Rais Dkt.Mwinyi:Serikali itaimarisha maslahi ya watendaji Ofisi ya CAG

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeanza mchakato wa kuimarisha maslahi ya watendaji katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ili kulinda nguvu kazi iliyopo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Charles E. Kichere kulia kwa Rais baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo na kushoto kwa Rais) niMdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt.Othman Abass Ali.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania, Charles E. Kichere, ambapo pamoja na mambo mengine amefika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema, Serikali inatambua umuhimu wa kazi inayofanywa na watumishi hao (wakaguzi) na kusema tayari mchakato wa kuimarisha maslahi yao umeanza kuambatana na mfumo uliopo wa makundi, akitolea mfano wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA) inayopaswa kuwa katika kundi la taasisi zinazozalisha kama vile Bandari.

Amesema, kuna umuhimu wa kuondoa tatizo la kimaslahi kwa watendaji wa taasisi hiyo kwa kuzingatia kuwa wengi wa watu wanaokaguliwa wana maslahi makubwa, hivyo kuwepo uwezekano wa kuondoka na kwenda kutafuta maslahi makubwa maeneo mengine.
Akigusia ukaguzi wa vyombo vya Muungano vilivyopo Zanzibar, Dkt.Mwinyi alisema anafarijika kuwepo kwa ushirkiano wa taasisi mbili za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Tanznaia na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar huku akibainisha kuwepo changamoto kubwa katika vyombo hivyo kuwa havikaguliwi au havikaguliwi vizuri.

Mheshimiwa Rais amesema, kuna matatizo makubwa katika Idara ya Uhamiaji Zanzibar, “kuna wakati ilitumwa kamati kwenda kufanya ukaguzi na kugundua kiasi cha shilingi Bilioni nane zilikuwa zimepotea ndani ya miezi sita, bado kuna kazi ya kufanya”.

Alisema, kuna uwezekano wa vyombo hivyo vya Muungano vinavyofanya kazi hapa Zanzibar kujificha nyuma na kutokuwemo katika ukaguzi, jambo alilosema linapaswa kurekebishwa, akibainisha hatua ya taasisi hizo kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia juhudi hizo.

Aidha, alipongeza ukaguzi wa hivi karibuni kuwa umeondokana na ukaguzi wa vitabu na badala yake kwenda kwenye miradi ili kuona uhalisia."Kuna watendaji hodari wa kuandika vitabu katika baadhi ya taasisi,"alisema.

Alisema, Zanzibar inaelekea kwenye sekta ya Mafuta na Gesi Asilia, hivyo kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka Tanzania Bara ambayo tayari imepiga hatua katika sekta hiyo, sambamba na kuwepo umuhimu wa kuwajengea uwezo watendaji (wakaguzi).

Aidha, alisema anafarijika na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya taasisi hizo, jambo ambalo amekuwa akilitilia mkazo kwa kuzitaka taasisi za Zanzibar kuchota uzoefu kutoka taasisi zinazofanana Tanzania Bara.

Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (CAG), Charles E. Kichere alimpongeza Dkt.Mwinyi kwa kazi kubwa na maono yake katika kuiletea Zanzibar maendeleo pamoja na kusimamia rasilimali za nchi.

Alisema, jukumu la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni kumsaidia Rais kwa kufuata dira kupitia nyanja mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo.

Alieleza kuwa taasisi CAG Tanzania pamoja na ile ya CAG Zanzibar zimekuwa na ushirikianao mzuri, ambapo baadhi ya nyakati huunganisha nguvu katika utekelezaji wa majukumu hususani katika miradi mikubwa pamoja kujengeana uwezo.
Alisema, taasisi hizo kama zilivyo sawa katika utekelezaji wa majukumu yake, zinakabiliwa na changamoto zinazolingana, ikiwemo ile ya maslahi, hivyo akaziomba Serikali zote mbili kuangalia uwezekano wa kuondokana na changamoto hiyo.

Mapema, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, Dkt.Othman Abass alisema kumekuwepo ushirikiano mkubwa kati ya taasisi hizo mbili, akitolea mfano wa hatua za hivi karibuni, ambapo Ofisi ya CAG Tanzania ilisaidia CAG Zanzibar kufanikisha ukaguzi katika taasisi za Muungano, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi za Mabalozi pale ilipokuwa ikiendesha zoezi la ukaguzi kwa kuwawezesha watendaji wake kufika hadi Mikoa ya Tanzania Bara, sambamba na kusomesha watendaji kutoka Ofisi ya CAG Zanzibar, gharama zikitolewa na Ofisi ya CAG Tanzania.

Alisema, katika kipindi kifupi kijacho, taasisi hizo zinatarajiwa kukamilisha mchakato wa utiaji saini hati za mashirikiano (MoU).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news