Wamiminika banda la BoT maonesho ya Nanenane Zanzibar kujifunza

NA DIRAMAKINI

WANANCHI mbalimbali kutoka ndani na nje ya Jiji la Zanzibar wameendelea kumiminika katika banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo benki hiyo na huduma wanazotoa.
BoT inashiriki katika Maonesho ya Nanenane Zanzibar yanayofanyika katika Viwanja vya Kizimbani Mkoa wa Mjini Magharibi kuanzia Agosti 6 hadi Agosti 14,2022.
Wataalam mbalimbali kutoka BoT wapo katika banda hilo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi wote kuhusu kazi na majukumu ya msingi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ni benki inayohudumia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.
Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.
Majukumu mengine ya Benki Kuu ya Tanzania ni;

>Kutoa sarafu ya nchi ambayo ni Shilingi ya Tanzania
>Kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha
>Kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini.
>Kuhifadhi akiba ya nchi ikiwemo fedha za kigeni
>Benki ya Serikali
>Benki ya Mabenki; na
>Kutoa ushauri juu ya masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Agosti 8, 2022 wakati akiyafungua maonesho hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewahimiza wakulima na wafugaji wanaoshiriki katika maonesho hayo kuitumia vyema fursa hiyo kutafuta elimu ya matumizi sahihi ya zana za kisasa, mbegu bora na pembejeo ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo na Ufugaji nchini.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, wakulima na wafugaji wanapaswa kuyatumia maonesho hayo katika kutafuta elimu inayohusu matumizi ya zana za kisasa, upatikanaji wa mbegu bora, elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na njia za kupambana na maradhi yanayoathiri sekta hizo.

Amesema, kuwepo kwa maonesho hayo kunatoa fursa kwa wananchi kuona mbinu za kisasa za kilimo, ufugaji, uvuvi pamoja na shughuli mbalimbali za kibiashara na ujasiriamali.

Pia amesema, maonesho hayo yanatoa fursa ya kuwakutanisha ana kwa ana wadau mbalimbali, wakiwemo wazalishaji na wateja wao, hatua inayotoa mchango mkubwa katika kukuza na kuongeza ubunifu, kutambua mafanikio, changamoto pamoja na upatikanaji wa masoko.

Akigusia kauli mbiu ya maonesho hayo isemayo ‘Kilimo ni Biashara, Shiriki kuhesabiwa kwa Mipango bora ya Sekta ya Kilimo’,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, kaulimbiu hiyo imekuja kwa wakati mwafaka kwa kuzingatia changamoto kadhaa zinazoikabili Dunia na kutishia kuathiri hali ya Usalama wa Chakula.

Amesema, sekta zote za uzalishaji na usafirishaji zimeathirika kutokana na janga la UVIKO-19 pamoja na mgogoro ulioibuka baina ya mataifa ya Urusi na Ukrane ambayo ni mataifa yenye mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula,hususani ngano pamoja na uzalishaji wa mbolea na pembejeo.

Post a Comment

0 Comments