Ripoti: 2021, Sekta ya Fedha ilichangia kustawisha viwanda na biashara nchini

NA GODFREY NNKO

SEKTA ya Fedha nchini Tanzania imeendelea kuimarika licha ya athari mbalimbali zilizosababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya UVIKO-19 ambazo zilidhoofika uchumi na shughuli mbalimbali za kijamii duniani.

Ripoti ya Mwaka 2021 ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha nchini imeonesha, utendaji wa sekta hiyo ulikuwa ukiimarika huku benki zikitoa mchango mkubwa katika kuhakikisha uthabiti wa sekta na uwezo wa kusaidia ufufuaji wa viwanda na biashara nchini.

Hayo yamebainishwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga kupitia Ripoti ya 25 ya Mwaka ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha ambayo hutoa taarifa kwa umma kuhusu utendaji na maendeleo katika Sekta ya Fedha, kwa mwaka uliomalizika Desemba 31, 2021.

Aidha, uchambuzi wa soko la benki ulionesha kuwa, benki 10 kubwa zilitawala soko mwaka 2021 na zilichangia asilimia 76.0 ya mali zote, asilimia 73.4 ya mikopo yote na asilimia 78.3 ya jumla ya amana.

Ripoti hiyo pia inahusu shughuli kuu zilizofanywa na benki katika utekelezaji wa majukumu yake, sekta ya fedha na udhibiti wa mabadiliko yaliyotokea.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa, hatua zilizochukuliwa katika kipindi hicho ni pamoja na kupunguzwa kwa Akiba ya Kisheria (Statutory Minimum Reserves-SMR), kulegeza masharti kwa mawakala wa benki,kuzuia kiwango cha riba kinacholipwa kwenye akaunti za uaminifu wa fedha katika simu.

Sambamba na kuanzishwa kwa mkopo maalum wa shilingi trilioni 1.0 kwa benki na taasisi za fedha kwa ajili ya kukopesha sekta binafsi kama mikopo ya kilimo na kupunguza uzito wa athari kwenye mikopo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatua hizo zilipelekea sekta hiyo kudumisha mtaji wa kutosha na viwango vya kutosha vya ukwasi ambavyo vilisaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Pia kwa mujibu wa Benki Kuu, kupitia ripoti hiyo ubora wa mali uliendelea kuimarika na kupungua kwa uwiano wa mikopo isiyolipika.

"Utendaji wa sekta ya fedha unahusisha uchambuzi wa sekta ndogo za benki na taasisi za fedha zisizo za benki kwa kuzingatia jumla ya mali, amana, mtaji na madeni.

"Aidha, utendaji wa sekta ya benki unahusisha uchambuzi wa Viashiria vya Ufanisi wa Kifedha (FSI), upimaji wa Kielelezo cha Uimara wa Mfumo wa Kifedha (FSSI). Kwa upande mwingine, utendaji wa mifuko ya pensheni ulihusisha uchambuzi wa jumla ya mali, michango ya wanachama na mapato ya uwekezaji,"imeeza sehemu ya ripoti hiyo iliyotolewa na Prof.Luoga.

Sekta ya Benki

Prof.Luoga amefafanua kupitia ripoti hiyo kuwa, katika mwaka huo, Sekta ya Benki iliendelea kuwa na faida, yenye mtaji wa kutosha, na kiwango cha kutosha cha ukwasi.

Sambamba na kuboreshwa kwa ubora wa mali, kutokana na kufufua biashara kutokana na athari mbaya za janga kubwa la UVIKO-19.

"Sekta iliendelea kuhimili mitikisiko ya ndani na nje na kuendelea kukua katika amana na mali, inayoungwa mkono na mazingira mazuri ya uchumi, hatua za udhibiti na usimamizi thabiti nchini,"amebainisha.

Mali

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sehemu kubwa za mali za sekta hiyo zilikuwa mikopo, malipo ya awali na malipo ya ziada ambayo ilichangia asilimia 56.2, fedha taslimu,Benki Kuu ya Tanzania, benki nyingine na mambo mengine yalichangia asilimia 17.8.

Pia kwa upande wa uwekezaji katika dhamana za madeni ulichangia asilimia 17.4, huku mali iliyobaki ikichangia asilimia 8.6 ya jumla ya mali zote.

Aidha, jumla ya mali ilikuwa kwa asilimia 13.4 hadi shilingi bilioni 39,346.3 ikilinganishwa na shilingi bilioni 34,689.5 katika mwaka 2020, mchango ambao ulitokana na ongezeko la amana, mikopo na mapato yaliyobaki.

Pia mikopo na malipo ya ziada yalikua kwa asilimia 11.0 hadi shilingi bilioni 20,822.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 18,765.1 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukuaji uliongezeka kutokana na mazingira mazuri ya uchumi, sera wezeshi ya fedha katika sekta ya benki na hatua za udhibiti zilizochukuliwa kusaidia ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

Wakati huo huo, rasilimali za mapato ziliongezeka kwa asilimia 13.1 hadi shilingi bilioni 31,981.1 ikilinganishwa na shilingi bilioni 28,362.5 iliyorekodiwa mwaka 2020.

Hata hivyo, uwiano wa mali zinazopata mapato kwa jumla yake ulipungua kidogo hadi asilimia 81.3 ikilinganishwa na asilimia 81.8 iliyorekodiwa mwaka 2020. Licha ya upungufu huo, uwiano kulingana na ripoti hiyo unaonesha kwamba, sehemu kubwa ya mali ya sekta hiyo iliendelea kuelekezwa kwenye sekta za uzalishaji uchumi nchini.

Madeni

Jumla ya madeni ya sekta yaliongezeka kwa asilimia 13.3 hadi shilingi bilioni 33,145.5 ikilinganishwa na shilingi
bilioni 29,267.3 zilizorekodiwa mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuongezeka kwa madeni kulichangiwa na ongezeko la amana na mikopo. Jumla ya amana iliongezeka kwa asilimia 15.1 hadi shilingi bilioni 28,499.1 kutoka shilingi bilioni 24,765.9 ambapo amana za fedha za ndani na nje ziliongezeka kwa asilimia 14.3 na asilimia 16.9 hadi shilingi bilioni 20,326.4 na shilingi bilioni 8,172.7 kwa mtiririko huo.

Ripoti hiyo imebainisha kwamba, ongezeko hilo lilihusishwa kwa kiasi fulani na mikakati iliyoimarishwa ya uhamasishaji wa amana na benki zilichangia asilimia 86.0 ya madeni yote. Aidha, mikopo iliongezeka kwa asilimia 8.0 hadi shilingi bilioni 3,007.6 kutoka bilioni 2,784.2.

Benki za Biashara

Hizi ni benki zenye leseni ya kutoa huduma kamili za benki bila vikwazo vya kijografia. Mwaka 2021, kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania, kulikuwa na benki 34 za biashara na matawi 899.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa, jumla ya mali za benki za biashara zilichangia asilimia 96.4 ya mali zote za taasisi za benki, ambapo benki za biashara zinazomilikiwa ndani na nje zilichukua asilimia 59.9 na asilimia 40.1 mtawalia.

Aidha, huduma za benki hizo zinatolewa kupitia matawi, ATM, benki kwa njia ya simu, benki kwa njia ya mtandao na mashine za kubadilisha fedha za kigeni (FX ATM).

Katika kipindi hicho, ripoti inaonesha kuwa, benki moja ya biashara ilikuwa na tawi moja la kidijitali ambalo huwawezesha wateja kufanya huduma za kibenki binafsi kama vile kuweka na kutoa fedha taslimu, kufanya miamala mtandaoni, kuweka hundi na benki nyinginezo SOMA RIPOTI KAMILI HAPA>>>

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news