REA yatumia Trilioni 3/- kufikisha umeme vijijini, yavunja rekodi Kusini mwa Jangwa la Sahara

NA MWANDISHI MAALUM

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) hadi sasa umetumia takribani shilingi trilioni 3 kwa ajili ya kazi ya kupeleka miradi ya umeme vijijini.

Lengo ni kuhakikisha nishati ya umeme inafika na kutumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji, kuboresha huduma na shughuli za kiuchumi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (katikati) akifafanua jambo wakati wa kipindi maalumu kilichorushwa kupitia Kituo cha Runinga cha Azam na kuwashirikisha viongozi wa REA na wadau kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini, Agosti 11, 2022.

Hayo yamesemwa Agosti 11, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakati wa kikao kazi cha wakala huo na wadau wake kuelezea masuala mbalimbali ya nishati vijijini uliorushwa mubashara na Kituo cha Runinga cha Azam jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Saidy amesisitiza kuwa, mradi unaoendelea kwa sasa ni wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili) ambao pekee unagharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.2.

Ameongeza kuwa, kutokana na kazi zinazoendelea na mipango waliyoijiwekea, vijiji vyote nchini vitapata umeme kabla ya muda ulioelekezwa kwa maana ya mwaka 2025.
Viongozi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy (wa pili-kulia) wakishiriki katika kipindi maalumu na wadau, kilichorushwa kupitia Kituo cha Runinga cha Azam kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini, Agosti 11, 2022. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, Mhandisi Jones Olotu, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti, Mhandisi Elineema Mkumbo na Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia, Mhandisi Advera Mwijage.

"Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeahidi kufikisha umeme katika vijiji vyote ifikapo mwaka 2025, sisi kama REA hatutafika huko, tutakamilisha vijiji vyote kuvipatia umeme kabla ya mwaka huo.
Mtangazaji wa Kituo cha Runinga cha Azam, Goodluck Paul (kulia) akiongoza mjadala wakati wa kipindi kilichowashirikisha viongozi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wadau Agosti 11, 2022 jijini Dar es Salaam.

"Wananchi wakipata nishati ya umeme itasaidia sana katika uhifadhi wa mazingira, kwani hivi sasa zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa jambo ambalo linapelekea kuathiri mazingira kwa kuharibu misitu. Takwimu zinaeleza kuwa kwa mwaka mmoja, Tanzania inapoteza hekta 400 za misitu,"amesema Mhandisi Saidy.

Ameongeza kuwa, REA inatumia gharama kubwa kupeleka miradi ya umeme vijijini hivyo amewataka wananchi wa vijijini kuchangamkia fursa hiyo kwa kuutumia kwa shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa REA,Mhandisi Elineema Mkumbo, amesema hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imepanda kutoka asilimia mbili mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69.6 mwaka 2020.
Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo (katikati) akifafanua jambo wakati wa Kipindi Maalumu kilichorushwa kupitia Kituo cha Runinga cha Azam na kiushirikisha viongozi wa REA na wadau kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini, Agosti 11, 2022.

"Lengo letu ni kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote nchini vinapata umeme nyumba kwa nyumba,"amesema Mhandisi Mkumbo.

Mhandisi Mkumbo ameeleza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vijijini inaenda sambamba na kupeleka umeme katika vitongoji ambapo hadi sasa zaidi ya vitongoji 27,000 vimepatiwa umeme.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu ameeleza kwamba, kufuatia kasi ya upelekaji miradi ya umeme vijijini na nishati hiyo kuwafikia wananchi wengi wa vijijini, Tanzania imeweka rekodi na kuongoza katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo wananchi wake wamepunguza kuhama kutoka vijijini kwenda mijini na badala yake watu mijini kuhamia vijijini kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu (kushoto) akifafanua jambo wakati wa Kipindi Maalumu kilichorushwa kupitia Kituo cha Runinga cha Azam na kiushirikisha Viongozi wa REA na Wadau kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini, Agosti 11, 2022.

"Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kubadilisha mtazamo wa watu kuhama kutoka vijijini kuja mjini, siku hizi ni kawaida kabisa watu wanahama kutoka mjini na kuhamia vijijini,"amesema Mhandisi Olotu.

Mhandisi Olotu amebainisha kwamba, matokeo ya kasi ya upatikanaji umeme vijijini hivi sasa ni matokeo ya REA kuandaa mipango kabambe na mikubwa ukiwemo mpango mkubwa wa miaka mitano wa kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini ambao REA inaendelea kuutekeleza huku vipaumbele vikiwa ni taasisi za umma ikiwemo zahanati, shule, vituo vya maji, polisi, nyumba za ibada kwa lengo la kuboresha huduma za jamii.

Akichangia katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia wa REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema, kazi ya REA siyo tu kupeleka umeme vijijini bali ni kupeleka nishati mbalimbali vijijini ili ziweze kutumika na wananchi wa maeneo hayo katika shughuli mbalimbali ambapo katika kusambaza gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya majumbani wanashirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kazi hiyo wanaifanya katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.

Mhandisi Mwijage ameongeza kuwa, katika maeneo ya visiwa, REA imekuwa ikitumia nishati ya jua katika kupeleka miradi ya umeme ili kuhakikisha visiwa vyote nchini vinapata nishati hiyo ambapo kwa sasa mpango uliopo ni kuvipelekea umeme visiwa 36.
Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage (kulia) akifafanua jambo wakati wa Kipindi Maalumu kilichorushwa kupitia Kituo cha Runinga cha Azam na kiushirikisha viongozi wa REA na Wadau kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini, Agosti 11, 2022.

"Tanzania tuna visiwa 196, visiwa 53 havina makazi ya kudumu, vyenye makazi ya kudumu ni 143. Kati ya visiwa 143 vyenye makazi ya kudumu, visiwa 72 vina umeme na visiwa 71 havina umeme. Tulianza na visiwa 20 kuvipelekea umeme na sasa tuna mpango wa kupeleka umeme katika visiwa 36," amesisitiza Mhandisi Mwijage.

Akizungumzia suala la mawakala wa wauzaji mafuta vijijini ambao watakopeshwa ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi wa vijijini, Mhandisi Mwijage amesema, "Kitu kikubwa kitakachozingatiwa kwa wauzaji na vituo vya mafuta vijijini ni usalama, mazingira ya kuuzia mafuta, eneo na kituo husika.

"Watakaokidhi vigezo watawezeshwa kupitia mikopo na lengo letu ni kuhakikisha kwamba katika utekelezaji wa zoezi hili walengwa na wanufaika wote watoke vijijini,"amesema Mhandisi Mwijage.

Nao wahariri wa vyombo vya habari akiwemo Joyce Shebe, Salome Kitomari na Neville Meena wakizungumza katika mkutano huo wameishauri REA kuendelea kutilia mkazo suala la usawa wa kijinsia katika fursa na matumizi ya nishati, kuchangia na kukuza uchumi.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 umekuwa na desturi endelevu ya kukutana na wadau mara kwa mara katika vikao kazi kueleza na kutoa mrejesho wa masuala mbalimbali ya nishati vijijini, lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau na mwananchi mmoja juu kazi zinazoendelea kufanywa na wakala huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news