Wiki ya Maonesho ya Biashara na Uwekezaji Pwani yakaribia, RC Kunenge ateta na wadau

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inaendelea kutatuta changamoto zinazowakabili wawekezaji wa viwanda na wafanyabiashara.
Kunenge ametoa kauli hiyo Septemba 15 katika kikao maalum kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo,wafanyabiashara na wawekezaji wa viwanda waliopo mkoani Pwani.

Aidha, Kunenge amesema lengo la kikao hicho ni kutaka kuwahamasisha wadau hao kushiriki katika maonesho ya wiki ya biashara na uwekezaji yanayotarajia kuanza Oktoba 5 mpaka Oktoba 10, mwaka huu katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo Kibaha Mailimoja.

Kunenge amesema, kufanyika kwa maonesho hayo ni fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji hao kwani yatasaidia katika kutangaza bidhaa zao na hata kupata fursa mpya zilizopo katika Mkoa wa Pwani.

"Nitumie fursa hii kuwaomba wawekezaji wote kujitokeza kwa ajili ya kushiriki maonesho haya,Mkoa wa Pwani ndio mkoa pekee wenye viwanda vingi, kwa hiyo kujitokeza kwa wingi itakuwa sehemu ya kumrudishia heshima Rais wetu ambaye amekuwa akipambana kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa, Serikali inatambua changamoto zinazowakabili ikiwemo suala Umeme,Barabara na Maji lakini tayari changamoto hizo zimeanza kufanyiwakazi katika maeneo tofauti na muda sio mrefu changamoto hizo zitakuwa historia.
Amesema,kuhusu maji tayari Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi wa bwawa la Kidunda ambao kukamilika kwake utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji zaidi ya Lita milioni 7 kwa siku na kwamba maji hayo yatatumika Mkoa wa Morogoro,Pwani na Dar es Salaam.

Kunenge amesema, suala la barabara tayari linafanyiwa kazi na kwamba maeneo yote ya viwanda zinajengwa barabara za lami ikiwemo eneo la Zegereni , Vigwaza-Kwala na hata barabarani nyingine.

Ameongeza kuwa, jitihada zinazofanyika katika sekta ya maji na barabara vilevile zinafanyika katika sekta ya umeme na kwamba baada ya miezi michache kila kiwanda kitakuwa kinapata umeme wa kutosha.

"Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha changamoto zenu zinatatuliwa na tayari ameshaanza kutoa fedha na kazi zinafanyika,niwaombe wawekezaji kutumia fursa hii ya maonesho ili kumtia moyo Rais,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa,katika kuandaa maonesho hayo mkoa umeunda timu maalum ya ufuatiliaji na kwamba yeyote anayetaka kushiriki atapewa utaratibu maalum na mzuri kwa ajili ya kuonyesha bidhaa zake .

Kunenge amewaomba wamiliki wa viwanda waliopo mkoani Pwani kuhakikisha wanalipa ushuru wa huduma (Service Levy) katika Mkoa wa Pwani ili kusaidia kukuza pato la mkoa na kwamba mapato hayo yatasaidia kutengeneza barabara,kuleta maji na umeme.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, Abdallah Ndauka,amempongeza Mkuu huyo wa Mkoa na kamati yake kwa kuandaa wiki ya biashara na uwekezaji na kusema viwanja vinavyotumika kufanya maonesho hayo ni mazuri.

Ndauka amesema miaka ya nyuma wakati maonesho hayo yakifanyika kulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wawekezaji kukaa nyuma kiasi cha kushindwa kufikiwa na wageni muhimu.

Pia ameomba changamoto hizo zifanyiwe kazi ili kusudi maonesho hayo yawe bora kiasi ambacho kitawavutia wawekezaji na wafanyabiashara kupenda kushiriki katika maonesho hayo pale yanapofanyika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news