Barabara ya Mpemba-Isongole kilomita 50.3 yakamilika, Waziri Mbarawa atoa wito

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amewataka wananchi wa Kata ya Msongole, Wilayani Ileje kuchangamkia fursa za kibiashara mara baada ya kukamilika kwa barabara ya Mpemba - Isongole (km 50.3) kwa kiwango cha lami ili kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (mwenye kofia), akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya (kushoto) na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe,Mhandisi Suleimani Bishanga (wa pili kulia) wakati alipokagua Daraja la Isongole linalounganisha Wilaya ya Ileje nchini Tanzania na Wilaya ya Chikota nchini Malawi, mkoani Songwe.(PICHA NA WUU).
Muonekano wa barabara ya Mpemba – Isongole (km 50.3) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Songwe.

Prof. Mbarawa ametoa wito huo alipokagua barabara hiyo inayounganisha nchi yetu na nchi ya Malawi ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilion 107.

"Moja ya matokeo makubwa ya kukamilika kwa barabara kwa wananchi wa wilaya hii na wilaya jirani ni ongezeko la biashara kati ya wilaya hii na Wilaya ya nchi jirani ya Malawi na haya ndiyo matarajio ya kila mmoja maana mpaka kipato kinaongezeka na ajira,"amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha ujenzi wa barabara hiyo ambayo imekamilika kwa asilimia 100 ambayo imeleta matunda ya haraka ikiwemo kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia mpaka wa Tunduma na maeneo mengine na hivyo kupelekea kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa kata ya Isongole, Wilayani Ileje mara baada ya kukagua barabara ya Mpemba – Isongole (km 50.3) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. Mkoani Songwe.

Prof. Mbarawa amefafanua kuwa ujenzi wa barabara nchini unahusisha gharama kubwa ambapo kilometa moja ni takriban shilingi bilioni 1.2 mpaka 1.6 hivyo ni jukumu la wananchi kuilinda miudombinu ya barabara hii ili iweze kudumu muda mrefu na kusaidia vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umesaidia ongezeko la magari ya biashara na hivyoo kupelekea kuvuka malengo yao waliojipangia katika ukusanyaji wa mapato.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (mwenye kofia), akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya, kuhusu mipaka ya Daraja la Isongole linalounganisha Wilaya ya Ileje -Tanzania na Wilaya ya Chikota nchini Malawi, wakati Waziri huyo alipoikagua barabara ya Mpemba – Isongole (km 50.3) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Songwe.

Aidha, amemuahidi Waziri huyo kuwa kuendelea kusimamia miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS),Mhandisi Suleimani Bishanga amemueleza Waziri huyo kuwa sasa TANROADS wanakalimisha kazi ya kuweka taa za barabara kwenye mji wa Isongole ili kuupendesha mandhari ya mji, kuongeza usalama, kurahisisha shughuli za kila siku na kuchochea biashara nyakati zote.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua na kuangalia shughuli za upimaji wa magari katika mzani wa Mpemba na kuagiza kufanyike tafiti za namna bora ya upimaji mizigo kwenye mzani ili kupunguza changamoto za faini kwa wasafirishaji.
Muonekano wa Daraja la Isongole linalounganisha Wilaya ya Ileje nchini Tanzania na Wilaya ya Chikota nchini Malawi ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

Waziri Prof. Mbarawa yupo mkoani Songwe ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara ikiwemo miundombinu ya barabara na mizani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news