HEKO TEMBO WARRIORS: Japan mmemalizana, Haiti wasifurukute leo

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Oktoba 6, 2022 timu ya Taifa ya watu wenye ulemavu ya Tembo Warriors itakuwa katika dimba la TFF Riva Facility jijini Instabul nchini Uturuki kumenyana na timu ya Haiti ikiwa ni mchezo wa hatua ya robo fainali ya Mashindano ya Kombe la Dunia ya Watu wenye Ulemavu 2022 yanayoendelea nchini Uturuki.
MAMBO YALIKUWA HIVI DIMBANI.

Tembo Warriors imefikia hatua hiyo Oktoba 5, 2022, baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Japan ambao waliupata katika mtanange uliopigwa katika dimba hilo.

Wakiwa katika Kundi E, Tembo Warriors imefika hatua hiyo baada ya kumaliza nafasi ya tatu hatua ya makundi wakiwa na jumla ya alama nne kisha wakaitoa Japan katika hatua ya 16 bora ya mashindano hayo. Ungana na mshairi wa kisasa, Lwanga Mwambande akushirikishe furaha ya wengi kupitia shairi hapa chini;


1.Waliketi na wakuu,
Wako matawi ya juu,
Ona wafanya makuu,
Heko Tembo Warriors.

2.Huko Kombe la Dunia,
Tumefika Tanzania,
Kwa kweli twajisikia,
Heko Tembo Warriors.

3.Sisi kule kuingia,
Kule Kombe la Dunia,
Tulikwishafurahia,
Heko Tembo Warriors.

4.Makubwa mwatufanyia,
Timu mnajipigia,
Mwatukosha twawambia,
Heko Tembo Warriors.

5.Hiyo Robo Fainali,
Jinsi mlivyo wakali,
Timu mnazikabili,
Heko Tembo Warriors.

6.Huku twawashangilia,
Tena twawasubiria,
Mkirudi Tanzani,
Heko Tembo Warriors.

7.Ahadi mlipokea,
Palilia endelea,
Punde mtazipokea,
Heko Tembo Warriors.

8.Serikali Tanani,
Yake Rais Samia,
Huko mwaifagilia,
Heko Tembo Warriors.

9.Robo mmeshafikia,
Nusu mwaifukuzia,
Ng’ang’ana twawaambia,
Heko Tembo Warriors.

10.Heri tunawatakia,
Mchezo naufwatia,
Muweze kutushindia,
Heko Tembo Warriors.

11.Mliketi na wakuu,
Mlipofanya makuu,
Ya sasa pia makuu,
Heko Tembo Warriors.

12.Tena mwaonyesha njia,
Wasioijua njia,
Waweze changamkia,
Heko Tembo Warriors.

13.Soka mnalijulia,
Sote twawakubalia,
Mmetuhakikishia,
Heko Tembo Warriors.

14.Ramani yetu mwaichora,
Duniani twawa bora,
Kote tutauza sura,
Heko Tembo Warriors.

15.Tena Yetu Royal Tour,
Mwazidi kuwastua,
Kwetu wapate kutua,
Heko Tembo Warriors.

16.Nyie matawi ya juu,
Mnatupa sikukuu,
Watajua wajukuu,
Heko Tembo Warriors.

17.Mmeonesha vipaji,
Timu zitawahitaji,
Wajipatie mataji,
Heko Tembo Warriors.

18.Serikali tumeona,
Na nyie inapambana,
Mema muweze kuvuna,
Heko Tembo Warriors.

19.Ushindi wenu hamasa,
Kwa wengi vijana hasa,
Mpira hawatasusa,
Heko Tembo Warriors.

20.Hapo mlipofikia,
Ushindi mejipatia,
Sote tunafurahia,
Heko Tembo Warriors.

21.Tupo tunafwatilia,
Dimbani mkiingia,
Tupate washangilia,
Heko Tembo Warriors.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments