Matokeo ya Mtihani wa Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa Darasa la Saba yatangazwa huku viongozi wa kiroho wakidaiwa kukosa maadili

NA DIRAMAKINI

VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kusimamia maadili na kujiepusha na vitendo vya aibu vinavyochafua taswira na maana halisi ya kuwa viongozi wa kiroho.
Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania,Sheikh Mussa Yusuph Kundecha (katikati),akitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba wa elimu ya dini ya kiislamu uliofanyika Septemba 14,mwaka huu.Kulia ni mwenyekiti wa taasisi ya Taasisi ya Islamic Education Panel.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Islamic Education Panel (IEP), Mohammed Kassim wakati utangazji matokeo ya mtihani wa Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa Darasa la Saba uliofanyika Septemba mwaka huu.

Amesema, kushuka kwa maadili nchini na kushamiri kwa vitendo vya ulawiti, ubakaji na usagaji, vimesababishwa na viongozi wanaosimamia maadili hayo, kutokuwa na maadili.

Mohammed amesema, viongozi wa dini watalazimika kurudi shule ili kupata maarifa ya namna ya kulea maadili, ili kukabiliana na tatizo la ukatili linaloikumba jamii kwa sasa.

Amesema, kinachotisha katika jamii ni kutokana na viongozi wa madhehebu mbalimbali wamekuwa wakihusika moja kwa moja kutenda katika vitendo hivyo ambapo wengine tayari wamefikishwa mahakamani.

"Viongozi wa dini wanabaki kuwa wanaadamu kama walivyo wengine, na wanaweza kukosa kama ilivyo kwa wengine. Pia wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa makosa kama wanavyochukuwa wanadamu wengine.
‘‘…isipokuwa tu ni jambo la kusikitisha kwa mtu ambaye ulimtegemea ndiye awe mwalimu wa kusimamia maadili, yeye akakosa maadili hayo au akwa msimamizi mbaya wa maadili hayo,’’ amesema Mohammed.

Akizungumzia matokeo ya Darasa la Saba katika Elimu ya Dini ya Kiislam mwaka huu amesema, jumla ya shule 3,710 katika mikoa 25 na Halmashauri 151 zilishiriki kufanya mtihani huo.

"Watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 163,143 na waliofanya mtihani walikuwa 142,522 sawa na asilimia 87.36 huku watahiniwa 20,621 wakishindwa kufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali.

"Idadi ya ya watahiniwa waliofaulu kwa kupata madaraja A hadi C ni 95,166 sawa na asilimia 66.77 ya watahiniwa wote. Aidha, watahiniwa waliopata daraja D na E ni 47,356 sawa na asilimia 33.23 ya watahiniwa wote," amesema Kassim.

Upande wake Amir Mkuu Baraza Kuu la Jumhiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha amesema, wanafunzi 3,567 wamefanya vizuri kwa kupata ufaulu wa alama A katika mtihani huo na kwamba ufaulu huo umeenda vizuri ikilinganishwa na mwaka jana.
"Shule 10 bora kwa kitaifa katika kundi la shule zenye watainiwa 20 au zaidi namba moja ni Mumtaaz ya Mwanza, Istiqaama ya Tabora, Rahma ya Dodoma, Algebra Islamic ya Dar es Salaam, Dumila ya Morogoro, Islamia ya Mwanza, Hedaru ya Kilimanjaro, Daarul Arqam, Mbagala Islamic na Maarifa Islamic zote za Dar es Salam." amesema Sheikh Kundecha.

Post a Comment

0 Comments