Waziri Balozi Mulamula ashiriki Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa AU

LUSAKA-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) yupo jijini Lusaka, Zambia kushiriki Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza tarehe 14 jijini humo.
Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) ukiendelea jijini Lusaka, Zambia.

Mkutano huo wa siku mbili umepokea na kujadili taarifa za kiutendaji za Taasisi za Umoja wa Afrika ikiwemo Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (Mabalozi) kwenye Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Afrika katika kipindi cha Februari-Juni 2022.

Mkutano huo pia utapitisha Bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2023 pamoja na bajeti ya kifungu cha utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika yaliyopitisha Kiswahili kuwa Lugha ya Kazi ya Umoja huo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaoendelea jijini Lusaka, Zambia.

Katika mkutano huo Waziri Mulamula anatazamia kusisitiza Kamisheni ya Umoja wa Afrika kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa maamuzi ya Kiswahili kuwa Lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika, kuhimiza matumizi sahihi ya rasilimali fedha na kusisitiza umuhimu wa uwazi na usawa kwenye mchakato wa ajira ili kuwezesha Watanzania kupata ajira kwenye umoja huo. 

Mkutano huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje utafuatiwa na Mkutano wa 4 wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 17 Julai 2022. 

Kamati hiyo inaundwa na nchi za Senegal (Mwenyekiti); Libya (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti); Angola (Makamu wa Tatu wa Mwenyekiti); Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Katibu) na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya za Kikanda za Umoja wa Afrika. 
Picha ya pamoja ya Mawaziri, Viongozi waandamizi wa Serikali, Taasisi mbalimbali za Kimataifa na Watendaji wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea jijini Lusaka, Zambia.Umoja wa Afrika una Jumuiya nane za kikanda ambazo ni Arab Maghreb Union (AMA), COMESA, Community of Sahel-Saharan States (CEN-SAD), EAC, ECCAS, IGAD na SADC.

Waziri Mulamula katika Mkutano huo ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Hassan Simba Yahya, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Shiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi wa Sheria Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Balozi Caroline Chipeta na Maafisa wengine Waandamizi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news