TANZANIA YAJIPANGA KUKABILIANA NA MAAFA IKIWA NI NCHI WANACHAMA SADC

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema itachukua hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza shughuli zote zinazosababisha madhara ambayo yanaweza kusababisha majanga.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene ofisini kwake bungeni jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Msumbiji uliojadili kuhusu namna ya kuchukua tahadhari ya mapema katika hatua za kudhibiti Majanga.

Mhe. Simbachawene alisema, miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni pamoja na kuweka mifumo thabiti ya utayari kuhakikisha wananchi wanachama wanapata taarifa mapema pindi majanga yanapotokea na kudhibiti ukubwa wa madhara yake, na kuhakikisha makundi yaliyo katika hatari ya kuathirika na majanga wakiwemo Wanawake, Watoto na Watu Wenye Ulemavu wanafikiwa ili kuchukua hatua za tahadhari.

“Eneo lingine ni kuongeza uwekezaji ili kuimairisha taasisi zinazohusika na mifumo ya tahadhari za mapema na huduma za usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa kisheria wa kuziwezesha mamlaka zenye dhamana ya tahadhari kama hapa kwetu ni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA), wanaokusanya taarifa na kuzipeleka na kushirikiana na vitengo vinavyohusika na majanga,”alisema. Mhe. Simbachawene.

Aidha, amewahimiza wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotelewa na wataalam na kuzitumia katika shughuli za kila siku pamoja na watu wanaoishi katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa kuwa na mfumo wa kubadilishana taarifa na kusaidiana kitaasisi hatua itakayosadia kuepuka majanga kabla hayajatokea.

Ikumbukwe Mkutano huo wa siku mbili ulifanyika Mjini Maputo Nchini Msumbiji ulifunguliwa na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi kwa lengo la kupokea maoni ya maandalizi ya maafa na namna ya kushughulikia na kutekeleza maelekezo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress aliyezitaka nchi kuhakikisha raia wake wanapokea taarifa zinazoweza kusababisha majanga ikiwa ni mkakati wa kimataifa wa kupunguza madhara ya maafa ifikapo mwaka 2030.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news