na Mato Kata ya Nyakahanga na kueleza kuwa, barabara hiyo imekuwa kilio kikubwa cha wananchi ya kata hiyo kwa muda mrefu.

Amesema, barabara hiyo itatengenezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) na itawezesha wananchi kupata huduma nzuri ya barabara hasa kwa kipindi cha mvua ambacho wananchi walikuwa wakisumbuka sana.

Aidha, Bashungwa amemuagiza Meneja wa Maji RUWASA Wilaya ya Karagwe kuhakikisha anasisimamia vizuri utekelezaji wa mradi wa maji Bisheshe na Rwandaro na ukamilike ndani ya miezi mitatu kulingana na mkataba wa utekezaji wa mradi huo.
Pia, ameeleza kuwa Serikali italeta kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Mato kilichopo Kata ya Nyakahanga na kumaliza kero hiyo.

Vilevile, ameeleza kumekuwa na changamoto ya barabara ya Kihanga-Bujuruga-Mato-Kibogoizi mpaka Rugu lakini sasa mkandarasi anaendelea na kazi ya kumwaga vifusi vya changarawe na kuhakikisha barabara hiyo ya mkakatiti inatengenezwa vizuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news