Mabalozi fungueni njia zaidi kwa kutangaza vivutio vya nchi yetu-Mhe.Othman

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema msingi mkuu wa diplomasia ya sasa nchini na kote duniani ni kutanua fursa za kuleta maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, akizungumza na Ujumbe wa Mabalozi wateule wa Tanzania katika Mataifa mbali mbali, waliofika Ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar, kwa lengo la kujitambulisha, kubadilishana mawazo, na kuagana wakielekea katika Vituo vyao vipya vya kazi.

Amesema kuwa diplomasia hiyo inajengwa kwa kuzingatia misingi ya mambo muhimu yanayopatikana katika Mataifa ya Kigeni, sambamba na fursa nyingi ziliopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbele ya nchi nyingine, pia kwa manufaa ya pande zote.
“Msisitizo mkubwa kwa sasa ni kuzingatia ni yepi tunaweza kufaidika nayo kutoka kwa wenzetu, na kwa upande mwingine tunaangalia pia ni yepi kutoka kwetu wenzetu wanaweza kunufainika nayo”, amesema Mheshimiwa Othman.

Aidha, Mheshimiwa Othman amebainisha wajibu wa Wanadiplomasia hao kutangaza, katika Mataifa wanayokwenda, vivutio mbali mbali viliopo Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla, hali ambayo itasaidia kufungua njia zaidi kwa wawekezaji na washirika wa maendeleo kuja kuwekeza hapa Nchini na hivyo kuongeza fursa za moja kwa moja za kufanikisha juhudi za kuhamasisha maendeleo.
Pamoja na kuwapongeza na kuwatakia kila la kheri Wanadiplomasia hao kutokana na hatua ya Uteuzi wao wa hivi karibuni kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Othman amewataka watumie nafasi yao ya kuwa Mabalozi wema wenye ubunifu, na hasa ikizingatiwa kwamba Nchi hii inazo fursa nyingi ambazo watu wake bado wanashindwa kuziibua.

Naye Kiongozi wa Ujumbe huo, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Bw. Simon Sirro, amesema kuwa yeye na wenzake wapo tayari kwa kazi ya kwenda kuiwakilisha Nchi pamoja na kutangaza fursa nyingi ziliopo, ili kusaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi.
Mkuu huyo Mstaafu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) amemuahidi Mheshimiwa Othman kuwa, pamoja na heshima kubwa waliyoipata yeye na wenzake, ya kuaminiwa na Mkuu wa Nchi ili kuiwakilisha Tanzania katika Mataifa ya Kigeni, hawatosita kila inapobidi kuja kupata miongozo na mashauri yatakayowezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa maslahi ya Taifa zima.
Katika Ujumbe wake, Balozi Sirro aliambatana pia na Balozi Mteule wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule; Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Bi Catherine Chipeta; na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki-Zanzibar, Bi Mariam Haji Mrisho.

Post a Comment

0 Comments