Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la MICC,Dkt.Zakayo Nzogere atoa maoni yake kuhusu shuhuda za waliokuwa wachawi

ANAANDIKA Dkt.Zakayo Nzogere (PhD), Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la MICC, Mwanza. Huu ni mtazamo wake binafsi kuhusu shuhuda za namna hii;
1. SHUHUDA ZA WALIOKUWA WACHAWI:

Shuhuda nyingi nilizosikia za wapendwa ambao wanadai walikuwa "wachawi", wengi wao husema walikuwa "WENYEVITI" wa wachawi. Mara nyingine najiuliza hivi hao wachawi huwa wana 'WENYEVITI" wangapi? Pia najiuliza inakuwaje ULIMWENGU WA KIROHO (uchawi) uwe na wenyeviti?

Mimi naamini kwamba ni kweli Yesu Kristo anaweza kuokoa mtu wa aina yoyote bila kujali alikuwa amepotelea gizani kiasi gani; lakini shuhudu zingine huwa zina nia ya "KUONGEZA CHUMVI" ili kunogesha ushuhuda (kupiga "kamba" kwa utukufu wa Mungu 🤣🤣).

Wengine wanataka kuwaonyesha wasikilizaji kwamba jamaa alikuwa hatari sana na washukuru tu kwamba Yesu amemuokoa! Yani ni mkwara wa "kiroho".🤔

Unakuta mtu anajitangaza madhabahuni kwamba alikuwa akila nyama na damu za watu!! Hivi unajua hilo ni kosa linalohitaji uchunguzi wa vyombo vya usalama??

2. SHUHUDA ZA WALIOWAHI KUFA NA KWENDA MBINGUNI AU KUPATA MAONO/ NDOTO ZA JEHANAMU.

Mimi naamini kwamba kweli Mungu anao uwezo wa kufufua wafu lakini pia Mungu anaweza kumpa mtu maono/ndoto ya taswira ya mbinguni na jehanamu palivyo.

Ila napata shida kwa wenye shuhuda hizi ambao wengine wanasema walienda jehanamu wakakuta viwanda vya kutengeneza urembo wa wanawake, nguo za aina fulani, nk. Najiuliza, inakuwaje ULIMWENGU WA ROHO uwe na viwanda vya kutengeneza vitu huko Jehanamu?

3. SHUHUDA ZA WALIOKUWA WEZI:

Ni kweli Mungu anawaokoa watu waovu na majambazi. Hata hivyo, utakuta hata mtu ambaye alikuwa MWIZI WA KUKU NA MIWA naye anajinasibu kwamba alikuwa jambazi sugu wa silaha. Wengine hawajui kwamba kwa kuongeza huko chumvi unaweza hata chukuliwa hatua na vyombo vya usalama ili kusaidia kuelezea hiyo silaha unayodai ulikuwa unaitumia uliipeleka wapi?

MAMBO YA MUHIMU:

✅ Shuhuda zinazohusisha maono, ndoto, na kwenda kuzimu ama mbinguni ni lazima ZIPIMWE kwa kutumia NENO LA MUNGU, Biblia. 

Maelezo yoyote kuhusu "Ulimwengu wa Roho" (Mbinguni/Jehanamu) hayatakiwa kupishana na kile ambacho Biblia imekifunua kuhusu sehemu hizo.

❌ Viongozi wa kanisa/huduma; tusifanye haraka kuwapa watu madhabahu eti kwa sababu tu wanasema walikuwa wachawi, jambazi sugu, au alipelekwa kuzimu na kurudi. Ni vyema kuchambua hizo shuhuda na kuhakikisha hazipotoshi ukweli.

✅ Lengo la ushuhuda ni kumwinua Mungu aliyetenda makuu; siyo kumpa KIKI au kumpandisha aliyetendewa na Mungu. Hivyo ushuhuda wa kweli hauhitaji kufanyiwa EDITING ili uwavutie wasikilizaji.

❌ Lengo la ushuhuda siyo kuwajengea watu HOFU bali kuwajengea watu TUMAINI lililopo katika YESU KRISTO.

✅ NAKUBALI KWAMBA MUNGU ANAOKOA WATU WA KILA AINA; LAKINI NI MUHIMU KUCHAMBUA BAADHI YA SHUHUDA KULINGANA NA NENO LA MUNGU, UHALISIA, NA TAARIFA ZA VYOMBO VYA USALAMA.

NB: Dr.Ngozere ni msomi wa shahada ya uzamivu katika uongozi wa taasisi (PhD in Organizational Leadership) kutoka Chuo kikuu cha Biblia Singapore. Kwa sasa anasoma PhD nyingine ya theolojia chuo kikuu cha DTS huko Dalas  Marekani.

Post a Comment

0 Comments