Grumeti Fund inavyowaandaa vijana wa kiume wa kike watimize ndoto zao mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Grumeti Fund kupitia makongamano yake ya kuwawezesha vijana, limewataka vijana wa kiume mkoani Mara kujitambua na kusimamia ndoto zao ipasavyo na waache tabia hatarishi zitakazowafanya wasifikie malengo yao na pia washiriki kikamilifu kuwatetea, kuwasimamia watoto wa kike ili watimize ndoto zao.
Wameambiwa hatua hiyo itasaidia katika kuleta maendeleo na mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika jamii, kwani vijana wa kiume na vijana wa kike watatoa mchango wao sawa wenye manufaa makubwa ambao utakuwa na tija katika kuleta mageuzi chanya.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Shirika la Grumeti Fund, Frida Mollel ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza katika kongamano lililohusisha wanafunzi hao katika Wilaya ya Bunda na Serengeti mkoani Mara ambapo pia amewataka kuzingatia matumizi ya teknolojia kwa faida na kujipatia maarifa.

‘’Kwa nini tumeanza kuzungumza na wavulana, lakini zamani tulikuwa tunazungunza na wasichana, sababu kubwa ni kwamba, Grumeti Fund inajihusisha na uhifadhi na maendeleo ya jamii katika uhifadhi mojawapo ya shughuli inayofanyika ni utoaji wa ufadhili wa masomo. Tukiamini kwamba, baadae huwezi kuja kuwa jangili au kutegemea maliasili tu hivyo kupitia elimu tunayoitoa inakuwa na wigo mpana wa kuwasaidia kujiajiri,’’amesema Mollel.
Amesema, vijana wa kiume wana nafasi kubwa ya kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii hususan katika kupinga ukatili wa kinjisia na kuondoa mmomonyoko wa maadili, lakini pia wana nafasi ya kumtetea na kumsaidia mtoto wa kike ili kuleta usawa wa kinjisia ambao utasaidia kuleta maendeleo katika jamii na taifa pia.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo Mwalimu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt.Chris Mauki amewataka vijana wa kiume kubadili fikra zao sambamba na kupinga mila na desturi ambazo ni kandamizi na potofu lakini pia wawe mstari wa mbele kumsaidia, kumlinda na kumtetea mtoto wa kike kusudi afikie ndoto zake.
‘’Inaaminika kwamba, ukimuwezesha mtoto wa kike,ukimuendeleza mtoto wa kike unamtengeneza mtu wa kuja kushindana na wewe, yaani unaanda mshindani wako huo ni uongo. Badala yake, unamuandaa msaidizi,unamuandaa mtu wa kukushauri,'’amesema Dkt.Mauki.

Kwa upande wa wananfunzi waliohudhuria kongamano hilo wamelishukuru Shirika la Grumeti Fund kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kuwasaidia vijana wa kiume na wa kike katika mkoa wa Mara jambo ambalo linachangia wafike mbali zaidi katika kutimiza ndoto zao.

‘’Tumejifunza vitu vingi , ikiwemo kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii pamoja na kuwalinda watoto wa kike ambao kimsingi wana mchango mkubwa sana katika kuleta maendeleo na mabadiliko chanya kuanzia katika familia, jamii hadi katika taifa, na pia kuachana na mila na desturi ambazo hazina faida kama ukeketaji, bali zilizo nzuri tuziendeleze kwa manufaa yetu," amesema Peter Juma kutoka Shule ya Sekondari Bunda.

Makongamano ya watoto wa wa kiume yalianza mnamo mwaka 2021 na kuwafikia jumla wa wavulana 2,316 katika wilaya ya Bunda na Serengeti mkoani Mara katika shule 10.
Pia, makongamano ya kuwawezesha watoto wa kike yalianza mwaka 2017, ambapo watoto wa kike wameweza kufikiwa kutoka shule 19 za sekondari, ikiwa shule 12 za Serengeti na shule 7 za Wilaya ya Bunda.

Kupitia makongamo hayo yanayofanywa na Grumeti Fund jumla ya wasichana na wavulana wa Sekondari waliofikiwa ni 10,898. Ambapo wasichana waliohudhuria ni 8,582 na wote walipewa taulo za kike za kufua zinazotumika kwa muda wa mwaka mmoja, na jumla ya wavulana waliofikiwa ni 2,316.

Shule ambazo zimefaidika na makongamano hayo kwa Wilaya ya Serengeti ni pamoja Shule ya Sekondari Nyichoka, Shule ya Sekondari Serengeti, Shule ya Sekondari Mugumu, Shule ya Sekondari,Manchira, Shule ya Sekondari Ikoma, Shule ya Sekondari Sedeco, Shule ya Sekondari Robanda , Shule ya Sekondari Makundusi, Shule ya Sekondari Natta, Shule ya Sekondari Nagusi, Shule ya Sekondari Rigicha, na Shule ya Sekondari Issenye.
Huku upande wa Wilaya ya Bunda ni Shule ya Sekondari Chamriho, Shule ya Sekondari Hunyari, Shule ya Sekondari Sizaki, Shule ya Sekondari Kunzugu, Shule ya Sekondari Sazira, Shule ya Sekondari Bunda na Shule ya Sekondari Ikizu.

Post a Comment

0 Comments