Musoma Vijijini wamweleza Prof.Muhongo wapo tayari kuhesabiwa Agosti 23

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Kata ya Makojo Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara, wamemuahidi Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini ambaye ni mbunge wao kuwa, wamejitayarisha kwa asilimia 100 kuhesabiwa siku ya Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022 baada ya kupata elimu na hamasa thabiti ya umuhimu wa sensa kutoka kwa Mbunge wao Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo.
Kata ya Makojo inaundwa na vijiji vitatu Chimati, Chitare, na Makojo ambapo wananchi hao walitoa ahadi hiyo Agosti 13, 2022 wakati Mbunge Prof. Sospeter Muhongo alipokuwa ndani ya kata hiyo akifanya ushawishi, hamasa na kutoa elimu kwa wanavijiji wa kata hiyo ambapo aliwaambia wao pamoja na wageni wao washiriki kuhesabiwa siku hiyo ya Agosti 23, 2022.

Wakati wa majadiliano ya kila kaya na kila mwananchi kuhesabiwa Mbunge Mheshimiwa Muhongo aliwakumbusha wananchi wa kata hiyo kuwa vipaumbele vya kata yao ni pamoja na elimu, afya, kilimo, uvuvi, vinavyohitaji ushiriki na uchangiaji wa Serikali.
Mheshimiwa Muhongo katika kampeni hiyo ya utoaji wa elimu na hamasa aliambatana na viongozi wa kata hiyo akiwemo Peresi Mujava Afisa mtendaji Kata ya Makojo, na Maafisa Watendaji wa Vijiji hivyo.

Kufuatia elimu hiyo iliyotolewa na Mheshimiwa Prof.Muhongo wanavijiji wa Kata ya Makojo wanao uelewa mkubwa juu ya umuhimu wa kuhesabiwa na wanakubali kwamba takwimu sahihi zinahitajika sana kwa mipango mizuri sana ya miradi yao ya maendeleo. Hivyo kama zilivyo kata nyingine 20 za Jimbo la Musoma Vijijini watahesabiwa wote kwa asilimia 100.
Aidha, miradi ya kata ya Makojo ambayo imekwisha pokea fedha kutoka serikalini ni ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Makojo na shilingi milioni 500 zimekwishatolewa huku viongozi na wananchi wao wakiishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za Mradi huo muhimu sana kwao.

Mradi mwingine ni wa Maji wa bomba ya Ziwa Victoria ambao una thamani ya Shilingi Bilioni 1.072 ni wa kusambaza maji ya bomba kwenye vijiji vya Chitare na Makojo ambao ulianza kwenye mwaka wa fedha 2013/2014 umechelewa kukamilika na ulisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Ambapo RUWASA inajitahidi kurekebisha kasoro zilizopo.

Huku, wananchi wakiwa na imani kubwa na serikali sambambana na Mbunge wao Mheshimiwa Muhongo kwamba mradi huo utakamilika wananchi waanze kupata huduma ya maji Safi na salama kwani ni dhamira ya serikali kuhakikisha huduma ya maji inaimarika kwa kiwango stahiki.
Pia, fedha za UVICO -19 Makojo Sekondari ilipewa Shilingi Mil. 60 kujenga vyumba vitatu vya madarasa, Shule Shikizi ya Mwikoko ilipewa Shilingi Mil. 60 kujenga vyumba vipya vitatu vya madarasa na Ofisi moja ambapo shule hii tayari imeshapewa fedha za ujenzi wa vyumba vipya viwili vya madarasa na Ofisi moja kutoka mradi wa Serikali wa EQUIP.
Kuhusu fedha za Mfuko wa Jimbo Makojo Sekondari imepewa mabati 158 na saruji mifuko 52 kutoka kwenye fedha za Mfuko wa Jimbo zilizonunua (mei, 22) vifaa vya ujenzi kwa Sekondari kadhaa ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.

Kuhusu miradi ya TARURA ndani ya kata ya Makojo, TARURA imekamilisha na inaendelea kubooresha eneo la Makojo- Chitare- Kurugee na Chitare - Mwikoko- Rusoli. Ambapo barabara hizo ni muhumu sana kwa uimarikaji wa uchumi wa Wavuvi na Wakulima wa eneo hilo.
Baadhi ya miradi mipya iliyopangwa kutekelezwa ndani ya kata ya Makojo ni pamoja na Uvuvi wa Vizimba. Ambapo wavuvi wako tayari kuanzisha vyama vya ushirika vya uvuvi kwa lengo la kupata mikopo ya uvuvi wa vizimba, Huku ujenzi wa zahanati wa Kijiji cha Chimati ukiwa unaendelea.

Mradi wa tatu ni ujenzi wa Makojo-High school Wanavijiji wamemuomba Mbunge wa Jimbo lao Mheshimiwa Prof. Muhongo ashirikiane nao kwenye ujenzi wa High School hiyo. Ambapo Mbunge amekubali ombi hilo na kikao Cha mradi huo kitafanyika mwishoni mwa mwezi Septemba 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news