Waziri Prof.Mkenda adokeza siri ya Serikali kuwekeza katika elimu bora

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa dhati kuwekeza katika sekta ya elimu nchini ili iweze kutoa matokeo bora kwa Watanzania na mipango mbalimbali ya Serikali.
Prof.Mkenda ameyasema hayo leo Julai 29,2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika mkutano maalumu wa kikazi kati ya Wizara ya Elimu na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Amesema, nchi nyingi ambazo zimeendelea duniani bila kujali ukubwa au udogo wa kieneo, kigezo kikubwa ambacho kimetumika kufikia mafanikio yao ni uwekezaji mkubwa kupitia elimu na teknolojia.

"Nchi haziendelei kwa sababu ya rasilimali zake, bali kuwekeza katika elimu. Hivyo tunaendelea kufanya maboresho makubwa ili kuhakikisha tunafikia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu ya kuwekeza katika ubora wa elimu na upatikanaji wake.Na katika ubora utahakisi mahitaji katika maeneo husika,"amesema Prof.Mkenda.

Amesema,katika ubora ni kuhakikisha kile kinachotolewa shuleni kinakuwa na matokeo mazuri ili kuwapa maarifa wanafunzi ambayo yataweza kupanua ufahamu wao.

"Dhamira ni kuwa na elimu ambayo inamuandaa kila mmoja vizuri.Miongoni mwa mambo ambayo yanaendelea ni pamoja na mapitio ya sera, ambapo tuna sera mbili tunazifanyia mapitio,Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Sera ya Sayansi na Teknolojia.

"Pili ni sheria ya elimu ambayo tunataka iendane sambamba na sera, sheria ya COSTECH, suala la mitaala ambapo lazima iendane na sera.

"Kwanza tutahakikisha wanapatikana walimu, wakufunzi na wahadhiri wa kutosha, pia tunahitaji walimu, wakufunzi na wahadhiri ambao wana sifa stahiki. Miundombinu na vitendea kazi,"amesema Waziri Prof.Mkenda.

Wakati huo huo, Waziri Mkenda amesema kuwa, Serikali imetenga shilingi bilioni 570 kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi wa elimu ya juu kupata mikopo.

Amesema, kila mmoja ambaye anaomba mikopo hiyo kwa ajili ya kuendelea na masomo anapaswa kufuta taratibu ili kuhakikisha kuwa anapata mikopo hiyo kwa wakati.

Pia amesema,kuna shilingi bilioni 3 ambazo zimetengwa na Serikali kwa ajili ya wanafunzi ambao wamefanya vizuri sana katika masomo ya sayansi kupitia Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) ambao watachagua kusoma masomo ya sayansi

"Kigezo cha atakayepatiwa ufadhili huo ambao wengi wanataka uitwe Samia Scholar ni kufaulu vizuri katika masomo ya sayansi na upo tayari kuendelea kusoma masomo ya uhandisi,elimu tiba.Kwa sasa tunatoa udhamini huo kwa vyuo vya ndani tu,"amesema Prof.Mkenda.

Pia amesema, hivi karibuni wameongea na Benki ya NMB ambayo imekubali kuwa mstari wa mbele kuinua Sekta ya Elimu nchini kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaotoka kwenye familia zenye uhitaji.

Amesema, tayari Benki ya NMB imetenga kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa kuanzia katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuanza kutoa mikopo ya elimu.

Fedha hizo zitatolewa kwa utaratibu maalumu wa kibenki na kwa mujibu wa makubaliano rasmi kati ya wizara na NMB ambapo itatolewa kwa riba nafuu ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news