TUNAWIKA TANZANIA: Madola wanasikia, Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeendelea kung'ara katika anga za Kimataifa kutokana na namna ambavyo washiriki wa michezo ya Jumuiya ya Madola wanavyoonesha vipaji vyao, huku wakitwaa medali na hata kuonesha umahiri wa hali ya juu katika mashindano hayo.
Sean Lazzerini wa Scotland (kushoto) na Yusuf Changalawe wa Tanzania wakichuana wakati wa mpambano wa nusu fainali wa ndondi ya uzito wa Light Heavy kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Birmingham, Uingereza, Jumamosi, Agosti 6, 2022. (Picha na AP).

Alianza mwanariadha, Alphonce Felix Simbu kwa kutwaa medali ya Fedha baada ya kuibuka mshindi wa pili mbio za riadha katika Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Birmingham, Uingereza, nyuma ya Victor Kiplagat wa Uganda na Agosti 6, 2022 bondia Mtanzania, Yusuf Changalawe ameondoka na medali ya Shaba baada ya kuchuana vikali na bondia wa Scotland, Sean Lazzerini katika pambano la uzito wa juu.

Ni pambano ambalo limepigwa katika Ukumbi wa NEC uliopo jijini Birmingham nchini Uingereza ambapo alishinda kwa pointi 4-1 katika pambano ambalo lilikuwa na ushindani mkali.

Changalawe alitinga hatua hiyo kwa kumtoa Arthur Langelie wa St.Lucia katika uzito wa juu wa Light kupitia pambano la robo fainali, mafanikio yaliyotokana na kumtwanga kwa pointi Curlin Richardson wa Aquila Isles.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kwa kuguswa na namna ambavyo Watanzania wanazidi kulipa Taifa heshima kutoka medali ya fedha hadi shaba, anakushirikisha jambo kupitia shairi lifuatalo;

1:Tunawika Tanzania, Madola wanasikia,
Simbu tulimsikia, medali kutupatia,
Changalawe kaingia, kitu ametufanyia,
Hii medali ya shaba, pia tunayo ya fedha.

2:Yusufu kapambania, hii yetu Tanzania,
Mwisho hakukufikia, medali katushushia,
Ni heshima Tanzania, medali zinaingia,
Hii medali ya shaba, pia tunayo ya fedha.

3:Ziko mbili Tanzania, medali mejishindia,
Ya fedha litangulia, Simbu alitushushia,
Nyingine twafurahia, Changalawe fagilia,
Hii medali ya shaba, pia tunayo ya fedha.

4:Kile tunatamania, zama zile Tanzania,
Ambapo tulivutia, riadha kujishindia,
Na ndondi kupigania, medali zikaingia,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

5:Michezo sisitizia, ni ajira nakwambia,
Serikali meingia, mengi inatufanyia,
Hao walojishindia, minoti tajipatia,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

6:Tuzidi jiandalia, vijana kutushindia,
Michezo tukisikia, tuwekeze Tanzania,
Kesho tutajivunia, tukiwika Tanzania,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

7:Yusufu twafagilia, Madola kujishindia,
Hapo ulipofikia, Mandonga angeushia,’
Hongera twakuambia, meibeba Tanzania,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

8:Chonde chonde Tanzania, wacheza zote sikia,
Mkicheza Tanzania, au nje Tanzania,
Kushinda twafurahia, kushindwa tunaumia,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

9:Anga nyingi Tanzania, kwa sasa tumeingia,
Iwe kombe la dunia, timu mbili meingia,
Na Kabadi Tanzania, nako tunainukia,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

10:Kote tunakofikia, bendera ya Tanzania,
Vema sana kupania, vizuri kuifanyia,
Nchi yatutangazia, na pesa zinaingia,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

11:Serikali Tanzania, hongera zetu sikia,
Waziri unasikia, medali zinaingia,
Pesa uloahidia, andaa kuwapatia,
Hii medali ya shaba, tunayo ya fedha pia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news