Mapato ya ATCL yapaa kwa kasi

NA DIRAMAKINI

KAMATI ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imesema mapato ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) yameongezeka kutoka shilingi bilioni 58 mwaka 2018/2019 hadi shilingi bilioni 239 mwaka 2021/2022.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa ameyabainisha hayo Septemba 5,2022 jijini Dodoma baada ya kuchambua taarifa ya ATCL na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).

Amesema,shirika hilo limekuwa likipata ongezeko la mapato kuanzia 2017/18 walipata shilingi bilioni 53, 2018/19 shilingi bilioni 111, 2019/20 shilingi bilioni 157, mwaka 2020/21 shilingi bilioni 174.5 na mwaka 2021/22 ilipata shilingi bilioni 239 bilioni.

Mheshimiwa Silaa amesema, hasara ya shirika hilo imepungua kutoka shilingi bilioni 48 kwa mwaka fedha 2018/2019 hadi shilingi bilioni 27 kwa mwaka 2021/2022.

“Ukiangalia wanafanya vizuri na hasara imekuwa ikipungua walianza mwaka 2018/19 hasara ilikuwa shilingi bilioni 48, mwaka 2020/21 shilingi bilioni 36, mwaka 2021/22 ilikuwa shilingi bilioni 27,"alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Wakati huo huo,amesema kila kiti cha ndege kinavyoingiza faida ambapo imeongezeka kutoka shilingi 251,000 kwa mwaka 2019/20 hadi shilingi 283,000 kwa mwaka 2020/21.

Alisema, hesabu walizofunga mwaka 2020/21 walifunga na faida ya shilingi bilioni 45 ikilinganishwa na shilingi bilioni 18 za mwaka 2019/2020.

Post a Comment

0 Comments