Waguswa na utayari wa Serikali iliyopo madarakani kuelekea maboresho sheria za vyombo vya habari

NA MWANDISHI WETU

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kuguswa na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inavyoonesha dhamira njema ya kufanya maboresho katika sheria za vyombo vya habari ambazo zinaonekana zinabinya uhuru wa habari nchini.

Hayo yanabainishwa ikiwa tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameelekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru vya vyombo vya habari zirekebishwe.

Rais Samia aliyasema hayo Mei 3 ,2022 wakati akiwahutubia wadau wa vyombo vya habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti’ katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote. Tunatumia busara,lakini sheria zipo pale pale. Busara ninayotumia, twende tufanye kazi kwa kushirikiana.Waandishi wa habari mna mchango mkubwa katika maendeleo, kwa nini mimi nifanye kazi bila waandishi wa habari. Hivyo hatuhitaji kugombana, tukae tuzungumze tujenge nchi yetu,"Rais Samia alieleza siku hiyo.
Katika mahojiano na Radio Tumaini (Tumaini FM) ya jijini Dar es Salaam leo Agosti 5, 2022 wakili wa kujitegemea James Marenga akiwakilisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, ni jambo la heri kwa Serikali iliyopo madarakani kuonesha utayari wa kupitia upya sheria za habari nchini.

Pia amesema, mabadiliko ya sheria huwa yanachukua muda mrefu, wakati wa sasa ni mzuri kwa kuwa, rais aliyepo madarakani ameonesha dhamira hiyo.

“Mchakato wa marekebisho ya sheria iliyotungwa mwaka 2016, ulichukua miaka 10. Mchakato huo ulianza mwaka 2006, ni bahati utawala uliopo umeona kuna haja ya kupitia upya sheria hizi kama ambavyo wadau wamekuwa wakipiga kelele,” alisema Marenga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania (MISA TAN).

“Tunaamini sheria hizi na zingine ambazo tumeorodhesha kwenye nakala yetu ya mapendekezo ya mabadiliko, wadau na serikali kwa pamoja tutapitia na kuona namna ya kunyoosha ili mapendekezo hayo yatapopelekwa bungeni, tuwe na msimamo unaofanana,” amesema.

Post a Comment

0 Comments