Raila Odinga asema hapana, Dkt.Ruto asema wataijenga Kenya

NA DIRAMAKINI

ALIYEKUWA mgombea urais wa Jamhuri ya Kenya kupitia wa Azimio la Umoja,Mheshimiwa Raila Odinga Amolo Raila amekataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022.

Ni matokeo yaliyotangazwa Agosti 15, 2022 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), Bw.Wafula Chebukati.

Bw.Chebukati alimtangaza mgombea urais kupitia Kenya Kwanza, Mheshimiwa Dkt. William Ruto kuwa mshindi kwa kupata kura milioni 7.1 sawa na asilimia 50.49 dhidi ya kura milioni 6.9 sawa na asilimia 48.85 alizopata Mheshimiwa Odinga.

Aidha, katika kinyang'anyiro hicho ambacho wawili hao walionekana kuwa na ushindani zaidi, wagombea wengine kwenye uchaguzi huo ni George Wajackoyah aliyepata kura 61,969 sawa na asilimia 0.44 na David Waihiga ambaye alipata kura 31,987.

Agosti 16, 2022 Mheshimiwa Odinga amezungumza na waandishi wa habari na kuweka wazi kuwa hatambui matokeo hayo na hamtambui Dkt.Ruto kuwa ni rais mteule kwa sababu amepatikana kutokana na matokeo batili.

Licha ya kutoutambua ushindi na matokeo hayo, Mheshimiwa Odinga amewataka wafuasi wake kuendelea kuwa wapole, kwani wataenda kutafuta haki mahakamani.

“Takwimu zilizotangazwa na Chebukati si halali na tutalishughulikia jambo hili katika mahakama ya sheria. Kitendo cha Chebukati kutangaza mshindi ni kinyume cha sheria na taratibu,”amesema.

Pia amebainisha kwamba, sheria inayounda IEBC inaelekeza kwamba uamuzi katika jambo lolote utapitishwa na makamishna walio wengi.

Aidha, Mheshimiwa Odinga amesema jambo la kushangaza ni kwamba mwenyekiti huyo wa IEBC alitangaza matokeo licha ya makamishna wanne kujitenga katika mchakato wa kutangaza matokeo hayo.

Ruto

Awali baada ya kutangazwa na tume kuwa Rais mteule wa Jamhuri ya Kenya, Dkt.William Ruto ambaye ni Naibu Rais ambaye alikosana na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa muhula wa pili aliipongeza tume kwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki.

"IEBC ambayo ni tume ya uchaguzi ilitushangaza sote…ninataka kupongeza IEBC kwa kuongeza uaminifu wa viwango vingine.

Pia amepongeza mchakato wa uchaguzi, licha ya kwamba hapo awali kundi la makamishina walisema hawakuweza kushiriki katika utoaji wa matokeo.

"Wananchi wa Kenya walipiga kura, makamishena hawafai kupiga kura. Makamishena hao wanne hawana tishio lolote kwa uhalali wa matokeo. Msimamizi wa uchaguzi ndiye atangaza matokeo, na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alifanya hivyo kwa mujibu wa sheria. Wafula Chebukati ambaye ni mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ndiye shujaa wetu.

"Watu wa Kenya wameonyesha kutuamini, sio kwa sera za makabila yetu, bali kwa kile tulichokuwa tunakizungumzia.
Nitaendesha serikali ya uwazi, na ya kidemokrasia.Ninataka kuwaahidi watu wote wa Kenya, kwa njia yoyote waliyopiga kura kwamba hii itakuwa serikali yao.

"Hatuna haja ya kuangalia nyuma. Hatuna haja ya kunyoosheana vidole. Hatuna tamaa wala haja ya kutupiana lawama. Ni lazima tushirikiane kwa ajili ya Kenya inayofanya kazi, ya kidemokrasia na yenye ustawi.

''Ninataka kuwaahidi watu wote wa Kenya, bila kujali jinsi walivyopiga kura kuwa hii itakuwa serikali yao. Najua wengi wanashangaa, haswa wale ambao wametenda mambo mengi dhidi yetu, nataka kuwaambia kwamba hawana chochote cha kuogopa," alisema Dkt.Ruto.

Alipiga simu

Dkt.Ruto alisema kuwa, "Nilimpigia simu Raila na tukafanya mazungumzo naye na tukakubaliana kuwa vyovyote itakavyokuwa, tutafanya mazungumzo.

"Hata hivyo, alipuuzilia mbali kupeana mkono na Raila au washindani wake akisema yeyote anayepinga matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anafaa kwenda mahakamani.

"Uchaguzi huu ulikuwa wa uwazi zaidi kuwahi kufanyika nchini Kenya. Labda watu waliokatishwa tamaa walikuwa watu walioamini serikali ya kina,"alisema.

Dkt.Ruto pia aliahidi atashirikiana upinzani kwa kiwango ambacho watatoa usimamizi kuhusu utawala wake. "Nataka kuwaambia wapinzani kwamba hawana chochote cha kuogopa, hakuna nafasi ya kulipiza kisasi. Ninafahamu kabisa kwamba nchi yetu ipo katika hatua ambayo tunahitaji juhudi za pamoja ili kusonga mbele,''alieleza.

Akizungumzia namna tume ilivyochukuwa muda kutoa matokeo ya uchaguzi wa urais na jinsi alivyosubiri kukamilika kwa mchakato huo alisema kuwa, "Mimi ni mwanademokrasia. Ninaamini katika utawala wa sheria. Ninaheshimu taasisi. Tutaheshimu uamuzi wa kila taasisi nyingine.

"Nina uhakika kutakuwa na mazungumzo. Mimi ndiye Rais mteule na kutakuwa na mpito na nina uhakika kutakuwa na majadiliano kati ya Rais wa sasa na mimi.Kama kungekuwa na mtu wa kuamua mkondo wa siasa za nchi ningejua, nadhani dhana hizo zimetokomezwa.

"Uchaguzi huu ulikuwa wa uwazi zaidi kuwahi kufanyika nchini Kenya. Labda watu waliokatishwa tamaa ni wale walioamini kuna watu watakaosaidia kuamua mkondo wa siasa za nchi,"alisema Dkt.Ruto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news