Soko la Machinga jijini Dodoma lakamilika

NA REVINA TURNER

SOKO la wazi la Machinga lililojengwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma limekamilika kwa asilimia 100 na wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) kuanza kuingia na kufanya biashara zao katika mazingira salama na rafiki kwao na wateja.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru (katikati) akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Dennis Gondwe akifuatilia kwa utulivu na Afisa Biashara, Donatila Vedasto (kulia).

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari kuwapa taarifa ya kukamilika kwa soko hilo na utaratibu wa kuwahamisha Machinga maeneo ya mjini, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa soko la wazi la Machinga limekamilika kwa asilimia 100 katika eneo la Barabara ya Bahi na wafanyabiashara hao wanaanza kuingia.

Alisema kuwa, shughuli ya kuhama Machinga kutoka maeneo yasiyo rasmi ya katikati ya mji imeanza na inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 23 Septemba, 2022.

Kuanzia tarehe 24 Septemba, 2022 hakutakuwa na Machinga katika maeneo yasiyo rasmi badala yake Machinga wote watakuwa katika soko la wazi la Machinga, aliongeza.

Akiongelea uwezo wa soko hilo, alisema kuwa lina uwezo wa kubeba wafanyabiashara 5,000. Alisema kuwa wafanyabiashara walioakikiwa ni 3,000 hivyo, waliopo mtaani wote wataondoka na watakapokuja wafanyabiashara wapya wataongezwa kwa kuzingatia sifa zilizowekwa. “Kwa hiyo yeyote hata kama ndio unaanza leo utaingia kwenye soko na hata kama utakosa pale utaingia kwenye masoko tuliyoyaandaa ila utaratibu ni kwamba kwa wale tuliowasajili mwanzo watatangulia na wale wanaoongezeka tutaendelea kuwapokea” alisema Mafuru.

Akiongelea usalama katika soko hilo, Mkurugenzi wa Jiji alisema kuwa usalama umezingatiwa kwa kiwango cha juu. Alisema kuwa soko hilo lina kituo cha Polisi kitakachofanya kazi saa 24.

Alisema kuwa soko hilo limefungwa mifumo ya kisasa ya Tehama Pamoja na mfumo wa camera za usalama CCTV kuwahakikishia usalama wafanyabiashara, wateja wao na mali zao. Ujenzi wa soko la wazi la Machinga umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.53 mpaka kukamilika kwake ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi bilioni tatu na Halmashauri Jiji tulitoa kiasi cha shilingi bilioni sita na nusu kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news