Serikali yavunja ukimya wafanyabiashara kudai wanadhulumiwa nje, kuzuiliwa mipakani na uhakika wa chakula

NA GODFREY NNKO

MHESHIMIWA Dkt.Ashatu Kijaji ambaye ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara amewataka wafanyabiashara wa Tanzania wanaokwenda nje au kushirikiana na wenzao wa nje kufanya biashara kuhakikisha kabla ya chochote wanasaini mikataba halali kisheria ili kuepuka kudhulumiwa.

"Kwa nini (wafanyabiashara) tunadhulumiwa? Kwa sababu tunaingia kwenye biashara bila kuwa na mikataba halali ya kazi tunayofanya. Ukiwa na mkataba halali ambao mmesainiana kisheria huwezi kudhulumiwa.

"Wale mliosoma uchumi mtakuwa mnajua kuna theory moja ya Game Theory...na sisi Watanzania sasa tuondoke huko ni kweli tunahitaji mahusiano zaidi, lakini biashara haifanyiki kimahusiano zaidi, inafanyika kwa misingi ya sheria, inalindwa na sheria, na sio sisi tu tunaodhulumiwa kule.

"Wiki iliyopita nilikuwa kwenye mkutano pale Kigali nchini Rwanda, walikuja wafanyabiahara wa kule wakilalamika wameingia makubaliano na sisi huku ya kuwapelekea bidhaa...kwanza tunapeleka bidhaa ambazo hazifiki kwenye standard ambayo tumekubaliana, na pili hatupeleki kwa kiwango tulichokubaliana, hali hiyo kwa nini inapatikana kwa sababu mikataba yetu hatujaiweka kisheria ili tukubaline na tufanye hivyo.

"Na hiyo inatupunguzia sana upatikanaji wa masoko na ulinzi wa masoko yetu, uhimilifu wa masoko unakuwa na mashaka akiharibu mmoja tumeharibikiwa wote.

"Aidha, tunadhulumiwa sisi au tudhulumu sisi humu ndani, lakini tutakuwa tumepoteza ule uaminifu kwenye biashara, tutajikuta tunazalisha masoko hakuna. Siku nyingine atatumia wenzetu wengine kwa sababu tunafanana kwenye jograghia yetu, tunazalisha nini, tunauza nini masoko ni yale yale, lazima hilo tulifanye kwa uaminifu mkubwa;
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt.Ashatu K.Kijaji.

Dkt.Kijaji ameyasema hayo Septemba 15, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kutoa taarifa za mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini katika kipindi cha Agosti 15 hadi Septemba 15, 2022.

Ambapo katika mkutano huo, mmoja wa waandishi wa habari alitaka kupata ufafanuzi wa Serikali kuhusu sababu zinazochangia baadhi ya wafanyabiashara kutoka nchini kudai wanapofanya biashara na wenzao wa nje ya nchi hususani ya mazao wamekuwa wakidhulumiwa.

Kwa wafanyabiashara

"Na huu ni wito wangu kwa wafanyabishara wote wa kitanzania. Twendeni kwenye biashara kwa mikataba, lakini tuhakikishe uaminifu wetu kwenye biashara ili tuweze kulinda masoko haya.

"Nitoe mfano tulipokuwa katika kongamano lile la siku tatu la eneo Huru la Biashara Afrika, tulijadili mengi na tunakwenda kuwa na soko moja kwa Afrika nzima, sasa tukipoteza uaminifu maana yake wataacha kununua kutoka kwetu na sisi tutabaki kuwa wasindikizaji,"amesema Dkt.Kijaji.

Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika ulianza Septemba 12, 2022 hadi 14, 2022 jijini Dar es Salaam huku ukiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, mkutano huo uliongozwa na kauli mbiu isemayo Wanawake na Vijana: Injini ya ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (Women and Youth: The Engine of AfCFTA Trade in Africa).

"Hii sio dhamira ya Serikali na ndio maana Mheshimiwa Rais wetu anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha masoko yanafunguka kwa ajili ya bidhaa tunazozalisha ndani ya Taifa letu.

"Sisi kama wizara, tumeamua kusimamia kwanza tuzalishe kwa standard zinazohitajika kule sokoni, lakini tunaanza vikao sasa na wafanyabiashara wetu tuhakikishe hatupotezi hii fursa njema ya kufunguliwa kwa taifa letu iliyofunguliwa na kipenzi chetu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ili tunufaike kwa pamoja, sisi tuwe ni washiriki hasa washindi kwenye hili soko moja la Afrika,"amefafanua Dkt.Kijaji.

Chakula kipo

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, "Hatuna upungufu wa chakula ndani ya taifa letu, tumepata upungufu wa uzalishaji kulingana na tulichokuwa tumezalisha mwaka uliopita.

"Kwa hiyo tumezalisha kidogo kuliko tulichokuwa tunazalisha mahitaji yetu tumeyasema kitakwimu mmeyasikia. Kwa hiyo meseji yetu kwa Watanzania tunachakula cha kutosha ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, Serikali imefanya mahesabu yake vizuri na kubaini kuwa chakula tulicho nacho kinatufikisha kwenye msimu mwingine wa uzalishaji nchini.

Kuzuiliwa

"Na wafanyabiashara ambao mliosema wamezuiliwa mpakani, hakuna mfanyabiashara aliyezuiliwa kule mpakani. Kwamba asinunue bidhaa hizi za vyakula ndani ya Taifa letu kupeleka kwenye nchi nyingine zilizotuzunguka, hayo ni makubaliano yetu kama Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"...Ununuzi holela, Watanzania mtakumbuka miaka miwili iliyopita yalikwenda mahindi yetu nchi jirani na tukaambiwa mahindi yale yana sumu kuvu, sasa tulichofanya sasa kama Serikali kwanza tunampongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia tu madarakani alifanya ziara nchini Kenya ya kufungua mipaka yetu na kweli mipaka yetu ikafunguka.

"Sasa ili tusirudi kule tulikotoka, Serikali sasa tumeamua kurasimisha ufanyaji huu wa biashara ili kwanza tuondokane na wafanyabiashara holela wanaokwenda mpaka kwa wakulima wetu kuwaumiza tuwajue waje na certificates zao walizoandikishwa kule kwao sio kwamba waje hapa tuwasajili kama kampuni, hapana.

"Anakuja kama kampuni, lakini aombe vibali vya kwenda kununua mahindi hayo tutambue kaingia nani, kaenda wapi, na mazao yote ya chakula aliyonunua yawe mazao salama, tunawapa cheti cha usalama wa mazao ambayo yanapelekwa nje ya nchi yetu, ili kuwalinda Watanzania, kuwalinda wazalishaji, na hao tunaowapelekea na kuhakikisha biashara yetu inakuwa salama.

"Nini kinatokea mmesema vizuri kumekuwa na uholela sisemi Watanzania, Waafrika sisi uholela tunaupenda sana. Kuondoka kwenye uholela kuja kwenye urasimishaji kuna changamoto yake, wengi hawapendi kuja kwenye mfumo rasimi wanataka kuendelea kununua kiholela kwa sababu ukishanunua kiholela lazima utakwenda kupita pale mpakani na sisi kama Serikali utatukuta tupo tutataka tuone una vyeti vyote.

"Tutajiridhisha pale mpakani kuona kama una vyeti hivyo tutakuuliza kuona chakula kinachokwenda ni salama tutajiridhisha sisi wanajiridhisha wao tunawafungulia wanakwenda. Kwa kuwa wanafika pale hawana vibali hivyo anachukua muda.

"Na kama serikali ili kupunguza ile foleni pale mpakani tumeweka utaratibu wa kujisajili online (mfumo wa mtandao) wala mfanyabiashara hahitaji kuja ofisini, anaingia online pale kwenye Wizara ya Kilimo anaomba kibali pale na wataalam wetu wanamfikia pale alipo tunajiridhisha na mazao aliyopewa na tayari sasa ni salama yaweze kwende huko kwa walaji ili tuwalinde Watanzania na soko letu wazalishaji wa bidhaa hizi,"amefafanua Waziri Dkt.Kijaji.

Ongezeko dogo

Wakati huo huo, Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, matokeo ya tathmini iliyofanywa katika kipindi cha mwezi Agosti 15 hadi Septemba 15, 2022 imebainisha ongezeko dogo katika baadhi ya bidhaa za vyakula hususani mchele, mahindi, na maharage.

Amesema, kupanda kwa bei za bidhaa hizo ni kutokana na uhaba wa mvua kwenye maeneo mengi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 uliosababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao hayo.

"Takwimu za bei za baadhi ya mazao ya chakula zinakusanywa kutoka kwenye masoko mbalimbali kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia Wakusanya Taarifa za Masoko (Market Monitors).

"Aidha, taarifa za bei za baadhi ya bidhaa muhimu kama vile bidhaa za vyakula, vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine zinakusanywa kwa kutumia Maafisa Biashara wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini,"amesema Dkt.Kijaji.

Waziri amebainisha kuwa, kila mwezi Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakusanya taarifa za bei kutoka kwenye masoko yaliyopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa lengo la kukokotoa kiwango cha mfumuko wa bei kwa mwezi husika.

Amesema,bei za bidhaa kwa kila mkoa hupatikana kwa kukokotoa wastani wa bei za mazao na bidhaa hizo kutoka kwenye masoko yaliyopo kwenye mikoa hiyo.

Ujenzi

Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa saruji kwa mwaka 2020/21, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, ulikuwa tani 6,496,000.

"Aidha, kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa saruji umeongezeka kwa asilimia 0.5 hadi tani 6,531,000. Vilevile, uzalishaji wa nondo kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 278,000 na kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa nondo uliongezeka kwa asilimia 4.7 hadi tani 291,000.

"Pia, uzalishaji wa bati kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 108,000 na kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa bati uliongezeka kwa asilimia 5.6 hadi tani 114,000. Kiuchumi tunasema soko letu la vifaa vya ujenzi linakua na hii ni dalili njema kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi jumla wa Taifa letu,"amesema Dkt.Kijaji

Amesema,bei ya saruji kwa mfuko wa kilo 50 ni kati ya Shilingi 14,600 na 23,000. "Bei hiyo haina mabadiliko ikilinganishwa na bei ya saruji kwa mwezi Agosti.

"Aidha, bei za chini za saruji zipo kwenye mikoa ya Mtwara, Tanga, Lindi, Dar es Salaam na Kilimanjaro ambayo ni mikoa iliyo karibu na viwanda vya saruji. Bei za juu za saruji zipo kwenye mikoa ya Kigoma, Kagera, Mara, Simiyu na Mwanza kutokana na umbali wa mikoa hiyo kutoka kwenye viwanda na gharama za usafirishaji,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Kwa upande wa bei ya nondo za mm12, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema ni kati ya shilingi 23,000 na 28,000 kwa mwezi Septemba.

Amesema, bei hiyo imeshuka kutoka kati ya shilingi 24,500 na 30,000 kwa mwezi Agosti. "Bei za chini zipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Bei za juu za nondo zipo kwenye mikoa ya Njombe, Songwe, Rukwa na Katavi kutokana na umbali kutoka viwandani na gharama za usafirishaji,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Mabati

Akizungumzia kwa upande wa bei ya bati nyeupe za geji 30, amesema ni kati ya Shilingi 21,000 na 32,500 kwa mwezi Septemba.

Ikilinganishwa na bei ya kati ya Shilingi 22,000 na 28,500 kwa mwezi Agosti. Bei ya chini ya bati nyeupe ya mwezi Septemba ipo kwenye Mkoa wa Pwani na bei ya juu ipo kwenye Mikoa ya Njombe na Kigoma.

Mahindi

Waziri Dkt.Kijaji amesema, uzalishaji wa mahindi kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 7,039,064 na mahitaji yalikuwa tani 5,978,257 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya mahindi ya tani 1,060,807.

Aidha, amesema kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa mahindi ulishuka kwa asilimia 7.1 hadi tani 6,537,203 na mahitaji yaliongezeka kwa asilimia 0.9 hadi 6,034,943. Hivyo, ziada ya mahindi ilipungua kwa asilimia 56.6 hadi tani 502,260.

"Bei ya mahindi kwa mwezi Septemba ni kati ya Shilingi 900 na 1,550 kwa kilo ikilinganishwa na Shilingi 700 hadi 1,500 kwa mwezi Agosti. Aidha, bei ya chini ya mahindi ipo katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Manyara na Ruvuma. Bei ya juu ya mahindi ipo katika mikoa ya Pwani na Kagera,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Unga wa mahindi

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, bei ya unga wa mahindi ni kati ya Shilingi 1,250 na 2,000 kwa kilo kwa mwezi Septemba ikilinganishwa na Shilingi 1,400 hadi 1,700 kwa mwezi Agosti.

Bei ya chini ya unga wa mahindi ipo katika mikoa ya Iringa, Rukwa na Ruvuma. Bei ya juu ya unga wa mahindi ipo katika mikoa ya Kagera, Mara, Pwani, Shinyanga na Arusha.

Mchele

Amesema, uzalishaji wa mchele kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 2,686,829 na mahitaji yalikuwa tani 1,095,743 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya mchele ya tani 1,591,089.

Aidha, kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa mchele ulishuka kwa asilimia 30.9 hadi tani 1,856,731 na mahitaji yalikuwa tani 1,065,534.

"Hivyo, ziada ya mchele ilishuka kwa asilimia 50.3 hadi tani 791,198. Bei ya mchele ni kati ya Shilingi 2,000 hadi 3,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba, ikiwa imepanda kutoka kati ya shilingi 1,700 na 3,000 kwa mwezi Agosti.

"Bei ya chini ya mchele kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Kigoma. Bei ya juu ya mchele ipo katika mikoa ya Kagera, Dodoma, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Manyara, Singida na Arusha,"ameema Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Maharage

Akizungumzia upande wa uzalishaji wa maharage kwa mwaka 2020/21 amesema kuwa, ulikuwa tani 1,428,434 na mahitaji yalikuwa tani 553,791 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya maharage ya tani 879,643.

Aidha, kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa maharage ulishuka kwa asilimia 11.1 hadi tani 1,269,487 na mahitaji yalikuwa tani 488,753.

Hivyo, ziada ya maharage ilishuka hadi tani 780,734. Bei ya maharage amesema ni kati ya shilingi 1,750 na 3,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba; ikiwa imepanda kutoka kati ya shilingi 1,800 na 2,600 kwa kilo mwezi Agosti.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, bei ya chini ya maharage kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Katavi, Morogoro, Songwe, Kilimanjaro na Mbeya. Bei ya juu ya maharage ipo katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

Viazi mviringo

Amesema, bei ya viazi mviringo ni kati ya Shilingi 500 na 1,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba. Bei ya viazi haijaonesha mabadiliko ikilinganishwa na mwezi Agosti.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, bei ya chini ya viazi mviringo kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Manyara. Bei ya juu ya viazi mviringo ipo katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Arusha na Mara.

Akizungumzia kwa upande wa ulezi amesema kuwa, bei ni kati ya Shilingi 1,600 na 3,000 kwa kilo kwa mwezi Septemba.

"Bei ya chini ya ulezi imepanda kwa Shilingi 400 ikilinganishwa na mwezi Agosti. Bei ya chini ya ulezi kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Morogoro na Ruvuma na bei ya juu imeripotiwa kwenye mikoa ya Kagera na Shinyanga,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Mafuta ya kupikia

Wakati huo huo, Mheshimiwa Dkt.Kijaji amesema, bei ya mafuta ya kupikia ya alizeti ni kati ya shilingi 5,000 na 9,000 kwa lita kwa mwezi Septemba.

Bei ya mafuta ya kupikia haijaonesha mabadiliko ikilinganishwa na mwezi Agosti. Bei ya chini ya mafuta ya kupikia ipo katika mikoa ya Iringa, Njombe, Manyara, Dodoma, Singida na Songwe na bei ya juu imeripotiwa kwenye mikoa ya Lindi, Pwani na Tabora.

Aidha, kwa upande wa unga wa ngano amesema, bei ni kati ya shilingi 2000 na 2,500 kwa kilo kwa mwezi Septemba. Bei ya chini ya unga wa ngano haijaonesha mabadiliko wakati bei ya juu imeongezeka kwa shilingi 1,500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Agosti ambayo ilikuwa kati ya shilingi 2,000 na 4,000.

Bei ya chini ya unga wa ngano ya Shilingi 2,000 ipo kwenye mikoa mingi nchini; wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Kagera, Arusha, Mbeya na Songwe.

Sukari

Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, bei ya sukari ni kati ya Shilingi 2,500 na 3,000 kwa kilo kwa mwezi Septemba. Bei ya sukari haijaonesha mabadiliko ikilinganishwa na mwezi Agosti.

Amesema, bei ya chini ya sukari kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Katavi, Kagera, Pwani, Rukwa na Ruvuma.

"Jitihada za Serikali za kuvutia uwekezaji kwenye uzalishaji wa sukari zimeanza kuzaa matunda kwa kuongezeka kwa kiasi cha sukari kinachozalishwa nchini baada ya upanuzi wa viwanda vilivyopo vya Kilombero na Kagera na ufunguzi wa kiwanda kipya cha sukari cha Bagamoyo.

"Ongezeko hilo la uzalishaji linatarajiwa kuendelea kupunguza pengo la uzalishaji na kuongeza uhimilivu wa bei ya sukari nchini.

"Nini maana ya takwimu hizi za uzalishaji wa bidhaa za vyakula? Tafsiri ya takwimu hizi za uzalishaji wa bidhaa za vyakula ni kwamba chakula kipo cha kutosha ndani ya Taifa letu kama takwimu zilivyoonyesha, hivyo hatuna upungufu wa chakula na Serikali inaendelea kufuatilia upatikanaji wa bidhaa za vyakula kwenye masoko yote nchini,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Hata hivyo, amesema kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa hizo ukilinganisha na mwaka jana lazima kutakuwa na mabadiliko kidogo ya bei za bidhaa hizo sokoni ukilinganisha na kipindi kama hiki mwaka jana, "kwani tupo kwenye biashara ya soko huria. Hii ni kanuni ya kawaida kabisa ya kiuchumi sokoni 'the price is determined by market forces,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Gesi ya kupikia

Akizungumzia kwa upande wa bei ya gesi yenye ujazo wa kilo 15, amesema ni kati ya Shilingi 53,000 na 60,000 kwa mwezi Septemba.

Mheshimiwa Waziri amesema, bei ya chini ya gesi ipo katika mikoa ya Kilimanjaro, Tabora na Mbeya; wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Kagera, Shinyanga, Simiyu na Ruvuma.

Akizungumzia kwa upande wa bei ya sabuni za mche, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema ni kati ya Shilingi 2,000 na 5,000 kwa mwezi Septemba.

"Bei ya chini imepungua kwa shilingi 1000 na bei ya juu imepanda kwa shilingi 500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Agosti ambayo ilikuwa ni kati ya shilingi 3,000 na 4,500.

"Bei ya chini ya sabuni za mche kwa mwezi Septemba ipo katika mikoa ya Katavi na Kigoma, wakati bei ya juu ipo kwenye mikoa ya Kagera, Iringa na Mtwara.

"Nipende kuuhakikishia umma wa watanzania kuwa, Serikali inaendelea kufuatilia na kufanya tathmini ya bei za bidhaa muhimu ili kuwalinda watumiaji, wazalishaji, na wafanyabiashara wa bidhaa husika,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kufanya majadiliano na wasambazaji wa bidhaa na wenye viwanda kwa lengo la kuhimiza umuhimu wa kuongeza ufanisi kwenye mifumo ya usambazaji wa bidhaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news