Wateja wa Tigo Tanzania kupata burudani bure kupitia Boomplay

NA GODFREY NNKO

WATEJA wa Tigo nchini Tanzania kuanzia sasa baada ya kujiunga na vifurushi vya siku,wiki au mwezi watasilikiza muziki bure kupitia App ya Boomplay.Sambamba na punguzo la asilimia 30 pale watakapohitaji kujiunga na malipo ya siku,wiki au mwezi ya Boomplay.
 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tigo Tanzania,William Mpinga akizungumza.

Haya yanajiri baada ya Tigo Tanzania kusaini na kutangaza ushirikiano wa kimkakati kupitia programu hiyo tumishi ambayo inashikilia nafasi ya kwanza barani Afrika ya Boomplay kama sehemu ya Kampeni ya Wakishua.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tigo Tanzania, Bw.William Mpinga ameyabainisha hayo leo Septemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi mbalimbali wa habari kuelezea kuhusu ushirikiano huo.

"Mtandao wa Tigo umekuwa ukisaidia tasnia ya muziki kwa muda sasa kwa kutoa fursa kwa wasanii kuungana na mashabiki wao,hivyo tuna furaha kutoa jukwaa litakaloendeleza dhumuni hili.

"Tunatambua hitaji la wateja nchini Tanzania kuwa na chaguzi zaidi za kupata muziki na burudani na kukidhi hitaji hili, hakuna mtoa huduma bora wa kushirikiana nae zaidi ya Boomplay. Kupitia kampeni hii ya Wakishua, tunawapa wateja wetu jukwaa la kidijitali ili kusikiliza bila malipo, ubora wa sauti na machaguo mapya ya muziki,"amefafanua Bw.Mpinga.

Ushirikiano huu wa kimkakati baina ya Tigo na Boomplay unakuja katika kipindi ambacho, programu hiyo tumishi imejaa utajiri wa mamilioni ya nyimbo, video na habari za burudani.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, Boomplay ambayo inaongozwa kwa utoaji wa huduma za kupakua na kusikiliza muziki barani Afrika huwawezesha watumiaji wake kutimiza mahitaji au machaguo yao wanayoyapenda ikiwemo kujiunga na huduma za kipekee kama kusikiliza muziki bila matangazo na kuhifadhi muziki kwa ajili ya kusikiliza baadaye bila bando.

Ikiwa na zaidi ya watumiaji milioni 70 wa kila mwezi na idadi ya nyimbo zaidi ya milioni 80, Boomplay inapatikana duniani kote kupitia programu tumishi za Android, IOS na katika tovuti yake.

Meneja Mkuu wa Boomplay Tanzania, Natasha Stambuli akizungumzia ushirikiano huo amesema kuwa, "Maono yetu ni kuwezesha sekta ya muziki wa Kiafrika na kuhakikisha unafika mahali pazuri, hivyo, tuna matumaini makubwa kupitia ushirikiano huu na Tigo.

"Tunaamini ushirikiano wetu utaongeza usikilizwaji wa nyimbo zaidi ya milioni 85 kwenye App ya Boomplay na kuongeza kipato kwa wasanii wa Tanzania katika siku za usoni,"amesema.

Wakati huo huo,Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tigo Tanzania, Bw.William Mpinga amesema kuwa, Kampeni ya Wakishua inaruhusu wapenzi w amuziki kuwasikiliza wasanii wanaowapenda kutoka ndani na nje ya Tanzania.

"Ni kwa kutumia fursa ya ofa yya usikilizaji muziki bila malipo kupitia Boomplay na hatimaye kuongeza kipato kwa wasanii hao. Na wateja sasa wanaweza kufurahi machaguo mbalimbali ya muziki kwenye App ya Boomplay kwa kununua kifurushi chochote kutoka Tigo.

"Kwa wale ambao bado hawapo kwenye mtandao wa Tigo, wanaweza kupata SIM kadi ya Tigo kote nchini na kupakua App ya Boomplay na kuwa sehemu ya kundi la Wakishua,"amesema Bw.Mpinga.

Tigo ambayo ilianzishwa mwaka 1994 ikiwa mtandao wa kwanza Tanzania wa simu za mkononi, ni kampuni ya mawasiliano yenye ubunifu mkubwa nchini ambayo inatoa huduma zinazolenga kuleta mageuzi ya kidigitali katika maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake msanii wa kizazi kipya, Mario amesema kuwa, huduma hiyo mpya ya kusikiliza muziki kupitia mtandao kwenye programu tumishi itazidi kuwatangaza wasanii na kuwaingizia kipato kutokana na kazi zao kusikilizwa za mamilioni ya watu.

Mario amesema, kupitia Kampeni ya Wakishua mashabiki wa muziki watapata fursa kupakua na kusikiliza muziki wa wasani mbalimbali bure

“Binafsi nawashukuru sana Tigo Tanzania na Boomplay kwa kuja na huduma hii ambayo ni fursa mpya kwa wasanii kuingiza kipato na kujitangaza duniani kote,"amesema Msanii huyo wa kizazi kipya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news