NHC kutumia Bilioni 466/- Samia Housing Scheme (SHS), ujenzi kuanzia Kawe Tanganyika Packers

NA DIRAMAKINI

AFISA Mauzo na Masoko Mwandamizi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Bw.Daniel Kure amesema kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa linatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba nyingi kama sehemu ya mpango mkakati wake ukiwemo mradi wa Samia Housing Scheme (SHC).
Kupitia mradi huo jumla ya nyumba 5,000 zitajengwa na utazalisha si chini ya ajira 26,000 kwa wananchi wa Tanzania na utagharimu shilingi Bilioni 466.

Kure amesema kuwa, kwa awamu ya kwanza mradi huo utaanzia jijini Dar es Salaam katika eneo la Kawe Tanganyika Packers na baadaye utasambaa katika nchi nzima na ujenzi wake utaanza mwezi Oktoba, mwaka huu na utafanyika kwa kipindi cha miezi 12.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 29, mwaka huu katika Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mjini Geita.

‘’Kwa mara ya pili sasa, yaani mwaka wa pili mfululizo tunashiriki katika maonesho haya ya madini mwaka huu wa fedha, mara ya kwanza tuliposhiriki tulipata faida nyingi sana, kwanza kukutana na wananchi mbalimbali ambao hawakuwa na taarifa juu ya miradi tunayotekeleza.

‘’Lakini pia, tulikutana na wateja wetu ambao tulitatua changamoto zao wanazopata katika nyumba tulizowapangisha. Na tukaona tena tuje kusudi tukutane na wadau wengi zaidi kwa sababu mwaka huu maonesho haya wamekuja watu wengi zaidi.
‘’Shirika la Nyumba la Taifa linatekeleza miradi mingi kama sehemu ya mpango mkakati wake, katika maonesho haya tunatazama kwa umakini sana mradi mpya unaotekelezwa kwa awamu nchi nzima tunatarajia kujenga nyumba 5,000. Kupitia mradi huu unaoitwa Samia Housing Scheme. Mradi huu unaanzia Dar es Salaam baadaye utahamia Dodoma na maeneo mengine.

‘’Tutautekeleza kwa awamu nchi nzima, tunatarajia kujenga nyumba 5,000. Na mradi huu unatarajia kuzalisha ajira si chini ya 26,000. Kwa wananchi wa Tanzania kwa hiyo kwa awamu ya kwanza tunaanzia Dar es Salaam mwaka huu na baadaye tutahamia Dodoma, tumekuja katika maonesho haya ili wananchi wawe na taarifa, makampuni, taasisi tuweze kuwapa taarifa ili wale wanaotaka nyumba waweze kupata nyumba kwa wakati.

‘’Mradi huu utakapokamilika katika awamu zote utagharimu shilingi bilioni 466 kama nilivyoanza kusema mwanzoni utekelezaji wake utaanzia katika eneo la Kawe Tanganyika Packers na baada ya hapo utasambaa nchi nzima, tunatarajia katika muda wa utekelezaji wake tutakuwa tumejenga nyumba 5,000.
Afisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bi. Domina Rwemanyila akizungumza na mmoja wa raia wa kigeni waliotembelea katika banda la shirika hlo kwenye maonesho hayo mjini Geita.

‘’Niwakaribishe wananchi wote wanaotufuatilia kupitia vyombo vya habari wanaokuja katika maonesho haya hapa Geita kukutana na sisi uso kwa uso, lakini pia katika ofisi zetu taarifa hizi zinapatikana na niwakaribishe kwa wote wanaohitaji nyumba wasichelewe kwa sababu mradi huu tunautekeleza kuanzia mwezi Oktoba na tunatarajia ndani ya miezi 12 tutakuwa tumemaliza utekelezaji wake.

‘’Hata sasa kuna fomu maalum ambazo atakayekuja kwenye banda letu au yeyote atakaye tupigia simu tutamtumia atajaza na atarejesha kwetu na tutakapozindua rasmi mradi tutamkaribisha kwa ajili ya kufanya malipo ya awali.
Afisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bi. Domina Rwemanyila akimfafanulia jambo, Bw. Andrew Mwinuka mnufaika wa mradi wa nyumba za NHC Bombambili mjini Geita aliyetembelea katika banda la shirika hilo kwenye maonesho ya madini mjini Geita.

‘’Shirika la Nyumba la Taifa katika kutekeleza hii miradi huwa linaingia katika mchakato kwanza wa kununua ardhi, kuweka miundombinu kama barabara, umeme, maji hivi vitu vyote vinagharimu shirika na hizi gharama wakati fulani huwa zinaongeza kidogo gharama ya nyumba kwa sababu tunahitaji mradi wetu unapotekelezwa mtanzania anaponunua akute nyumba iko kamili kabisa.

"Wakati fulani hizi gharama za kuweka miundombinu kama maji na umeme huwa zinapandisha gharama kidogo, lakini kwa sehemu kubwa shirika limejitahidi kuhakikisha kwamba bei zetu za nyumba zinaendana na kipato cha watanzania,"amesema Bw.Kure.

Wakati huo huo, Afisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bi. Domina Rwemanyila amesema, Mradi wa Samia Housing Scheme unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambapo shirika hilo linatamani Watanzania kukumbuka kwa miaka mingi ijayo.
Aidha, amewaomba wananchi wanaofika katika maonesho hayo ambayo mbayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "Madini na Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu" ambapo yanatarajiwa kufikia tamati Oktoba 8, mwaka huu kufika katika banda la NHC ili kujifunza mengi kuhusu miradi na uuzaji wa nyumba za shirika.

Post a Comment

0 Comments