IJP Wambura aunda timu mauaji Kilombero

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IJP Camillus Wambura metoa ufafanuzi juu ya tukio la mauaji yaliyotokea Oktoba 23, 2022 katika Kijiji cha Ikwambi kilichopo Kata ya Mofu, Tarafa ya Mgeta wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Mauaji hayo yalitokea wakati Jeshi la Polisi likiwa katika harakati za kuzuia uvunjifu wa amani ambapo walitutumia risasi za moto na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine wawili kujeruhiwa.
IJP Wambura ameeleza kuwa, chanzo cha tukio hilo ni kufuatia malalamiko ya wakulima dhidi ya wafugaji kwa vitendo vya kulisha mifugo yao kwenye mazao yao huku wakidai wakulima wawili kushambuliwa na jamii ya wafugaji Oktoba 22, 2022.

"Kutokana na malalamiko yao hayo, wananchi hao jamii ya wakulima waliamua kujichukulia sheria mkononi kwa kuwakamata viongozi wa kijiji hicho cha Ikwambi pamoja na Mkaguzi wa Kata hiyo na kuwafungia kwenye ofisi ya kijiji.

"Hali hiyo ilipelekea askari Polisi kufika eneo hilo wakiwa na lengo la kuwaokoa viongozi hao, lakini kulitokea fujo zilizosababisha matumizi ya risasi za moto pamoja na mabomu ya machozi na kusababisha mauaji ya watu hao wawili,"ameeleza IJP Wambura.

Wakati huo huo, kutokana na hali hiyo, IJP Wambura amesema kuwa, timu maalum imeundwa chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja taasisi zingine za Serikali kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi huru utakaowezesha kupata majibu ya chanzo cha tukio hilo.

"Na kikubwa ni kuibaini uwiano wa matumizi ya nguvu iliyotumiwa na Jeshi la Polisi katika kudhibiti vurugu hizo na ikiwa zilikwenda sambamba na vurugu zenyewe,"amesema.

Pia IJP Wambura amewataka wananchi wa Kijiji cha Ikwambi kuwa watulivu katika kipindi hiki huku askari waliohusika katika tukio hilo wakitakiwa kukaa kando ili kupisha uchunguzi.

"Natoa maelekezo mengine kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro, wahakikishe wanatoa ushirikiano mkubwa kwa timu hiyo ambayo inakwenda kufanya uchunguzi ili ukweli ubainike.Na endapo kutabainika mapungufu, madhaifu au chochote kinachoonyesha uzembe kwa yoyote basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,"amesisitiza IJP Wambura.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news