VISHIKWAMBI KUIBIWA: ZICHUKULIWE HATUA

NA LWAGA MAMBANDE (KiMPAB)

SENSA ya Watu na Makazi ambayo inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi katika maeneo yote nchini tangu Agosti 23, 2022 imekuwa ya tofauti na kisasa zaidi kutokana na mfumo wa ukusanyaji wa taarifa ambao unatumia Vishikwambi (tablets) katika hatua zote za utekelezaji wa sensa kwa lengo la kupunguza gharama.
Hii ndiyo Sensa ya kwanza nchini kufanyika kwa kutumia vishikwambi, ni mfumo ambao ni rahisi na haraka katika kukusanya na kutuma taarifa ngazi husika bila kikwazo chochote.

Licha ya juhudi za Serikali kubuni na kuja na wazo la kutumia vishikwambi hivyo, baadhi ya watu wenye nia ovu wamekuwa wakiwapora makarani wa sensa vifaa hivyo,mfano katika moja ya tukio huko jijini Arusha na kule Katavi ambapo makarani waliporwa vishikwambi.

Mshairi wa kisasa,Bw.Lwaga Mwambande anarejea kusema kuwa,wenye tabia za namna hii inafaa jamii iwaweke wazi ili mamlaka zinazohusika likiwemo Jeshi la Polisi liweze kuchukua hatua haraka kwa lengo la kudhibiti tabia za namna hiyo ambazo hazina dhamira njema kwa zoezi hilo la Kitaifa,kupitia shairi hapa chini unaweza kujifunza kitu;

1.Hizi habari si nzuri, vishikwambi kuibiwa,
Habari hizi za shari, si vizuri kusikiwa,
Kwani zaleta dosari, kwa watu kuhesabiwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

2.Endapo kuna uzembe, sababu ya kuibiwa,
Wakabiliwe wazembe, tuache kusumbuliwa,
Kama wezi tuwachambe, tupate kuwaelewa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

3.Sensa jambo la muhimu, vile tulielezewa,
Tena ni jambo adhimu, lapaswa kufanikiwa,
Wezi hawa kwetu sumu, siyo wa kuvumiliwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

4.Sensa inaendelea, watu tunahesabiwa,
Makarani endelea, yale ya kuzingatiwa,
Vifaa livyopokea, viepushe kuibiwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

5.Vishikwambi mali yetu, japo mmekabidhiwa,
Nyie kwa niaba yetu, mnavyo vya kutumiwa,
Tambueni lengo letu, ni sensa kufanikiwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

6.Hili zoezi la sensa, kwa sisi kuhesabiwa,
Limepamba moto hasa, kwa hatua twapitiwa,
Muhimu kutolikosa, takwimu zinatakiwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

7.Sasa nyie mkiiba, na sensa tukachelewa,
Takwimu mnazikaba, gharama twaongezewa,
Mjue tutawabeba, mwisho mtahukumiwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

8.Halafu msichojua, kitu mmetegeshewa,
Serikali inajua, vifaa vikitumiwa,
Kokote mtakotua, mtakuja chukuliwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

9.Tahadhari hii pia, vifaa kununuliwa,
Mtu akikupitia, kishikwambi kuuziwa,
Fedha ukimpatia, unaweza shikiliwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

10.Heko tunawapatia, wote walohesabiwa,
Kongole hizi sikia, jinsi nyie waelewa,
Ni kujenga Tanzania, malengo yakifikiwa,
Zichukuliwe hatua, kukomesha jambo hili.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news