Waziri Mkuu asisitiza umuhimu wa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania, atoa angalizo

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni na kuwataka watu wote wanaojihusisha na vitendo viovu vinavyokiuka misingi ya maadili waache mara moja na badala yake waamue kuishi kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Fatuma Mtanda (wa pili kushoto) wakati alipotembelea banda la Mkoa wa Mtwara baada ya kufungua Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni kwenye uwanja wa Uhuru, Temeke Mkoani Dar es salaam.

“…kwa kuwa suala zima la maadili linaanzia katika ngazi ya familia na jamii, ninatoa wito kwa wazazi na walezi, taasisi za dini, machifu na wadau wengine, kuendelea kukemea uovu huo na kuwafunza watoto na vijana wetu maadili mema ili kukilinda kizazi chetu cha sasa na kijacho.” 

Waziri Mkuu amefungua tamasha hilo leo (Jumamosi, Julai 02, 2022) katika Uwanja wa Uhuru, Temeke mkoani Dar Es Salaam. Amesisitiza kuwa kuwa familia ni kitovu cha makuzi na malezi kwa watoto na vijana. “Familia ni asasi ya msingi na muhimu katika mfumo wa jamii na hivyo inaweza kuendeleza maadili, malezi na urithishaji wa utamaduni wetu wa Kitanzania.” 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa (katikati) wakifurahia ngoma wakati Waziri Mkuu alipofungua Tamasha la Kwanza la Utamaduni kwenye Uwanja wa Uhuru, Temeke Mkoani Dar es salaam, Julai 2, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michewzo, Dkt. Hassan Abbas. 

Waziri Mkuu amesema walezi na wazazi wanatakiwa wajifunze kutilia maanani malezi ya watoto kwa kutenga muda wa kukaa na watoto na vijana na siyo kuziachia shule peke yake. “Tushirikiane na Serikali, taasisi za dini na wadau wengine, kukemea mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu.” 

Waziri Mkuu amewataka vijana wote wa Kitanzania waache kuendekeza tabia ya kutumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii kwa kusoma au kuangalia mambo ambayo hayaongezi thamani ya maisha yao na badala yake watumie muda huo kufanya kazi. “Tutumie mitandao kutafuta maarifa yanayofaa na tujikite zaidi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.” 

“Kwa kuwa maadili ni chimbuko la uzalendo na utu wetu, ninaitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuongeza jitihada katika kuandaa programu za elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kuthamini mila na desturi zetu, pamoja na uzalendo, ili tutengeneze kizazi kinachozingatia maadili mema. Tusikubali kamwe kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni.” 
Baadhi ya washiriki wa Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua tamasha hilo kwenye uwanja wa Uhuru, Temeke mkoani Dar es salaam.

Amesema jukwaa mojawapo ambalo wizara hiyo inaweza kuanza nalo ni kuandaa mdahalo wa kitaifa kuhusu mmomonyoko wa maadili, ambapo wanaweza kupata picha halisi ya hali ya maadili ilivyo nchini kwa sababu watakutanisha makundi mbalimbali. 

“Programu nyingine ni kuunda kablu za maadili katika shule za msingi na sekondari. Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) wana klabu ambazo zinawaelimisha wanafunzi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa. Kwa hiyo na nyinyi Wizara kwa Kushirikiana na TAMISEMI igeni mfano huo mzuri.” 

“Nyote mtakubaliana nami kwamba hali ya mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu ni mbaya sana kwa rika zote. Mlezi wetu namba moja Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mama mlezi wa familia anaguswa sana jambo hili ambapo, katika hotuba zake nyingi haachi kugusia suala la maadili.” 

“Vilevile, tumeshuhudia baadhi ya vitendo viovu vingi kama vile kuongezeka kwa vitendo vya watoto kuwauwa wazazi wao; ulawiti; wanawake kuuwawa na waume zao; ubakaji hususani kwa watoto na wanafunzi; watoto na vijana kutowaheshimu watu wazima hususani katika vyombo vya usafiri na kutumia lugha zisizofaa wanapozungumza na watu wazima; uvaaji wa mavazi yasiyo na stara hususani kwa wasichana na wavulana na matumizi ya madawa ya kulevya.” 

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa tamasha hilo, Waziri Mkuu amesema tamasha hilo limetokana na agizo la Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa akiwa mkoani Mwanza tarehe 8 Septemba, 2021 kwenye Tamasha la Utamaduni. “Mheshimiwa Rais alielekeza yafanyike matamasha ya utamaduni ya namna hii nchi nzima.” 

“Naiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, iandae mwongozo wa jinsi gani matamasha haya yataendeshwa. Pia ninaiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na wadau ambao wanaandaa matamasha ya Utamaduni. “ 

Pia, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa wadau wahakikishe wanaishirikisha Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wanapoandaa matamasha yao wahakikishe wizara husika inafahamu. “Si vema mdau unaandaa tamasha huku wizara yenye dhamana na utamaduni haifahamu kabisa au inafahamu dakika za mwisho.” 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha nakala za Mwongozo wa Maadili na Utamaduni wa Mtanzania baada ya kuuzindua katika Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Temeke Mkoani Dar es salam, Julai 2, 2022. Katikati ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Tameke, Joketi Mwegelo. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).

Akizungumzia kuhusu vyombo vya habari, Waziri Mkuu amesema vyombo vya habari vinatakuwa viwe walimu wema wa kuhakikisha maadili yanazingatiwa, visiwe chanzo cha mmomonyoko wa maadili. “Hakikisheni mnakagua kazi zenu kabla hamjazirusha hewani hususani filamu, muziki au programu zinazotoka nje ya nchi. 

Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema tamasha hilo ambalo linafanyika kwa siku tatu lilianzia jana Julai Mosi, 2022 litamalizika kesho Julai 3, 2022, limeandaliwa mahsusi katika wiki ya kuelekea siku ya Kiswahili Duniani ambayo kilele chake ni Julai 7, 2022. 

Amesema Tamasha hilo litachagizwa na shughuli mbalimbali zikiwemo mashindano ya ngoma za kitamaduni na vyakula vya asili pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali za kitamaduni. Kauli mbiu ya tamasha hilo inasema “Utamaduni wetu; tujiandae kuhesabiwa, kazi iendelee.” 

Amesema, moja ya matokeo tarajiwa la tamasha hilo ambalo limeshirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ni kuwepo kwa hamasa kubwa nchini ya kupenda, kuhifadhi, kulinda, kuendeleza mila na desturi ambazo ndio msingi wa maadili na utambulisho wa Taifa kwa ujumla. 

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alipokea matembezi ya utamaduni ambayo yalihusisha wananchi kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ambao walipita wakiwa katika magari ya wazi huku kila mkoa ukionesha na kucheza ngoma za utamaduni za mkoa husika.Tamasha hilo limejumuisha matembezi ya kiutamaduni (road carnaval) katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news