WAZIRI BITEKO AWATAKA WACHIMBAJI WA MADINI KUTUMIA VIWANDA VYA NDANI KUSAFISHA DHAHABU

NA STEVEN NYAMITI-WM

SERIKALI imewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kusafisha dhahabu katika viwanda vya ndani badala ya kuuza malighafi kwenye viwanda vya nje.
Rai hiyo imetolewa leo Julai 7, 2022 na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko alipotembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) cha mkoani Geita.
Amesema, kwa sasa atakayekwenda kuuza dhahabu ghafi kwenye kiwanda cha kusafisha dhahabu atalipa mrabaha asilimia nne badala ya asilimia sita ili wachimbaji wapate nafasi ya kusafisha katika viwanda hivyo.
"Ni muhimu sasa dhahabu tunayoichimba wenyewe iweze kusafishwa hapa iende ikiwa bidhaa ya mwisho,"amesisitiza.

Aidha, Dkt.Biteko amesema, kiwanda cha GGR kitatengemeza ajira kwa Watanzania pamoja na kulipa kodi husika ili Serikali iweze kukusanya mapato.
Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko ameupongeza mkoa wa Geita kwa usimamizi wa Sekta ya Madini. Amesema, mkoa unasimamia vizuri fedha zinazotolewa katika huduma za kijamii ambayo imesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya mkoa kupitia Sekta ya Madini.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa Geita, Said Nkumba amesema, kiwanda hicho kinakwenda kutangaza mkoa katika Sekta ya Madini. Amesema, wafanyabiashara wa madini na wachimbaji wadogo watumie nafasi hiyo kupeleka madini yao kusafishwa dhahabu katika kiwanda cha GGR ili manufaa yaweze kubaki katika mkoa wa Geita na nchini kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Jimbo la Geita, Constantine Kanyasu amempongeza Mama Masasi kwa kujenga kiwanda hicho katika mkoa huo. 

Amesema, kiwanda hicho ni mkombozi wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kwa mkoa ili waweze kusafisha dhahabu katika ubora wa kimataifa.

Hadi sasa Serikali ina viwanda vya kusafisha dhahabu katika mkoa wa Mwanza na Dodoma ambavyo wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ndani na nje nchi hupeleka madini kwa ajili ya kusafishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news