Aridhi yadhamiria kufanya mageuzi makubwa Sekta ya Milki na Nyumba nchini

NA ANTHONY ISHENGOMA-WANMM

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha kitengo kipya cha Uendelezaji Milki Nchini ili kwenda mbali zaidi kuandaa kanuni na sheria za kusimamia Sekta ya Milki na Nyumba ili kuboresha manufaa ya kiuchumi yatokanayo sekta hii.

Awali Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilijikita zaidi katika dhana ya uendelezaji nyumba zaidi bila ya kwenda kiundani kuangalia masuala yote yanayoendana na faida zilizopo katika Sekta ya Nyumba na sasa inatanua wigo zaidi kutunga kanuni na sheria zitakazowezesha upatikanaji wa taarifa kwa wateja nyumba ikilenga kuangazia uchumi zaidi katika uendelezaji milki na nyumba.
Hayo yamebainishwa Agosti 19,2022 na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uendelezaji Milki nchini, Lucy Kabyemela alipokutana na vyombo vya habari jijini Dodoma ili kutoa taarifa kwa umma kuhusu shughuli za uendelezaji Sekta ya Milki na Nyumba pamoja na mkutano wa wadau wa sekta hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 1 hadi 2 Septemba 2022.

Akifafanua zaidi kuhusu maana ya Milki  (Real Estate), Kabyemela amebainisha kuwa inaweza kutumika pia kumaanisha biashara ya kununua, kuuza au uwekezaji kwenye ardhi, nyumba na majengo kwa matumizi ya biashara.

Aidha, Kabyemela ameongeza kuwa moja ya kazi ya Kitengo cha Milki itakuwa ni kuwezesha wateja wa Nyumba kujua taarifa za gharama za kupanga nyumba tofauti na sasa ambapo anayechangia bei na upatikanaji wa taarifa hizi ni dalali wa nyumba ambaye ana mchango mkubwa kuamua bei ya pango la Nyumba.

Kwa mkutadha huu Wizara sasa itatoa sera na miongozo ikiwemo kutunga sheria ambazo zitatumika katika kusimamia masuala yote ya nyumba tofauti na awali ambapo taarifa au sheria hazikuwepo hivyo kuwezesha watu binafsi kufanya kazi bila uwepo wa sheria.

Kabyemela ameyataja malengo makubwa ya kuanzishwa kwa kitengo hicho kuwa ni kukamilisha utungwaji wa sheria ya usimamizi wa Milki nchini, utunzaji wa kanzi data ambayo inaenda kupatikana baada ya kukamilika kwa sensa ya watu na makazi na kushiriki na kuandaa mikutano ya wadau wa sekta ya Milki nchini.

Moja ya hatua ya utekelezaji wa Malengo haya inakuja kufuatia hatua ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuandaa mkutano wa wadau wa Sekta ya Milki Nchini utakaofanyika Septemba 1-2 mwaka huu katika ukumbi wa Kisenga Jengo la Millennium Towers Kijitonyama.

Kabyemela ameyataja malengo ya mkutano huo kuwa ni kujadili changamoto zilizopo katika Sekta hii ikiwemo changamoto ya upungufu wa Nyumba akibainisha kuwa kwa takwimu zilizopo Tanzania ina upungufu wa Nyumba Milioni tatu lakini pia kujadili matarajio ya Sekta hii kwa miaka ya usoni ambapo mahitaji ya Nyumba yatazidi kuongezeka pamoja na kuendelea kustawi kwa sekta ya Milki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news