RC Kunenge atangaza tarehe Wiki ya Maonesho ya Biashara na Uwekezaji

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge ametangaza Oktoba 5 hadi Oktoba 10, mwaka huu itakuwa ni Wiki ya Maonesho ya Biashara na Uwekezaji yatakayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo Mailimoja Mjini Kibaha.

Kunenge ameitangaza wiki hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali uliofanyika leo katika ofisi yake iliyopo Mjini Kibaha.

Amesema,maandalizi ya maonesho hayo yanakwenda vizuri na lengo ni kuhakikisha mwaka huu maonesho yanakuwa bora ili kuwavutia zaidi wawekezaji.

Kunenge amesema kuwa, maonesho hayo yanafanyika kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) kwa usimamizi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TAN TRADE).

Aidha,amesema maonesho hayo yatafanyika kwa kujumuisha mikoa ya Kanda ya Mashariki ukiwemo Mkoa wa Pwani,Lindi,Mtwara,Dar es Salaam na Morogoro.

Amesema kuwa,mpaka sasa washiriki 520 wanategemewa kuwepo katika maonesho hayo huku kukiwa na matarajio ya watu watakaotembelea maonesho hayo ni 15,000.

Kunenge ameongeza kuwa, lengo la maonesho hayo ni kutangaza bidhaa mbalimbali zinazozalishwa katika viwanda na kutoa fursa kwa wawekezaji kujua namna wanakoweza kupata malighafi,kuonesha fursa za uwekezaji hususani katika uvuvi,utalii,kilimo,uwindaji wa kibiashara na fursa za madini.

"Wiki ya biashara na uwekezaji itatoa taswira ya namna ambavyo Rais ameweza kutengeneza mazingira ya uwekezaji hapa nchini na itatafsiri kwa vitendo sera za mazingira ya uwekezaji kwa mkoa wetu wa Pwani.

"Oktoba 5 mpaka Oktoba 10, mwaka huu itakuwa Wiki ya Maonesho ya Biashara na Uwekezaji hapa mkoani kwetu,kwa hiyo niwaombe wananchi kujitokeza kwa wingi kuja kutembelea katika mabanda ili waweze kujua bidhaa zinazozalishwa ndani ya mkoa na hata zile za mikoa mingine,"amesema.

Kunenge ametumia nafasi hiyo pia kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa wawekezaji.

Amesema kuwa,kwa sasa tayari mkoa umeweka mpango maalum (Masterplan) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuendeleza biashara ikiwemo Vigwaza-Kwala,Bagamoyo,Chalinze na Mafia.

Kunenge amewaomba wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza Pwani waje katika maonesho hayo kwa kuwa ndio sehemu muhimu ya kujua maeneo mazuri ya uwekezaji huku washiriki wajitokeze zaidi kwa kuwa bado wanahitajika.

Hata hivyo,amesema Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1,460 ambapo kati ya hivyo vikubwa 90 huku akitoa wito kwa wawekezaji kuendelea kuwekeza Pwani kwa kuwa mazingira ni mazuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news