Wizara yapokea maoni, mapendekezo ya wadau wa Sekta ya Milki Tanzania

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeyapokea maoni na mapendekezo ya wadau wa Sekta ya Milki nchini kuhusu mapitio ya sera, sheria, kanuni na mifumo ya kutoa maamuzi ambayo wamedai imekuwa kikwazo kwao ili waweze kushiriki kikamilifu kutoa huduma bora nchini.

Hayo yamesemwa Septemba 2, 2022 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula wakati akifunga mkutano wa wadau wa Sekta ya Milki nchini

Katika mkutano huo ulioanza Septemba Mosi hadi 2, 2022 jijini Dar es Salaam washiriki 230 walikuwa ukumbini tofauti na wale ambao walishiriki mubashara kutoka ndani na nje ya nchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Dkt.Mabula amesema kuwa,michango na maoni ambayo yametolewa na wadau hao wameyapokea yote kama wizara kwa ajili ya kuwapa mwelekeo na kwenda kuboresha,kuimarisha na kukuza Sekta ya Milki Tanzania kwa manufaa endelevu ya jamii na nchi nzima.

"Tunayaheshimu sana maoni na mapendekezo yenu haya mazuri. Lakini pia katika mapendekezo yenu kuna masuala machache ambayo nitayagusia ambayo mmeyazungumza mmesema kuwa, Serikali ifanye mapitio ya sera, sheria na kanuni na mifumo ya kutoa maamuzi kwani imekuwa ni kikwazo.

"Hili tumelichukua vizuri na linafanyiwa kazi, na niwahakikishie kwenye sera haya ambayo mmeyazungumza na kwa sababu sera ambayo inakwenda kurekebishwa hata ile ya ardhi ipo katika mchakato,mwisho itakwenda kutoka,tunayo ile sera ya nyumba na makazi nazo zipo.

"Kwa hiyo kwa mchango wenu mlivyotoa tuna imani tutakwenda kutoa sera nzuri na mwisho wa siku tutapata sheria nzuri ambayo itakwenda kukidhi matarajio ya wadau ambao ni ninyi na wale ambao mmewawakilisha katika huu mkutano,"amesema Waziri Dkt.Mabula.

Amesema, Serikali imedhamiria hapa nchini kunakuwepo na miji na makazi bora yalipongika vizuri na yenye usalama na miundombinu yote muhimu ikiwemo barabara, umeme na maji kwa ustawi bora wa jamii.

Pia amesema, wizara yake itaweka utaratibu mzuri wa kuendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau na wananchi ili kuwepo na mabadiliko ya kasi katika Sekta ya Milki nchini.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, Sekta ya Milki ikitumika vema ni sehemu ambayo itazalisha ajira nyingi zaidi na itakuza uchumi kwa maslahi mapana ya jamii na taifa.

Pia Mheshimiwa Waziri amewataka wadau hao kufanya kazi kwa bidii na weledi ili Sekta ya Milki nchini ambayo imepewa Kurugenzi Maalum kwa ajili ya kuisimamia ili iweze kuwa na tija.

"Tunalo bango kitita ambalo lina hoja karibu 20 zilizotoka kwenu,naomba niwaahidi kwamba tunakwenda kufanyia kazi.Kama (Sekta ya Milki) itasimama vizuri na kama waendelezaji miliki watatumia utaalamu wao na fursa zao vizuri, ninaweza nikakuhakikishia hakuna sekta ambayo inaweza ikatoa ajira za kutosha, hakuna sekta ambayo inaweza kukuza uchumi kwa haraka, hakuna sekta ambayo inagusa kila eneo kama sekta hii. Hii ni sekta muhimu sana nchini,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amewataka watu wenye tabia ya kuchochea na kuchonganisha Serikali na wananchi kuacha tabia hiyo, kwani inasababisha kuzorota kwa mahusiano baina ya pande hizo mbili nchini.

“Jana (Septemab 1, 2022) hapa nilizizungumzia kuhusu kupiga marufuku uuzaji viwanja vya 20 kwa 20 kwenye miradi ya uuzaji wa ardhi, watu wanajitokeza kwenye mitandao na kusema Serikali haitaki watu wakipato cha chini kunufaika kupitia miradi hiyo wakati sio kweli.

“Serikali inapinga hilo kwa kulinda maslahi ya wananchi, wanasema wanauza kusaidia wananchi wa kipato cha chini lakini ukiangalia bei yake ni ghali unakuta kiwanja ni 20 kwa 20, lakini kinauzwa zaidi ya milioni 10. Hakuna huduma za kijamii,hakuna barabara zenye mapana, sasa hata ukitaka kupitisha huduma za maji na umeme inashindikana sasa unakuwa umemsaidia mwananchi ama umemwangamiza,"amehoji Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Awali, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula wakati akifungua mkutano huo alisema kuwa, hivi karibuni wizara imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wananchi ya kutaka kupimiwa maeneo yao ambayo wanadai kuuziwa na baadhi ya makampuni yakiwa hayajapangwa wala kupimwa.

“Makampuni hayo yananunua maeneo na kukata viwanja vidogo vidogo vyenye ukubwa chini ya mita za mraba 300 bila kuzingatia sheria na mahitaji ya huduma za jamii katika maeneo hayo na kisha kuuza kwa wananchi.

“Maeneo hayo barabara hazifiki upana wa mita nne. Baada ya kuwauzia wananchi wanawaelekeza kufika wizarani kwa ajili ya kupimiwa. Wakati huo wameshauza na kuleta migogoro ya matumizi ya ardhi.Kampuni hizo tumeshazibaini tunaangalia namna ya kuzichukulia hatua kwa mujibu wa sheria,”alibainisha Waziri Dkt.Mabula.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mipangomiji Na 8 ya Mwaka 2007 Sura 355, Kifungu Na. 77 (1) ((b)), ((i)), Kanuni za viwango vya upangaji wa maeneo zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na 91 na 93 la tarehe 9/03/2018, ukubwa wa maeneo kwa matumizi mbalimbali umeainishwa.

Aidha, kwa mujibu wa sheria hiyo na taaluma ya mipangomiji, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, viwanja vya matumizi mbalimbali vinatakiwa kuwa na ujazo wa aina mbalimbali kama ujazo wa juu (high density), ujazo wa kati (medium density) na ujazo wa chini (low density) ambapo viwanja hivyo vinatakiwa kuwa na mapana na marefu yenye uwiano wa 1:2 mpaka 1:2.5.

“Kwa mfano, kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 400 kinapaswa kuwa katika uwiano wa upana wa mita 16 na urefu wa mita 25, uwiano wa 1:1 yaani 20 kwa 20 haukubaliki kitaalam na hakuna kiwanja chenye upana na urefu ulio sawa,”alisema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Waziri Dkt.Mabula alisema,taaluma ya mipangomiji inaelekeza pia kuwa mpangilio wa viwanja kuhusiana na ujazo (density) unategemea mambo mengi ikiwemo umbali kutoka barabara kubwa, umbali kutoka eneo la maji (bahari, ziwa, mto), milima na mabonde.

“Mambo haya yote hayazingatiwi kwenye soko huria la uuzaji wa vipande vya ardhi, na jambo hili limeleta kero kubwa kwa jamii pamoja na kuathiri madhari au muonekano wa miji yetu. Kwa kuwa miji yetu inatakiwa kuwa na maendeleo endelevu ikiwemo makazi na sehemu zingine za jamii,”alisema Mheshimiwa Waziri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news