Mashujaa wa Mahakama Kanda ya Shinyanga watunukiwa vyeti maalumu

NA EMMANUEL OGUDA

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma amewatunuku vyeti vya pongezi Mahakimu watano walioshiriki katika zoezi maalum la kumaliza mashauri ya mrundikano katika Mahakama za Hakimu Mkazi Simiyu na Mahakama za Wilaya Bariadi na Maswa.
Mkuu wa Mashata Mkoa wa Simiyu, Mhe. Chema Maswi akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.

Vyeti hivyo vya pongezi vimetolewa Agosti 26, 2022 katika halfa fupi ya kuwapongeza Mahakimu hao iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga. Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Matuma aliwapongeza Mahakimu hao kwa moyo wao wa kujitolea pasipo malalamiko ya aina yoyote na kufanikiwa kumaliza mashauri ya mrundikano 54 kwa muda wa majuma mawili.

“Kazi hiyo ni ya kizalendo na ya kujitolea sana,’’ alisema Jaji Mfawidhi huyo. Alisema Kikosi kazi cha tatu ambacho kiliundwa kwa ajili ya kumaliza mashauri kama hayo kwenye Mahakama za Mwanzo hakijaanza kazi kwa kuwa hadi sasa hakuna mashauri ya mrundikano katika Mahakama za Mwanzo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe. Christian Rugumira, akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.

Alibainisha pia kuwa Kikosi kazi cha Mahakama Kuu ambacho kinajumuisha Majaji watatu na Mahakimu wenye mamlaka ya ziada kimefanikiwa kuondoa mashauri ya mlundikano 46 kati ya 56 yaliyokuwepo, hivyo kubakiwa na mashauri 10 ambayo yanaendelea kuondolewa.

Aidha, Jaji Matuma amewataka wadau wa Mahakama, wakiwemo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka (DPP) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kushirikiana bega kwa bega na Mahakama ya Tanzania katika kumaliza mashauri kwa wakati. Akashauri changamoto ambazo zipo ziendelee kutatuliwa ili wananchi waweze kupata haki zao kwa wakati.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Mhe. Christiana Chovenye, akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.

Akitoa taarifa ya kikosi kazi hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Meatu, Mhe. Mohamed Siliti amesema wamefanikiwa kumaliza mashauri hayo 54 kwa ushirikiano mkubwa kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka Simiyu pamoja na wadau wengine licha ya changamoto ndogondogo zilizojitokeza.

Alisema kuwa wakati wa usikilizwaji wa mashauri hayo kikosi kazi pia kilitumia TEHAMA kwa kusikiliza jumla ya mashauri saba (7) kwa njia ya ‘video conferencing’ ambapo jumla ya vielelezo 77 viliwasilishwa kwa njia hiyo huku shahidi akiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam.
Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Isungang’holo, Kishapu Mhe. Sayi Mabondo akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.

Hakimu huyo alisema hatua hiyo iliweza kupunguza muda na kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipa shahidi huyo iwapo angesafiri hadi Maswa. “Kikosi kazi hiki kipo tayari muda wowote kitakapohitajika,” aliongeza Mhe. Siliti.

Awali akiongea katika Hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema alimpongeza Jaji Matuma kwa ubunifu alioufanya ili kumaliza mashauri ya mlundikano na akawapongeza watumishi wanaojituma na kujitolea bila kujali stahiki za kiutumishi wala malipo kwani kujitolea huko pia kumepunguza malalamiko katika ofisi yake.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Maswa Mhe. Enos Misana akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.

“Nakupongeza sana Jaji Mfawidhi wa Kanda yetu ya Shinyanga, jitihada zako za kumaliza mlundikano wa mashauri kumepunguza kabisa yale malalamiko ya mara kwa mara katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa,’’ alisema Mhe.Mjema. 

Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda ambaye ameshiriki pia katika zoezi hilo. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu aliwapongeza ubunifu uliofanywa Shinyanga na ameahidi kufanya hayo katika Mkoa wake wa Simiyu.

Katika salamu zake kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Sylvester A. Mwakitalu aliahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Mahakama na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili kuharakisha usikilizaji wa mashauri, hivyo kuchochea utoaji wa haki kwa haraka kwa wananchi. 

Alisema atafanya kazi kwa kasi na kuleta mashataka mahakamani huku upelelezi ukiwa umekamilika.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Shinyanga Mhe. Catherine Langau akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Ramadhani Kingai alipongeza jitihada kubwa zilizofanywa Kanda ya Shinyanga pamoja na mikakati iliyowekwa kumaliza mashauri ya mlundikano. Aliahidi kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati kwa kukamilisha upeleleze kwa muda.
Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga (katikati) akiwa na viongozi wengine katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo Shinyanga.

Tarehe 7 Februari, 2022, Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga iliunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kuondoa mashauri ya mlundikano katika Kanda hiyo na Mahakimu hao walijitolea kufanya kazi hiyo bila kujali stahiki zao za kiutumishi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news