YALE MASWALI YA SENSA: Karani nipo tayari,Nitoe habari zote, ndiyo niende kutesa

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

KWA mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Sensa ya Watu na Makazi itafanyika usiku wa Agosti 22, 2022 kuamkia Agosti 23, 2022 ambapo Siku ya Sensa tarehe 23 itabaki kuwa tarehe rejea ya Siku ya Sensa.

Aidha, zoezi la kuhesabu watu litaendelea kwa takribani siku sita ambapo kwa mujibu wa NBS, Sensa haiwezi kukamilika kwa siku moja kwa nchi nzima.

Sensa hii ina umuhimu mkubwa katika maisha yetu sisi wananchi na Taifa kwa ujumla, kwani Serikali inategemea taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

Pia taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.

Sambamba na kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano pato la mtu mmoja mmoja,pato la Taifa, ajira na ukosefu wa ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi.

Kwa umuhimu na upekee wa zoezi hili la sensa ambalo linagusa maisha ya kila Mtanzania, mshairi wa kisasa,Bw. Lwaga Mwambande anasema,yupo tayari kuhesabiwa na kuyajibu maswali yote kadri atakavyoulizwa na karani wa sensa, hatua kwa hatua jifunze jambo hapa;


1:Nataka nijibu yote, yale maswali ya sensa,
Yatume nipitepite, ili ni wa kisasa,
Waulize wayapate, majibu yote ya sensa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

2:Majibu nijue yote, kwa kujipiga msasa,
Makarani waje wote, kwangu wasikute visa,
Watakacho wakipate, kuwachelewesha kosa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

3:Karatasi nilipate, tena niandike hasa,
Mtihani usipite, na mikasi ya makossa,
Huo ni wajibu wote, mwananchi wa kisasa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

4:Yahusuyo watu wote, wa zamani na wa sasa,
Walio nyumbani wote, siwezi fanya makosa,
Hao niwajue wote, umri jinsi kunasa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

5: Kwa uhusiano wote, demografia ya sasa
Masuala ndoa zote, uraia pia fursa,
Ya ulemavu wowote, kujua muhimu hasa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

6:Mambo ya elimu yote, wazee vijana sasa,
Ile mimi niipate, ya shuleni si kanisa,
Taarifa hizo zote, hata kujaza kurasa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

7:Ule uhamaji wote, wa hapa hata Mombasa,
Kwa Watanzania wote, watazitafutao fursa,
Taarifa hizo zote, ziwe kwenye ukurasa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

8:Miliki nyaraka zote, zile za taifa hasa,
Za vitambulisho vyote, nijue bila kudesa,
NIDA udereva vyote, taarifa sijekosa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

9:Vifo na vizazi vyote, na uchumi wa kisasa,
Miliki ardhi yote, mali za kuleta pesa,
Kilimo mifugo yote, takwimu muhimu hasa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

10:Jumanne ile yote, siwezi fanya makossa,
Nashinda nyumbani yote, hadi wafike wa sensa,
Nitoe habari zote, ndiyo niende kutesa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

11:Nataka maswali yote, nisiwachoshe wa sensa,
Watake habari zote, wazipate bila kosa,
Wajenge takwimu zote, zitengeneze fursa,
Sensa watu na makazi, tayari kuhesabiwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news