Wasimamishwa kutoa huduma za uuguzi na ukunga kwa kukiuka maadili

NA GODFREY NNKO

MSAJILI Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi.Agnes Mtawa amewasimamisha kutoa huduma za uuguzi na ukunga,John Chuma (RN) wa Zahanati ya Boheloi iliyopo Lushoto mkoani Tanga na Maclina Gwido Mduda (EN) wa Zahanati ya Mtibwa iliyopo Manispaa ya Subawanga mkoani Rukwa kuanzia leo Julai 6,2022.

Wawili hao wamesimamishwa kwa muda wa miezi mitatu wakati mashauri yao yakishughulikiwa na Baraza kisheria na kitaaluma.

"Kwa mamlaka niliyokabidhiwa kwa mujibu wa kanuni 7(1) ya Fitness’ to practice nawasimamisha kutoa huduma za uuguzi na ukunga ndugu John Chuma (RN) wa Zahanati ya Boheloi iliyopo Lushoto Tanga na Maclina Gwido Mduda (EN) wa Zahanati ya Mtibwa iliyopo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa,"ameeleza Msajili huyo.

Amesema, amefikia hatua hiyo baada ya watu hao kwa nyakati tofauti kushindwa kuzingatia Maadili na Miongozo ya Kitaaluma wakati wa kutoa huduma na kusababisha madhara kwa akina mama waliofika kujifungua. 

Msajili huyo amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 kifungu cha 25 (2)(a) na kifungu cha (3)(f) (k) pamoja na Kanuni na Misingi ya Maadili ya Kitaaluma ya Wauguzi na Wakunga Tanzania,kifungu hicho kinakataza kutelekeza wagonjwa wanaohitaji huduma, na jamii inapaswa kupata huduma zilizo salama, zenye ubora na staha.
Msajili Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi.Agnes Mtawa.

Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka ya Kisheria iliyoanzishwa kwa ajili ya usimamizi wa taaluma na wanataaluma ya Uuguzi na Ukunga nchini. 

Lengo la kuanzishwa chombo hiki ni kuhakikisha jamii inapata huduma zilizo bora na salama kutoka kwa wauguzi na wakunga. Baraza linafanya kazi chini ya Sheria ya Uuguzi na Ukunga ,yaani The Nursing and Midwifery Act of 2010.

"Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania litaendelea kuchukua hatua kwa wale wote watakao kiuka na Maadili na Miongozo popote walipo ikiwemo kuwafutia usajili na kunyang’anya leseni zinazowaruhusu kutoa huduma za Uuguzi na Ukunga nchini,"amesema.

Post a Comment

0 Comments