TANROADS yaanza kuchukua tahadhari maeneo korofi Morogoro

NA DIRAMAKINI

WAKALA wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Morogoro umeanza kuchukua tahadhari kwenye maeneo yote korofi ya barabara na madaraja kwa kukagua uimara wake ili yafanyiwe kazi kabla ya msimu wa mvua kuanza ili kuepusha maafa na usumbufu kwa watumiaji wa barabara.
Akizungumza katika daraja jipya la Kiyegeya lililopo Kata ya Berega wilayani Kilosa katika Barabara Kuu ya Morogoro-Dodoma, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema ukaguzi huo unalenga kujiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana majanga ya mafuriko ambayo hutokea wakati wa msimu wa mvua.

Licha ya ukaguzi huu meneja wa TANRODS Mkoa wa Morogoro alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha fedha za kutosha Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara.

Aidha, amewatoa hofu watumiaji wa barabara hiyo kuwa daraja Kiyegea kwa sasa lipo imara na hawategemee mvua yoyete itakayoweza kubomoa miundombinu ya ilipo. 

Msimamizi wa ujenzi wa Daraja la Kiyegea kutoka kampuni ya ujenzi ya CGI, Krsto Ilic alisema kabla ya ujenzi wa daraja hilo hali ilikuwa mbaya kwani ilikuwa ni moja ya sehemu hatari zinazosababisha msongamano na ajali za barabarani kutokana na ubovu wa mundombinu yake.

Krsto alisema kuwa, daraja lililojengwa pamoja na uimara wake lakini mvua zilizonyesha msimu huu licha kuwa nyingi hazikuweza kuleta madhara katika daraja hilo.

Nao baadhi ya wakazi wa eneo la Kiyegeya akiwemo Pius Digati wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kukamilisha kwa wakati ujenzi wa daraja hilo kwani tangu kubomoka kwa daraja hilo walikuwa wanapata adha ya usafili kutokana na msongamano.

Daraja la Kiyegeya katika Barabara Kuu ya Morogoro- Dodoma lilobomoka Machi 2, 2020 kutokana na mvua zilizokuwa zimenyesha mwaka huo na baadaye kutengenezwa daraja la muda lililowezesha magari kupita kwa kupokezana kwa zamu.

Katika kuwezesha hatua za awali ili kurejesha mawasiliano, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ilinunua makalavati makubwa 120 ya zege kutoka Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki inayojenga mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam – Makutupora na kujenga daraja la muda na njia ya mchepuko.

Barabara kuu hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi pamoja na nchi za maziwa makuu zikiwemo za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi ambazo bidhaa zake zinapitishwa kwenye barabara hiyo na inapotokea imekatika kunachangia kuzorotesha ukuaji wa uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news