'Tanzania itaendelea kushirikiana na AU, UN kushughulikia changamoto za amani na usalama'

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ameshiriki Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika katika Ofisi za Uwakilishi za Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa jijini New York.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Robert Kahendaguza aliposhiriki katika Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika katika Ofisi za Uwakilishi za Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa Jijini New York.

Akizungumza katika mkutano huo Balozi Mulamula ameuhakikishia Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania iko tayari na itaendelea kushirikiana na jumuiya hizo kushughulikia changamoto za amani na usalama.

Amesema utayari huo wa Tanzania unakwenda sambamba na kufanya mapambano dhidi ya ugaidi wa aina zote kuwa kipaumbele katika nchi zote na kutoa wito wa kuanzishwa kwa kamati ya mawaziri ya kukabiliana na ugaidi kama ilivyokubaliwa wakati wa mkutano wa AU uliofanyika mjini Malabo.

Amesema vita dhidi ya ugaidi na vitendo vyote vya kigaidi vinahitaji nguvu ya kushirikiana pamoja kwa ngazi zote kuanzia taasisi, nchi, kanda na taasisi za kimataifa na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuunganisha kazi ya uangalizi ya Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika ili kuwa na uratibu wa pamoja.

Amezisihi nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kusaini na kuridhia mikataba muhimu kama Mkataba wa kuzuia na kupambana na ugaidi; Mkataba wa Umoja wa Afrika wa ushirikiano wa kuvuka mipaka na Mkataba wa Afrika wa Ulinzi wa Usafiri majini,usalama na maendeleo ili kuimarisha nguvu katika kupambana na ugaidi, vitendo vya kidhalimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news