ALHAMDU LILLAH RABBIL ALAMIIN

NA ADELADIUS MAKWEGA

KUNA wakati nilipigiwa simu na ndugu yangu mmoja Mtanzania anayefanya kazi na vyombo vya habari vya Kimataifa, ninayefahamiana naye muda mrefu sana, kwanza ndugu yangu huyu anayependa kilimo aliniuliza juu ya kilimo cha migomba kama ninaendelea nacho?.

Nilimjibu kuwa naendelea kulima na kupanda kidogo kidogo japokuwa hali yangu ni ngumu, lakini Mwenyenzi Mungu ananipigania ninaendelea. Hata lolote likitokea wanangu wanaweza kuvuna ndizi za kula na watasema mgomba huu amepanda baba.

“Kilimo cha migomba ni muhimu sana, hasa hasa kwa familia zetu masikini kwa kujipatia chakula na kilimo hicho kikifanikiwa kinaweza kuwa ni kilimo cha biashara, hata mimi nimeanza kupanda migomba hiyo nikimaliza kazi za huku Ulaya kwa kuwa Uraia wangu wa Tanzania sijaukana Mungu akitujalia uhai huu na mimi na mke wangu tutarudi nyumbani Tanzania kuja kula ndizi hizo.”

Huku akiomba nimuelekeza pahala pa kupata mbegu hizo. Ndugu huyu nilimuelekeza pahala zilipo huko Mahenge Ulanga Wilaya inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Ngolo Malenya.

Ndugu huyu akasema anavyowatazama watoto wake kurudi nyumbani Tanzania itakuwa ngumu mno kwani wameshakuwa wazungu.Nikamjibu ni kweli mtoto anayazoea maisha anayokulia kwa muda mrefu, kama ughaibuni anakuwa mghaibuni kama Ketaketa atakuwa Mketaketa.

Mazungumzo haya yaliendelea kwa muda huku akasema anaona Watanzania mmemteua Zuhura Yunus kuwa msemaji wa Ikulu yetu?.


Nikamjibu naam. Akaniuliza je unadhani anaweza kuifanya kazi hiyo vizuri? Nikamjibu kuwa huyu Zuhura binafsi simfahamu, ninachokitambua ni wajihi wake wa nje na namna anavyoyatamka maneno ya Kiswahili katika ripoti zake pekee.

Pale BBC Kiswahili watangazaji ninaowafahamu kwa kina na ukaribu ni wawili tu nao ni Bi.Mariam Omari na Bi.Soloma Kassimu.

Ndugu yangu huyu akaniambia Wafrika ambao wapo ughaibuni na hawajaukana uraia wa mataifa yao wanafuatilia mno maendeleo ya nchi zao maana huko wapo ndugu zao na hata wale walioukana uraia wao bado makaburi ya ndugu zao yapo Afrika, wengi wana moyo ywa kuwekeza Afrika kwa fedha na ujuzi walioupata huko. Nikamwambia njoni muwekeze mnangoja nini? Nikimuomba na yeye asiukane uraia wa Tanzania.

Ndugu huyu akampa simu yake mkewe ambaye ninamfahamu, nikamsabahi huku kwa kando nikisikia kelele za watoto wa ndugu huyu wakiongea.

“Shemeji nimekumbuka yale mapishi yako ya vitumbua na chapati za kumimina.” Nilimwambia shemeji yangu huyu, alicheka sana alafu akasema sasa ndugu yako nampikia yeye anakula kwa niaba yako.Nilimuomba ampikie vizuri.
Simu hiyo ikarudishwa kwa ndugu yangu huyu na mazungumzo naye yaliendelea. Ndugu huyu akasema kuna wakati BBC Swahili walikuwa na mtangazaji wao anayefahamika kama Hafsa Mosi aliachana na kazi na kuingia katika siasa za Burundi kwanza akawa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Msemaji wa Serikali ya Burundi kutoka mwaka 2005 hadi 2007, pia Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka mwaka 2009 hadi 2011 katika Baraza la Mawaziri la Rais Nkurunziza. Kisha alikuwa mjumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), akiiwakilisha Burundi, kutoka Juni 12, 2012, hadi Julai 13, 2016.

Ndugu huyu alinisimulia kilichotokea na lililomfika mwanamama huyu, msomaji wangu unaweza kulitafuta na ukalifahamu wewe mwenyewe. Muda wake wa Ubunge katika Bunge la EALA ungemalizika mnamo 2017 lakini hakujaliwa hiyo nafasi.

Ndugu huyu akasema hata Al Ustadh Karenga Ramadhani ambaye alifanya kazi na shirika hilo hilo katika idhaa zake za Kirundi, Kinyarwanda na Kiswahili tangu mwaka 1992- 1998 na baadaye DW Kiswahili na kurudi nyumbani kwao Burundi na kushika nyadhifa kadhaa katika serikali na vyama vya siasa alikumbana na changamoto nyingi.

Ndugu huyu alimtaja Tido Mhando akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, kuondolewa kwake na hadi kupelekwa mahakamani. Akisema kuwa mifano hiyo ni darasa kubwa linalojieleza.

Nikamuuliza kaka je? Wewe hauwezi kurudi nyumbani kuja kujenga nchi yetu? Akasema hilo kwake ni ngumu kwani namna kete zinavyosukumwa inahitaji moyo.

“Wafrika walio ughaibuni yale yanayaoendelea katika mataifa yao wanaona kama vile filamu inayochezwa. Niliposikia tu Mwanakwetu wameshamtumbua nikasema yale yale, nikapiga simu nikijiuliza kweli ndugu yangu huyu anapatikana? Nilipokupata nikasema ALHADU LILAHI RABBIL ALAMIIN.”

Mwanakwetu nikacheka sana alafu nikamuuliza ulikuwa unamaanisha nini katika haya maneno ya kiarabu? Akasema Anamshukuru Mwenyeenzi Mungu Mola wa Viumbe Vyote. Nikamwambia njooni tujenge mataifa yetu msiogope, mnayajenga mataifa ya watu wengine bure. Simu ilikatika.

0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news