Mama Zainab aungana na Dunia kuadhimisha Siku ya Ulemavu wa Vichwa Vikubwa na Mgongo wazi Duniani

NA DIRAMAKINI

MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, leo amejumuika na wananchi mbalimbali wa Zanzibar katika Maadhimisho ya Siku ya Ulemavu wa Vichwa Vikubwa na Mgongo wazi Duniani.
Maadhimisho hayo yaliyoambatana na matembezi ya pamoja, yaliyoanzia katika Hospitali ya Mnazimmoja na kuishia katika Viwanja vya Mnara wa Mapinduzi, Kisonge Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, yameongozwa na Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui.

Mama Zainab ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Nuru ( Nuru Foundation) ya Zanzibar, ameshiriki maadhimisho hayo yaliyobeba Maudhui ya Kutoa Elimu kwa Jamii juu ya Ulemavu huo, yeye akiwa Mgeni Maalum.
Maadhimisho hayo yaliyoanza kwa shamrashamra mbali mbali tangu Oktoba 19 mwaka huu, yameandaliwa na Umoja wa Vichwa Vikubwa na Mgongo-Wazi Zanzibar (UVVMW) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, yamebeba kaulimbiu ya "Changamoto zangu zisifanye Mzazi wangu kutoa Uhai wake; Sote tuna haki sawa ingawa mahitaji tofauti".

Madhimisho hayo yaliambatana na shughuli mbali mbali ikiwemo burudani kutoka Chuo cha Mafunzo Zanzibar na mashairi, pia yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja Mhe. Rashid Simai Msaraka na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vichwa Vikubwa na Mgongo wazi Zanzibar ndugu Hassan Mohamed Saleh.

Post a Comment

0 Comments