Yanga SC, Singida Big Stars wang'ara huku Polisi Tanzania, Prisons wakikosa

NA DIRAMAKINI

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kuwa,mechi zijazo katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara watahakikisha wanajikusanyia ushindi wa kutosha ili kujiweka vizuri katika harakati za kutetea ubingwa wao tena.

Aliyasema hayo Agosti 16, 2022 baada ya Yanga SC kuichapa Polisi Tanzania mabao 2-1 kwenye mtanange uliopigwa dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

“Ilikuwa ni mechi ngumu, lakini tumeweza kupata ushindi hilo ni jambo la muhimu kwetu hivyo tunaendelea kusaka ushindi kwa mechi zijazo,”alisema Nabi.

Unaweza kusema kwa matokeo hayo, Yanga SC imeanza vema katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara licha ya ushindi mwepesi wa jana.

Kupitia mtanange huo ambao ulikuwa ni wa kasi mwanzo hadi mwisho, Polisi Tanzania walitangulia kwa bao la Salum Ally Kipemba dakika ya 34.

Aidha, bao hilo lilikuja baada ya mshambuliaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Fiston Kalala Mayele kukosa penalti dakika ya 11 tu ya mchezo huo.

Hata hivyo,Mayele alikwenda kufuta makosa yake kwa kuifungia Yanga SC bao la kusawazisha dakika ya 41, kabla ya Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto naye kufuta makosa yake yaliyosababisha bao la Polisi kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 84.

Polisi ilimaliza pungufu baada ya nyota wake, Ally Othman Mmanga kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 88 kufuatia kuoneshwa kadi ya pili ya njano kwa kucheza rafu.

Wakati huo huo,Singida Big Stars wameanza vema Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Ni kupitia mtanange uliopigwa Agosti 16, 2022 katika dimba la Liti ambao kwa zamani lilikuwa linajulikana kwa jna la Namfua mkoani Singida.

Mshambuliaji Mbrazil, Peterson Cruz dakika ya 36 ndiye aliyetikisa nyavu za Tanzania Prisons, bao ambalo lilidumu hadi dakika tisini, hivyo kuwawezesha Singida Big Stars kuchukua alama zote tatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news