WAZIRI MKUU AKEMEA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA ZA UMMA

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitakubaliana na mtumishi yeyote atakayehusika na matumizi mabaya ya fedha za umma, hivyo amewasisitiza viongozi wazisimamie vizuri ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendelezo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Isike Mwanakinyungi katika Manispaa ya Tabora kwa ajili ya Kikao na Viongozi wa Mkoa wa Tabora, Septemba 8, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Tuendelee kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki kuanzia ngazi ya halmashauri kwa lengo la kupata fedha zitakazotumika kujenga miradi ya wananchi ambayo kila siku lazima iwahudumie. Jukumu hili ni letu sote.”

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Septemba 8, 2022 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Tabora kwenye ukumbi wa Isike Mwanakiyungi akiwa katika ziara ya kikazi siku mbili mkoani hapa.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa halmashauri kuwa ni lazima wasimamie ukusanyaji wa mapato na fedha zote zinazopatikana zipelekwe benki kwa wakati.

“Tabora mapato yaliyokusanywa yakishaingia benki tuna wajibu wa kuyatumia kwa uwazi kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Sheria, kanuni na taratibu zilizopo lazima zitumike katika matumizi haya, hizi ni fedha za umma.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi wa halmashauri zote wasikubali mawakala kufanya kazi ya ukusanyaji wa mapato bila ya kuwa na mikataba. “Lazima muione na mridhike nayo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona usimamizi katika kila eneo unaimarishwa.”

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia mara zote anawasisitiza watumishi wa umma kuwatumikia wananchi, hivyo kila wanachokifanya katika maeneo yao lazima kiwe na viwango kulingana na taaluma waliyonayo. “Haya ndio matamanio ya Rais wetu.”

“Ndugu viongozi wenzangu ni lazima wananchi waelezwe miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yenu, hata fedha za utekelezaji wa miradi mnazopokea ni muhimu kuwajulisha. Viongozi hakikisheni watumishi wanatenga muda na kwenda kwa wananchi hususani waishio vijijini kwa ajili ya kusikiliza kero zao.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora linalojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.73 ambazo ni ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt. Peter Nyanja amesema mbali na jengo hilo kutumika kama ofisi za Idara mbalimbali za Manispaa hiyo, pia wataanzisha kituo cha pamoja cha utoaji wa huduma kwa ajili ya wawekezaji na huduma za kibenki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news