Tuungane kwa pamoja kupinga ukatili kwa watoto, wanawake asema Rhobi Samwelly

NA FRESHA KINASA

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu katika Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesema ushirikiano wa pamoja ni muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
"Tuungane kwa pamoja kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake, vitendo vya ulawiti na kila aina ya unyanyasaji ili kuimarisha ustawi bora na usawa wa Kijinsia katika Jamii na Taifa kwa ujumla. 

"Watoto wa kiume na wa kike wazidi kupewa fursa sawa ya kupata elimu kusudi waje kuwa msaada kwa jamii inayowazunguka kwa kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii. Tujikite kuwafundisha na kuwarithisha mila zinazofaa ambazo ni muhimu katika jamii yetu, sambamba na maadili mema kwa manufaa ya nchi yetu.

"Kila mmoja aone mtoto wa mwenzake ni mwanaye na hivyo akiona mtoto wa mwenzake anakengeuka ama anataka kufanya jambo baya lazima atashiriki kumkanya na kumrejesha katika mstari unaofaa na hatua hii itapunguza vitendo vya kihalifu ambavyo wasiposimamiwa vyema wanaweza kujiingiza huko na kuwa mwiba katika jamii,"amesema Rhobi. 
"Tuwalinde watoto wa kiume na wa kike na tuwathamini na tuwaandae kuja kuwa viongozi wa kesho kwa kuwajengea msingi bora wa kufikia ndoto zao kuanzia sasa."amesema Rhobi Samwelly Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania wakati akizungumza na DIRAMAKINI.

Post a Comment

0 Comments