Waziri Dkt.Kijaji ataja sababu ongezeko dogo la bei baadhi ya bidhaa za vyakula

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara, Dkt.Ashatu Kijaji amesema kuwa, hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kuondoa baadhi ya kodi na kutoa ruzuku kwenye mafuta ya petroli na dizeli umeleta nafuu kubwa kwenye soko.

Dkt.Kijaji ameyasema hayo leo Septemba 15, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kutoa taarifa za mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini katika kipindi cha Agosti 15 hadi Septemba 15, 2022.

"Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inashirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kutekeleza jukumu la kufuatilia na kufanya tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini. Taarifa ya leo ni mwendelezo wa utaratibu wa kutoa taarifa za kila mwezi kufuatia tathmini iliyofanywa na wizara kwa kushirikiana na wadau wengine.

"Ninapenda kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi imara wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, za kuendelea kuweka mazingira rafiki ya biashara nchini.

"Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuondoa baadhi ya kodi na kutoa ruzuku kwenye mafuta ya petroli na dizeli ili kuleta unafuu wa bei kwenye soko.

"Hata hivyo, kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba hali ya upatikanaji wa mafuta ya petroli na dizeli kwenye soko la dunia imeendelea kuimarika ambapo bei za bidhaa hizo zimeshuka na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji na usambazaji wa bidhaa. Kutokana na hali hiyo, tunatarajia katika siku zijazo bei za bidhaa nchini zitaendelea kushuka na kuleta unafuu katika soko la ndani,"amefafanua Dkt.Kijaji.

Ongezeko dogo

Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, matokeo ya tathmini iliyofanywa katika kipindi cha mwezi Agosti 15 hadi Septemba 15, 2022 imebainisha ongezeko dogo katika baadhi ya bidhaa za vyakula hususani mchele, mahindi, na maharage.

Amesema, kupanda kwa bei za bidhaa hizo ni kutokana na uhaba wa mvua kwenye maeneo mengi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 uliosababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao hayo.

"Takwimu za bei za baadhi ya mazao ya chakula zinakusanywa kutoka kwenye masoko mbalimbali kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia Wakusanya Taarifa za Masoko (Market Monitors).

"Aidha, taarifa za bei za baadhi ya bidhaa muhimu kama vile bidhaa za vyakula, vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine zinakusanywa kwa kutumia Maafisa Biashara wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini,"amesema Dkt.Kijaji.

Waziri amebainisha kuwa, kila mwezi Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakusanya taarifa za bei kutoka kwenye masoko yaliyopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa lengo la kukokotoa kiwango cha mfumuko wa bei kwa mwezi husika.

Amesema,bei za bidhaa kwa kila mkoa hupatikana kwa kukokotoa wastani wa bei za mazao na bidhaa hizo kutoka kwenye masoko yaliyopo kwenye mikoa hiyo.

Ujenzi

Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa saruji kwa mwaka 2020/21, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, ulikuwa tani 6,496,000.

"Aidha, kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa saruji umeongezeka kwa asilimia 0.5 hadi tani 6,531,000. Vilevile, uzalishaji wa nondo kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 278,000 na kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa nondo uliongezeka kwa asilimia 4.7 hadi tani 291,000.

"Pia, uzalishaji wa bati kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 108,000 na kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa bati uliongezeka kwa asilimia 5.6 hadi tani 114,000. Kiuchumi tunasema soko letu la vifaa vya ujenzi linakua na hii ni dalili njema kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi jumla wa Taifa letu,"amesema Dkt.Kijaji

Amesema,bei ya saruji kwa mfuko wa kilo 50 ni kati ya Shilingi 14,600 na 23,000. "Bei hiyo haina mabadiliko ikilinganishwa na bei ya saruji kwa mwezi Agosti.

"Aidha, bei za chini za saruji zipo kwenye mikoa ya Mtwara, Tanga, Lindi, Dar es Salaam na Kilimanjaro ambayo ni mikoa iliyo karibu na viwanda vya saruji. Bei za juu za saruji zipo kwenye mikoa ya Kigoma, Kagera, Mara, Simiyu na Mwanza kutokana na umbali wa mikoa hiyo kutoka kwenye viwanda na gharama za usafirishaji,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Kwa upande wa bei ya nondo za mm12, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema ni kati ya shilingi 23,000 na 28,000 kwa mwezi Septemba.

Amesema, bei hiyo imeshuka kutoka kati ya shilingi 24,500 na 30,000 kwa mwezi Agosti. "Bei za chini zipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Bei za juu za nondo zipo kwenye mikoa ya Njombe, Songwe, Rukwa na Katavi kutokana na umbali kutoka viwandani na gharama za usafirishaji,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Mabati

Akizungumzia kwa upande wa bei ya bati nyeupe za geji 30, amesema ni kati ya Shilingi 21,000 na 32,500 kwa mwezi Septemba.

Ikilinganishwa na bei ya kati ya Shilingi 22,000 na 28,500 kwa mwezi Agosti. Bei ya chini ya bati nyeupe ya mwezi Septemba ipo kwenye Mkoa wa Pwani na bei ya juu ipo kwenye Mikoa ya Njombe na Kigoma.

Mahindi

Waziri Dkt.Kijaji amesema, uzalishaji wa mahindi kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 7,039,064 na mahitaji yalikuwa tani 5,978,257 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya mahindi ya tani 1,060,807.

Aidha, amesema kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa mahindi ulishuka kwa asilimia 7.1 hadi tani 6,537,203 na mahitaji yaliongezeka kwa asilimia 0.9 hadi 6,034,943. Hivyo, ziada ya mahindi ilipungua kwa asilimia 56.6 hadi tani 502,260.

"Bei ya mahindi kwa mwezi Septemba ni kati ya Shilingi 900 na 1,550 kwa kilo ikilinganishwa na Shilingi 700 hadi 1,500 kwa mwezi Agosti. Aidha, bei ya chini ya mahindi ipo katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Manyara na Ruvuma. Bei ya juu ya mahindi ipo katika mikoa ya Pwani na Kagera,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Unga wa mahindi

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, bei ya unga wa mahindi ni kati ya Shilingi 1,250 na 2,000 kwa kilo kwa mwezi Septemba ikilinganishwa na Shilingi 1,400 hadi 1,700 kwa mwezi Agosti.

Bei ya chini ya unga wa mahindi ipo katika mikoa ya Iringa, Rukwa na Ruvuma. Bei ya juu ya unga wa mahindi ipo katika mikoa ya Kagera, Mara, Pwani, Shinyanga na Arusha.

Mchele

Amesema, uzalishaji wa mchele kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 2,686,829 na mahitaji yalikuwa tani 1,095,743 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya mchele ya tani 1,591,089.

Aidha, kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa mchele ulishuka kwa asilimia 30.9 hadi tani 1,856,731 na mahitaji yalikuwa tani 1,065,534.

"Hivyo, ziada ya mchele ilishuka kwa asilimia 50.3 hadi tani 791,198. Bei ya mchele ni kati ya Shilingi 2,000 hadi 3,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba, ikiwa imepanda kutoka kati ya shilingi 1,700 na 3,000 kwa mwezi Agosti.

"Bei ya chini ya mchele kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Kigoma. Bei ya juu ya mchele ipo katika mikoa ya Kagera, Dodoma, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Manyara, Singida na Arusha,"ameema Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Maharage

Akizungumzia upande wa uzalishaji wa maharage kwa mwaka 2020/21 amesema kuwa, ulikuwa tani 1,428,434 na mahitaji yalikuwa tani 553,791 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya maharage ya tani 879,643.

Aidha, kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa maharage ulishuka kwa asilimia 11.1 hadi tani 1,269,487 na mahitaji yalikuwa tani 488,753.

Hivyo, ziada ya maharage ilishuka hadi tani 780,734. Bei ya maharage amesema ni kati ya shilingi 1,750 na 3,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba; ikiwa imepanda kutoka kati ya shilingi 1,800 na 2,600 kwa kilo mwezi Agosti.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, bei ya chini ya maharage kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Katavi, Morogoro, Songwe, Kilimanjaro na Mbeya. Bei ya juu ya maharage ipo katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

Viazi mviringo

Amesema, bei ya viazi mviringo ni kati ya Shilingi 500 na 1,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba. Bei ya viazi haijaonesha mabadiliko ikilinganishwa na mwezi Agosti.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, bei ya chini ya viazi mviringo kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Manyara. Bei ya juu ya viazi mviringo ipo katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Arusha na Mara.

Akizungumzia kwa upande wa ulezi amesema kuwa, bei ni kati ya Shilingi 1,600 na 3,000 kwa kilo kwa mwezi Septemba.

"Bei ya chini ya ulezi imepanda kwa Shilingi 400 ikilinganishwa na mwezi Agosti. Bei ya chini ya ulezi kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Morogoro na Ruvuma na bei ya juu imeripotiwa kwenye mikoa ya Kagera na Shinyanga,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Mafuta ya kupikia

Wakati huo huo, Mheshimiwa Dkt.Kijaji amesema, bei ya mafuta ya kupikia ya alizeti ni kati ya shilingi 5,000 na 9,000 kwa lita kwa mwezi Septemba.

Bei ya mafuta ya kupikia haijaonesha mabadiliko ikilinganishwa na mwezi Agosti. Bei ya chini ya mafuta ya kupikia ipo katika mikoa ya Iringa, Njombe, Manyara, Dodoma, Singida na Songwe na bei ya juu imeripotiwa kwenye mikoa ya Lindi, Pwani na Tabora.

Aidha, kwa upande wa unga wa ngano amesema, bei ni kati ya shilingi 2000 na 2,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba. Bei ya chini ya unga wa ngano haijaonesha mabadiliko wakati bei ya juu imeongezeka kwa shilingi 1,500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Agosti ambayo ilikuwa kati ya shilingi 2,000 na 4,000.

Bei ya chini ya unga wa ngano ya Shilingi 2,000 ipo kwenye mikoa mingi nchini; wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Kagera, Arusha, Mbeya na Songwe.

Sukari

Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, bei ya sukari ni kati ya Shilingi 2,500 na 3,000 kwa kilo kwa mwezi Septemba. Bei ya sukari haijaonesha mabadiliko ikilinganishwa na mwezi Agosti.

Amesema, bei ya chini ya sukari kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Katavi, Kagera, Pwani, Rukwa na Ruvuma.

"Jitihada za Serikali za kuvutia uwekezaji kwenye uzalishaji wa sukari zimeanza kuzaa matunda kwa kuongezeka kwa kiasi cha sukari kinachozalishwa nchini baada ya upanuzi wa viwanda vilivyopo vya Kilombero na Kagera na ufunguzi wa kiwanda kipya cha sukari cha Bagamoyo.

"Ongezeko hilo la uzalishaji linatarajiwa kuendelea kupunguza pengo la uzalishaji na kuongeza uhimilivu wa bei ya sukari nchini.

"Nini maana ya takwimu hizi za uzalishaji wa bidhaa za vyakula? Tafsiri ya takwimu hizi za uzalishaji wa bidhaa za vyakula ni kwamba chakula kipo cha kutosha ndani ya Taifa letu kama takwimu zilivyoonyesha, hivyo hatuna upungufu wa chakula na Serikali inaendelea kufuatilia upatikanaji wa bidhaa za vyakula kwenye masoko yote nchini,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Hata hivyo, amesema kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa hizo ukilinganisha na mwaka jana lazima kutakuwa na mabadiliko kidogo ya bei za bidhaa hizo sokoni ukilinganisha na kipindi kama hiki mwaka jana, "kwani tupo kwenye biashara ya soko huria. Hii ni kanuni ya kawaida kabisa ya kiuchumi sokoni 'the price is determined by market forces,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Gesi ya kupikia

Akizungumzia kwa upande wa bei ya gesi yenye ujazo wa kilo 15, amesema ni kati ya Shilingi 53,000 na 60,000 kwa mwezi Septemba.

Mheshimiwa Waziri amesema, bei ya chini ya gesi ipo katika mikoa ya Kilimanjaro, Tabora na Mbeya; wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Kagera, Shinyanga, Simiyu na Ruvuma.

Akizungumzia kwa upande wa bei ya sabuni za mche, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema ni kati ya Shilingi 2,000 na 5,000 kwa mwezi Septemba.

"Bei ya chini imepungua kwa shilingi 1000 na bei ya juu imepanda kwa shilingi 500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Agosti ambayo ilikuwa ni kati ya shilingi 3,000 na 4,500.

"Bei ya chini ya sabuni za mche kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Katavi na Kigoma, wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Kagera, Iringa na Mtwara.

"Nipende kuuhakikishia umma wa watanzania kuwa, Serikali inaendelea kufuatilia na kufanya tathmini ya bei za bidhaa muhimu ili kuwalinda watumiaji, wazalishaji, na wafanyabiashara wa bidhaa husika,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kufanya majadiliano na wasambazaji wa bidhaa na wenye viwanda kwa lengo la kuhimiza umuhimu wa kuongeza ufanisi kwenye mifumo ya usambazaji wa bidhaa.

Ni ili kupunguza gharama za usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na hivyo kupunguza tofauti ya bei kati ya mikoa yenye viwanda na mikoa ya pembezoni.

"Lengo ni kufuata mfumo wa usambazaji unaotumiwa na wazalishaji wa baadhi ya bidhaa unaohakikisha usawa wa bei ya mlaji wa mwisho kwenye mikoa yote,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news