TEF:Sheria ni nzuri, lakini penye ukakasi ndipo tunataka marekebisho

NA MWANDISHI WETU

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limesema si sheria zote za habari zina ukakasi bali ni chache ambazo zinahitaji marekebisho yatakayoboresha zaidi tasnia hiyo.
Rashid Kejo ambaye ni Mjumbe wa TEF ameyasema hayo leo Agosti 5, 2022 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya jukwaa hilo alipowatembelea wahariri wa magazeti ya Serikali, Mgaya Kingoba wa Habarileo na Christopher Majaliwa wa Daily News kwa ajili ya kueleza kwa upana mchakato wa maboresho ya sheria ya huduma za habari nchini.

“Mchakato huu wa mabadiliko ya sheria, haulengi kung’oa sheria zote kwa kuwa, zipo nzuri na zenye maana kubwa katika tasnia ya habari, mfano kulazimisha maofisa wa Serikali kutoa taarifa kwa waandishi, kutambua maslahi na mikataba ya waandishi, haya ni mambo mazuri, yapo mengi.

“Lakini kuna maeneo ambayo yana athari kubwa kwa waandishi na vyombo vya habari, maeneo hayo ni mwandishi anaweza kufungwa hata asipoitwa mahakamani, usajili wa magazeti kila mwaka, uhuru wa hakimu kumfunga mwandishi apendavyo na mengine kama hayo, ndio tunapigania yaondolewe,"amesema.

Bw.Kejo ameeleza kuwa, Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, ina maeneo yanazuia kukua kwa tasnia hiyo akitoa mfano sheria inayozungumzia utwaaji wa vifaa vya vyumba vya Habari kwa uchunguzi, lakini pia mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Habari Maelezo ya kupeleka matangazo kule anakojisikia.

Amesema, taasisi zote zimeelekezwa kupeleka matangazo Habari Maelezo, ambao mkurugenzi wake ndiye atayeamua chombo cha habari cha kutangaza.

“Serikali ndiyo mtangazaji mkubwa, sasa chombo kitachoonekana kukosoa serikali bila shaka kitakosa matangazo, hapo ni kuua kazi ya uanahabari lakini pia kuua uchumi wa wanahabari.

“Lakini pia, tasnia ya habari inahitaji uwekezaji mkubwa, sheria yetu inambana mwekezaji wa nje ya nchi kuwekeza kwa asilimia 100, ametakiwa sizidi asilimia 49 tu, huku ni kufanya tasnia idumae. Tunatamani haya yote yabadilishwe,”Rashid Kejo ambaye ni Mjumbe wa TEF.

Post a Comment

0 Comments